WAKATI timu Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga, inarejea rasmi kesho, imebainika kwamba mambo yatakuwa magumu kwa kila mmoja ili mapambano ya kujilinda na corona yaendelee.
Imebainika kuwa hata kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani, Joachim Low hataruhusiwa kuingia viwanjani kuangalia viwango vya wachezaji wake wa timu ya taifa.
Mechi zitapigwa bila ya kuwa na mashabiki viwanjani katika kujaribu kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19 na inaonekana kwamba sheria ni msumeno, haitamuacha mtu salama.
Hiyo inamaanisha kwamba Low hataweza kufanya skauti ya wachezaji wake kama Timo Werner, Kai Havertz na Serge Gnabry pale mechi za kimataifa zitakaporejea.
Low alikuwa akiiandaa timu ya taifa ya Ujerumani kuelekea kwenye fainali za Mataifa ya Ulaya kabla ya michuano hiyo kusogezwa mbele kwa miezi 12 hadi 2021.
Kurejea kwa soka la Ujerumani kutawapa fursa mashabiki wa soka duniani hatimaye kukaa mbele ya televisheni zao kushuhudia burudani waliyoikosa kwa muda sasa.