Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Katika makala hayo anapendekeza ziwepo fursa za kupata mikopo mikubwa inayolipika na ya riba ndogo kwa sekta binafsi na wataalam kutoka nje ili kuiendeleza Zanzibar kuweza kuwa eneo huru lililojikita hasa katika shughuli za kibenki, biashara kwa makampuni ya nje, bima, teknolojia ya habari na mawasiliano, utalii na shughuli nyengine za kifedha ‘La muhimu’ aliandika, ni kuwa mipango yote ya maendeleo na miradi mengine inatekelezwa kwa mashauriano makubwa na ushiriki mkubwa wa wataalamu mahiri wenye sifa wa kimataifa wenye kuheshimika duniani … waliofanya shughuli za kuzishauri serikali zinazotambulika na kufuatilika tokea huko nyuma (Rashid 2011 : 3).
 
Kwa maneno mengine anazungumzia washauri kutoka katika Shirika la Fedha la Kimataifa, Benki ya Dunia na serikali za nchi za magharibi ambazo zinazishauri nchi zinazopendelea Marekani katika bara lote la Afrika, na ambao Rashid angelipenda kuwaona wakiwa na dhamana ya kuinyonya ardhi ya Zanzibar na watu wake.

Rashid alipendekeza kuwa Zanzibar ishirikiane na Norway na Qatar kuhusiana na mafuta na gesi yake. Baada ya kuwashukuru wafadhili wakubwa wote, alimaliza kwa kuutaja hasa, mchango wa Marekani: ‘Marekani ikiwa ndiye mfadhili mkuu wa Zanzibar inaweza kutoa mchango wa kimkakati kwa kushirikiana na wafadhili wengine katika kuubadili uchumi wetu na mtindo wa maisha ya watu wetu’ (Rashid, 2011: 18).
 
Zanzibar itapata uhuru gani kama itakuwa na utiifu wa kiasi hicho kwa Marekani, ambayo huko nyuma ilihusika chini kwa chini kuleta Muungano? Zanzibar yenye kung’aa, chini ya mfumo huria mambo leo, ikiwa huru au isiwe huru, itautia utajiri mkubwa sana katika mikono ya wanasiasa wachache na walanguzi na kuyafanya maisha kuwa magumu zaidi kwa kila mtu, na hasa kwa wale wanaoishi katika maeneo masikini ya Visiwa hivyo. ‘Vijana wasioridhika na ambao wamekasirika’ walioainishwa na wanadiplomasia wa Kimarekani, ambao idadi yao imezidi kukua na ambao wengi wao sasa wanaiunga mkono asasi ya Uamsho, hawatakuwa wadau katika hali hiyo.
 
Babu angelifikiri nini juu ya mijadala hii?
Mwaka 1994 aliandika juu ya hali ya Muungano na uwezekano wa kuwepo mabadiliko. Naye pia alitaka kuwepo kwa Zanzibar iliyo huru iliyoungana na Bara kwa njia ya mkataba kwasababu, aliendelea kuandika, uhusiano wa hivi sasa ‘umeifanya Bara kujifanya kuwa … mlinzi wa mojawapo ya serikali mbaya sana ya kipinga maendeleo na yenye mtizamo finyu wenye kuangalia nyuma … Iliyozuia maendeleo ya elimu na uchumi ya wananchi’ (Babu, 1994: 32).
 
Alieleza kuwa Muungano umeinyima Zanzibar haki ya kujadiliana na kuingia katika makubaliano ya kiuchumi ambayo yangelikuwa na maslahi kwa Zanzibar pekee na si lazima kwa Bara, na kuiweka Zanzibar ‘chini ya uongozi wa chama cha siasa ambacho dira yake inaishia kwenye mitazamo ya wasiwasi wa kiusalama iliyopotoshwa na isiyoona mbali katika masuala ya maendeleo ya kiuchumi’ (Babu 1994: 32).
 
Udhibiti wa serikali kuu wa sarafu ya Zanzibar, Babu alieleza, umeinyima Zanzibar haki ya kuwa na sera huru ya fedha na sarafu yenye kufaa kwa mikakati yake yenyewe ya maendeleo. ‘kimbilio lisilokuwa na mpango kwenda kwenye mitambo ya uchapaji ili kuchapa fedha za kulipia upungufu usiokwisha wa Bara, siku zote umekuwa ukiingiza Zanzibar katika mifumko ya bei ambayo haikusababishwa na wao wenyewe na kuipa shida Zanzibar kuweza kuanza mipango yoyote ya kiuchumi na kijamii … Zanzibar lazima iwe na haki ya kujiamulia mambo yake wenyewe, kufanyakazi kwa ajili ya kuleta maslahi yaliyo bora zaidi kwa watu wa Zanzibar’ (Babu, 1994: 32).
 
Babu alikuwa na dira gani ya maendeleo ya kiuchumi ambayo ingeliyafikia maslahi haya? Mwaka 1996, wakati alipofariki, mafuta yaliyokuwepo Zanzibar hayakuonekana kuwa na tija kiuchumi, kwa hivyo hakuandika kuhusu mchango wa mafuta hayo kwa maendeleo ya Visiwani. Hata hivyo, mtazamo wake kuhusu maendeleo unaonesha kuwa asingelipenda kuona kuwa udhibiti wa mafuta hayo unakabidhiwa kwa ujumla wake kwa makampuni ya kimataifa. Aidha angelisisitiza kuwa sera ya uchimbaji huru wa kitaifa wa gesi na mafuta upo sio Venezuela tu bali pia Bolivia na Argentina.
 
Nchi hizi zimetumia mafuta na gesi kwa kujiletea maendeleo makubwa ya kisiasa na kiuchumi. Nchini Bolivia kwa mfano, katika kipindi cha miaka minne baina ya mwaka 2004 na 2009 hali ya kutokujua kusoma na kuandika iliondoshwa, kiwango cha vifo vya watoto kilipunguzwa kutoka 52.1 hadi 43.4 kwa kila vizazi hai 1,000 na utaratibu wa malipo ya kiinua mgongo ulianzishwa. Ardhi na madaraka yaligawiwa upya kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 500. Mengi ya haya yalilipiwa kwa mapato ya mirabaha kutoka katika mafuta na gesi (Taylor, 2009: tradingeconomics, 2013).
 
Dira ya Babu, inatoa hoja kuhusu Zanzibar ambayo ingeliweza kuwa. Lakini pia inaweza kuwa ni Zanzibar ya siku za mbele. Katika hali ya kushindwa kwa mfumo huria mambo leo na mateso ya unyonyaji wa kikatili wa ubepari unaoporomoka, mawazo kama ya Babu hivi sasa yana umuhimu mkubwa zaidi kuliko wakati mwengine wowote wa hapo kabla. Yanadurusiwa tena na wale wote wanaotaka ukombozi kutokana na ubeberu na haki ya kiuchumi. Labda hapo baadae yatasaidia kuwepo kwa Zanzibar ya kisoshalisti iliyo tofauti.
 
Na kama kwa juu juu tu, Zanzibar imebadilika, kama unavyoonyesha waraka niliounukuu katika kitabu hiki, leo, katika maendeleo ya kisiasa ya kila siku, na mara nyingi yakisimamiwa na kuangaliwa kama ilivyokuwa katika miaka ya vita baridi, na wawakilishi wa kijeshi na kiuchumi – walio tayari kuingilia kati moja kwa moja ikiwa njia nyengine yoyote itashindwa.


Maoni ya Babu, yaliyoandikwa miaka 40 iliyopita katika sehemu za mwisho ya utangulizi wake katika kitabu cha Walter Rodney How Europe Underdeveloped Africa, bado yanafaa hadi hivi leo:

 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…