Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

TISHIO LA UKOMBOZI​
Siku za Awali za Mapambano Dhidi ya Ukoloni
Kipindi cha katikati ya miaka 1950 na mwanzoni mwa miaka ya 1960, wakati masimulizi haya yanapoanzia, kilikuwa na mambo mengi yanayofanana na yale ya hivi sasa. Katika bara la Afrika, Marekani na Uingereza walifanya kila juhudi ili kuleta ‘mabadiliko ya utawala’ na kuziweka madarakani serikali ambazo wangeliweza kuzichezea akili na kuzitumia kwa maslahi yao. Walitumia mbinu za chini kwa chini na itikadi za vitisho na kutia wahaka watu na kuanza kuwatafuta wachawi – lakini wakati huo ilikuwa dhidi ya makomunisti, na si ‘magaidi wa kiisilamu’.
 
Katika mpango wao wa kuendelea kuzinyonya nchi za Afrika (wakati huo nyingi zikiwa ndiyo kwanza zimepata uhuru au zinapambana na ukoloni), Zanzibar ilionekana kuwa ni pahala muhimu. Marekani waliiona kuwa ni sehemu ya ukanda wa Afrika ya Kati ambayo kama itadhibitiwa, itailinda sehemu ya Kusini mwa Afrika (pamoja na mali iliyowekezwa na nchi za magharibi) dhidi ya ushawishi wa wapenda maendeleo na masoshalisti wa nchi kama zile za Algeria na Ghana. Kama Zanzibar ingelitoka nje ya mzunguko huu, walikuwa na hofu kuwa na Afrika yote ingeliifuata.
 
Zanzibar ilikuwa, na bado ni sehemu muhimu mashuhuri. Kituo kikubwa cha biashara kwa miaka elfu mbili ikiziunganisha Afrika na Asia na rasi ya Arabuni. Imekuwa, kama ilivyokuwa hapo zamani, kituo cha mchanganyiko wa watu wa mataifa mbalimbali ya dunia.
 
Mwanahistoria Abdul Sheriff anaelezea kwa hisia mji wa Zanzibar jinsi ulivyokuwa wakati wa utoto wake, mwanzoni mwa miaka ya 1950, alipokuwa akicheza katika barabara nyembamba zenye vichochoro pamoja na watoto wenye asili ya kiswahili, ya kiomani, ya kiajemi, ya kihadhrami au ya kihindi, na jinsi kila upepo wa musimu (monsoon) ulivyoshuhudia kuwasili kwa ‘majahazi na mabaharia kutoka Arabuni, Ghuba ya Uajemi, Bara Hindi na Somalia … bandari vile vile ilijaa majahazi kutoka Lamu na Kilwa. Ulikuwepo mwingiliano mkubwa wa watu’ (Sheriff, 2008)
 
Taswira hii ya mchanganyiko wa utamaduni wa aina mbalimbali ilidhihirisha pia kuwepo kwa mapambano makali dhidi ya ubeberu yaliyotokana na uzoefu uliopatikana wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kujenga mwamko wa wananchi kuwa na hisia na nchi yao; na wanamapinduzi wengi wa miaka ya 1950 na 1960. Wakati wa vita, kama alivyoandika Abdulrahman Mohamed Babu:

 
Zanzibar: Ukabila, Matabaka na Mzuka wa ya Zamani
Vipi mfumo wa kijamii wa visiwa hivi umeumbika? Kuanzia miaka ya 1830 na kuendelea, vilitawalia na koo za Masultani, ambao ijapokuwa asili yao ni Oman, walilowea Zanzibar, wakaoana na wenyeji, wakisema Kiswahili na ilipofika katikati ya karne ya 20 hata hicho Kiarabu hawakukijua tena. Zaidi ya hayo, kwasababu ya pale ilipo, mahali pa aina ya pekee, Zanzibar ilikabiliana na mfululizo wa uvamizi wa wakoloni wa Kireno, wa Oman, Wajarumani na Wafaransa, na hatimaye, mwaka 1890 Waingereza.
 
Kwa kiwango fulani, ilikuwa ni kwasababu ya matokeo ya matukio hayo ya kikoloni ndiyo maana Zanzibar ikawa ni jamii iliyogawika kwa migogoro, ikiwa na umoja madhubuti wa kiutamaduni kwa upande mmoja, na migawanyiko mikubwa ya kikabila kwa upande mwengine; migawanyiko ambayo mzuka wake bado unavitisha visiwa hivi hadi hivi leo.

Historia ya Zanzibar, ikiwa ni kituo kikuu cha biashara, na ukweli kuwa ilikuwa ndiyo njia ya kuingizia na kutolea bidhaa kutoka ndani ya bara la Afrika, iliisababishia kuwa ndiyo njia ya kupatia na kusafirisha watumwa, ijapokuwa idadi ya watumwa hao ilikuwa ni ndogo sana ukilinganisha na ile ya biashara ya watumwa waliokuwa wakisafirishwa kuvuka bahari ya Atlantic[1]. Wakati huo huo, kukua kwa mahitaji ya nchi za kibeberu visiwani katika karne ya 19 kulisadifu kutokea pamoja na kuingizwa kwa zao la karafuu nchini Zanzibar.
 
Maendeleo yaliyofuatia ya kuwepo kwa mfumo wa mashamba makubwa yaliathiri sana mahusiano ya kiuzalishaji visiwani. Watumwa waliokuwa wakichukuliwa kutoka bara hawakuwa tena bidhaa ya biashara ya pekee lakini badala yake wakawa nguvu kazi ya uzalishaji mashambani’ (Depelchin, 1991: 14). Wakati huo Zanzibar ilikuwa ni jamii yenye mfumo wa utumwa, na iliendelea kuwa hivyo mpaka utumwa ulipoondolewa Unguja na Pemba mwaka 1897.
 
Awamu hizi zilizofuatana za historia ya Zanzibar zimekuwa na athari kubwa na ya kudumu visiwani. Historia ya utumwa ilikuwa na maana kuwa kila mmoja alionekana, na wengi walijiweka katika makundi ya ama ‘Waarabu’ au waliohusiana na ‘Waarabu’ na waliokuwa wakimiliki watumwa na kwa hivyo Mabwana (mabwana waliokuwa na kila fursa) au Waafrika waliokuwa watumwa waathiriwa wa Mabwana. Hata hivyo, juu ya kuwepo kwa mivutano hii, katika kipindi cha kabla ya ukoloni wa Kiingereza hapajawahi kutokea mgogoro mkubwa wa kikabila.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…