JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha linamshikilia mtu mmoja kwa tuhuma za kuendesha kiwanda feki cha kutengeneza pombe kali inayowekwa kwenye chupa inayofanana na ya Konyagi na kuziuza katika maeneo mbalimbali mkoani humo.
Akizungumza na chombo kimoja cha habari nchini, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Justine Masejo, amethibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kueleza uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kubaini mtandao wote wa watengenezaji wa Pombe hiyo.
Watuhumiwa hao walikamatwa juzi baada ya wananchi kuwafikishia taarifa polisi, waliposhuhudia kwa siku kadhaa vinywaji hivyo vikitoka katika nyumba hiyo iliyopo eneo la Elerai jijini humo.
Kwa upande wake, Balozi wa mtaa wa Kware kata ya Elerai, Ngoskeki James Meirura, amesema kabla ya kukamata vinywaji hivyo, alipokea taarifa ya kuwapo kwa kiwanda bubu, ndipo alipopeleka taarifa kwa Mwenyekiti wa Mtaa na kisha kwa Jeshi la Polisi.