Siku chache baada ya Mbunge wa Sengerema, Khamis Tabasamu (CCM), kuanika kisa cha kutishiwa kuuawa, ni vema tukatafakari kwa kina sababu za kutokea hali hiyo.
Akiwa bungeni wiki iliyopita wakati akichangia Bajeti ya Wizara ya Nishati, Tabasamu aliibua madai kwamba baada ya kushauri uwekaji wa vinasaba kwenye mafuta ufanywe na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), alipigiwa simu za vitisho
Baadaye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, akakiri kupata taarifa hizo akisema: “Jeshi la Polisi linazifanyia kazi; linaendelea kufuatilia uhalisia wa madai hayo.”
"Kama kweli jambo hilo lipo, waache mpango huo kwani si tu unakiuka misingi ya amani na usalama, bali unaingilia uhuru wa wabunge kutoa maoni yao kwa masilahi ya taifa na wananchi,” anasema Simbachawene
Akizungumza katika viwanja vya Bunge, Tabasamu anasema alipigiwa simu za vitisho baada ya kuzungumzia umuhimu wa fedha nyingi zinazolipwa kwa kampuni binafsi kwa ajili ya kuweka vinasaba kwenye mafuta, akitaka ziende kwenye taasisi za serikali.
"Wanadhani ninapanga kuanzisha mapambano nao. Nimewahi kuleta hoja bungeni kwamba suala hili (la kuweka vinasaba kwenye mafuta) linatakiwa kufanywa na taasisi ya umma, si kupewa mtu binafsi. Ni gharama kubwa sana.
"Sasa ninafikiri Spika amenielewa. Inabidi kuharakisha. Ametoa maelekezo sheria iletwe bungeni haraka, ndani ya siku 30, tuipitishe ili sasa uwekaji vinasaba iwe kazi ya taasisi ya serikali,” anasema Tabasamu.
Anaitaka serikali itengeneze vinasaba vyake badala ya kutegemea vinasaba kutoka nje, akionya kuwa ni hatari kubwa kumpa kazi mtu binafsi ambaye hata hajulikani kufanya kazi hiyo, kwa hoja kwamba vinaweza kutumika kukwepa kodi.
Spika ameahidi kulifuatilia, huku Simbachawene pia akifuata nyayo za Spika; kulifuatilia suala hili kwa karibu ili kupata taarifa ni akina nani wametoa vitisho hivyo.
Leo hii baada ya kubadilishwa kwa kanuni na taratibu za nani awe kiongozi, tumeshuhudia wabunge wengi wakiwa pia ni wafanyabiashara, hususan biashara ya mafuta; ambayo ni kitovu cha ustawi wa maisha ya watu.