Kwa ufupi 35: Umri wa bwana harusi Ally Kimbunga. 60: Umri anaotajwa kuwa nao bibi harusi Asha Abdallah ‘Binti Dulla’. Dar es Salaam. Hayawi hayawi sasa yamekuwa, ndivyo unavyoweza kusema, baada ya Asha Abdallah maarufu Binti Dulla anayesadikiwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 60, mkazi wa Mburahati Madoto kuolewa na Ally Kimbunga (35). Ndoa hiyo ilifungwa jana saa saba mchana nyumbani kwa Binti Dulla ikishuhudiwa na watu wengi ambayo ilitanguliwa na sherehe iliyoambatana na ngoma siku mbili kabla ya kufungwa. Ndugu katika familia ya bibi harusi, Hamisi Kondo alimwambia mwandishi wetu kuwa hiyo ilikuwa ni ndoa ya nne kwa dada yake na kwamba, waliomuoa awali walishafariki dunia. “Sasa hivi hana watoto, aliwahi kuwa na mmoja ila ikawa si riziki kwa kuwa alifariki akiwa na miaka mitatu,” alisema Kondo ambaye mama wa Binti Dulla ni shangazi yake. Kudra Saidi aliyewahi kuwa mpangaji nyumbani kwa Binti Dulla kwa miaka 12 tangu 1990 ambaye alihudhuria ndoa hiyo alisema majirani walipomfuata kuzungumza naye kuhusu kuolewa aliwaeleza kuwa hata Mtume Muhammad (SAW) alioa mwanamke aliyemzidi umri. Kudra alisema baadhi ya watu wamekuwa wakidai kwamba mume wa Binti Dulla amefuata nyumba na kwamba mama huyo hana haja ya kupata mtoto. Hata hivyo, Binti Dulla alisema maneno yanayozungumzwa kuhusu ndoa yake ni wivu wa baadhi ya watu katika maisha aliyoyachagua. “Wazushi tena hao ni mashilawadu (wambeya) kwa kuwa walijua sitafanikisha. Kuhusu suala la mtoto sina haja ya kupata mtoto kwa kuwa nia yangu ni kuolewa na kuwa na mume, Mungu amefanikisha hilo, Alhamdulillah Rabil-alamin,” alisema