Zanzibar yatoa changamoto kwa Tanzania Bara
MAFANIKIO ya Zanzibar katika mapambano dhidi ya malaria ni changamoto kubwa kwa Tanzania Bara dhidi ya ugonjwa huo unaoongoza kuua watu nchini.
Hayo yalisemwa Jumatano wiki hii na Rais Jakaya Kikwete, alipokuwa akizungumza katika mkutano wake na viongozi wa Kituo cha Maendeleo ya Kimataifa (CGD) jijini hapa.
Alisema changamoto kubwa iliyo mbele ya wananchi wa Tanzania Bara kutokana na mafanikio hayo ni kuhakikisha kuwa malaria inatokomea na kuacha kuwa muuaji kiongozi wa watu nchini.
Akipongeza hatua iliyofikiwa na Zanzibar katika mapambano hayo, Rais ambaye yuko katika ziara yake ya kwanza ya kikazi nchini Marekani, alisema njia pekee ni ya kutumia vyandarua vilivyowekwa dawa, unyunyiziaji sumu ya mbu katika mazalia na dawa za kupambana na malaria.
"Ni kweli kuwa Zanzibar ikilinganishwa na Tanzania Bara ni ndogo na yenye idadi ndogo ya watu na hivyo kuwa rahisi kufikia mafanikio hayo, lakini tunaweza kwa upande wa Bara tukaanza na sehemu ndogo ndogo hadi mafanikio yapatikane," alisema Rais.
Alisema Serikali yake imepanga kutangaza hatua madhubuti za kupambana na malaria ifikapo Oktoba mwaka huu, huku akiitaka Zanzibar kuhakikisha inalinda mafanikio hayo, kwa kutoruhusu wadudu wa malaria kuingia kisiwani humo.
Aliipongeza Serikali ya Marekani kwa mchango wake mkubwa uliowezesha Zanzibar kufikia hatua hiyo ya mafanikio hayo ambapo mwaka 2005 iliweza kupambana na malaria na kubakiwa na maambukizi kwa asilimia 25 na mwaka huu maambukizi ni asilimia moja tu.
Naye Balozi wa Marekani nchini, Bw. Mark Green, alisema ili mapambano hayo yafikiwe katika nchi yoyote inayotishiwa na ugonjwa huo, kinachotakiwa ni dhamira ya dhati na raslimali.
"Kinachotakiwa ni wanawake na watoto kutumia vyandarua vyenye dawa, nyumba zinyunyiziwe sumu ya mbu, wajawazito watibiwe na huduma ya afya iwe ya kuridhisha kwa jamii," alisema Bw. Green ambaye anafuatana na Rais Kikwete katika ziara hiyo ya siku tatu.
Wengine katika ziara hiyo, ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Elimu, Ufundi na Mafunzo ya Amali za Taifa, Bw. Haroun Ali Suleiman.
Source:
Majira