Vigogo wengine BoT kortini wadaiwa kusababisha hasara ya Sh104 bilioni
Pauline Richard na Salim Said
VIGOGO wanne wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi, ikiwemo la kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh104 bilioni katika mkataba wa uchapishaji wa noti.
Kufikishwa mahakamani kwa vigogo hao kumekuja siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kutangaza kuwa kuna kesi tatu zitafikishwa mahakamani wakati wowote dhidi ya vigogo, ikiwa ni mwendelezo wa vita dhidi ya ufisadi.
Tayari maofisa wa BoT wameshafikishwa mahakamani kwa tuhuma za kufanikisha wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) na matumizi mabaya ya ofisi yaliyosababishia serikali hasara katika ujenzi wa majengo ya maghorofa pacha ya makao makuu ya taasisi hiyo ya fedha.
Tofauti na kesi hizo za awali, watuhumiwa hao wanne wa jana wameshtakiwa chini ya sheria ya uhujumu uchumi ya mwaka 2002.
Wakurugenzi hao wameshtakiwa kwa makosa tofauti, likiwemo la kupandisha gharama za uchapishaji noti tofauti na gharama za awali zilizo kwenye mkataba mkuu na kusababisha hasara hiyo.
Waliofikishwa mahakamani jana ni Simon Jengo, ambaye ni mkurugenzi wa huduma za benki wa BoT, Kisima Thobias Mkango (kaimu mkurugenzi wa fedha), Bosco Kimela (kaimu mkurugenzi wa huduma za sheria) na Ali Farjalah Bakari, ambaye pia ametajwa kuwa ni mkurugenzi wa huduma za benki.
Mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Benny Lincon alimwambia hakimu Samuel Maweda kuwa vigogo hao wanne, wakiwa watumishi wa umma walitenda makosa hayo kwa nyakati tofauti na kuisababishia serikali hasara ya Sh 104,158,536,146.
"Kwa pamoja na kwa makusudi na kwa kushindwa kuchukua tahadhari au kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa njia inayoeleweka, waliandaa bila ya kuwa na sababu nyongeza katika mkataba wa mwaka 2001 wa gharama za juu zaidi katika uchapishaji noti kuliko ilivyokuwa kwenye mkataba mkuu na hivyo kuisababishia serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasara ya Sh104,158,536,146, " alidai Lincon.
Lincon aliendelea kuieleza mahakama kuwa mwaka 2004 washtakiwa Jengo na Mkango, wakiwa ndani ya jiji na mkoa wa Dar es Salaam na wakiwa wameajiriwa katika utumishi wa umma katika nyadhifa tofauti BoT, kwa pamoja na kwa makusudi, wakiwa na ufahamu na nia ya kupotosha ukweli.
Alidai kuwa watu hao kwa pamoja walifanya mahesabu ya bei kabla ya ofa iliyotolewa na msambazaji wa noti katika nyongeza ya nyaraka za mkataba wa mwaka 2004 kwa kurejea bei iliyokuwepo kwenye mkataba wa mwaka 2001 na kuituma idara ya sheria kwa ajili ya kuangaliwa upya, kitu ambacho kwa ufahamu wao kililenga kumpotosha mkuu wao.
Aidha Lincon alidai kuwa mwaka 2005, Jengo akiwa ndani ya mkoa wa Dar es Salaam na mfanyakazi wa BoT katika wadhifa wa mkurugenzi wa huduma za benki, alimpotosha mkuu wake kwa kuomba kuchapwa kiasi kikubwa cha noti za benki katika mkataba wa nyongeza wa 2005, ikilinganishwa na mkataba uliotengenezwa na kitengo cha mtumiaji, akijua anafanya hivyo kwa lengo la kumdanganya mkuu wake.
Wakili wa upande wa utetezi, Mpale Mpoki alidai baada ya kusomewa mashtaka hayo kuwa kesi hiyo imefunguliwa mahakamani hapo kimakosa kwa kuwa mahakama ya wilaya, haina mamlaka ya kisheria kusikiliza kesi kubwa kama hiyo.
Alisema kwa vile washitakiwa wote wanne wanadaiwa kuwa walifanya makosa hayo wakiwa watumishi wa BoT na hawakufanya hivyo kwa nia mbaya, sheria ya kuanzishwa kwa benki hiyo inawapa kinga ya kutoshtakiwa.
Alidai kuwa kifungu namba 65 cha sheria ya ya BoT, kinawalinda maofisa wake kushtakiwa na kwamba kama kutatokea mkanganyiko wa kisheria, kifungu cha 68 cha sheria hiyo, bado kinawalinda.
"Mheshimiwa hakimu sheria hii ya BoT iliyotungwa na wataalamu, kifungu cha 68 kinasema kama kutatokea mkanganyiko wa kisheria, basi sheria ya BoT inapaswa kufuatwa na kuachwa sheria nyingine," alisema Mpoki.
"Kifungu cha 65 cha sheria ya kuanzishwa kwa Benki Kuu kinasema: bila ya kujali sheria nyingine zote isipokuwa katiba ya nchi, sheria ya BoT ifuatwe iwapo kutatokea mkanganyiko wa sheria. Hivyo basi kesi hii iliyoletwa chini ya kifungu cha 29, haiondoi kinga ya wateja wetu."
Hoja ya wakili Mpoki iliungwa mkono na wakili mwenzake wa utetezi, Mabere Marando ambaye alimwomba hakimu kuwaachia huru wateja wao kwa sababu hawana kesi.
Alisema washtakiwa hao hawana kesi kwa kuwa walikuwa na kinga ya utumishi wa BoT na kwamba hawakufanya hivyo kwa nia mbaya.
"... kwa hiyo mheshimiwa hakimu, mahakama yako haina mamlaka ya kisheria kusikiliza kesi hii na kwa mujibu wa sheria ya BoT, si kuisikiliza tu bali hata kuipokea kwake ni ukiukwaji mkubwa wa sheria," alisema Marando.
"Naiomba mahakama yako isome vizuri vifungu mbalimbali vya sheria na hatimaye inawe mikono na kuwaachia huru wateja wetu kwa kuwarudishia Takukuru kesi yao, ili watafute watu wengine wa kuwashitaki kwa sababu hawa hawahusiki kwa vile wote walikuwa watumishi wa BoT. Tunaomba warudi wakaendelee na utumishi wao."
Akijibu hoja hizo, Hakimu Maweda alipinga hoja ya watuhumiwa hao kuachiwa huru na kusema kesi hiyo imepokelewa mahakamani hapo kwa ajili ya maandalizi ya kuipeleka Mahakama Kuu baada ya kukamilika kwa upelelezi.
Awali mwendesha mashitaka huyo wa Takukuru alidai kesi hiyo imefunguliwa kwa kifungu namba 29 cha sheria ya uhujumu uchumi kinachotoa fursa kesi zote za uhujumu uchumi kuanzia mahakama za wilaya kabla ya mahakama za ngazi ya juu zaidi.
"Sheria inaturuhusu kuanzia mahakama ya wilaya na baada ya upelelezi kukamilika kesi hii itahamishiwa katika mahakama za ngazi ya juu zaidi zenye uwezo wa kusikilzia kesi za uhujumu uchumi," alifafanua Lincon.
Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo na kurudishwa rumande hadi Septemba 18 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.
Source: Gazeti la Mwananchi