SoC04 Vijana Ajira Village: Mfumo rahisi wa kuisaidia serikali kutatua changamoto ya ajira kwa vijana wa Kitanzania

SoC04 Vijana Ajira Village: Mfumo rahisi wa kuisaidia serikali kutatua changamoto ya ajira kwa vijana wa Kitanzania

Tanzania Tuitakayo competition threads

mapuno

New Member
Joined
Jun 16, 2024
Posts
3
Reaction score
0
CHANGAMOTO KUU : Zaidi ya vijana 885,000 wanaohitimu masomo vyuoni kila mwaka hawana Ajira, Mbaya zaidi jamii zetu tunazotoka bado zina matatizo makubwa kama usosefu wa nishati bora, magonjwa yanayozuilika, Ukosefu wa vyoo safi, ukosefu wa chakula, mbinu mbovu za uzalishaji, ubovu wa miundombinu, Uhaba wa Maji, na ukosefu wa elimu yenyewe kwa wadogo zetu.

Matatizo yote haya na mengineyo mengi yangeweza kutatuliwa na elimu zetu katika jamii zetu. Mbaya zaidi na zaidi tunakufa na elimu zetu jamii ikiendelea kuishi na matatizo yaleyale kwa sababu ya kukosa mfumo bora na rahisi wa kutatua changamoto za jamii kupitia elimu iliyozalishwa na kupandikizwa kwa vijana wao waliowapeleka chuo. Wahitimu wengi wanahitimu chuo na kwenda viijijini mwao wakiwa hawana ajira na hivyo kwenda kuendelea kusubiria ajira kutoka serikalini ambayo hawajui itakuja lini. Wachache hubaki mjini kutafuta maisha wakizicha jamii zao bila mabadiliko miaka na miaka. Jukumu la kupeleka mabadiliko limebaki ni la serikali na jamii yenyewe. Mwaka 2016 Nilihitimu masomo ya chuo kikuu nikiwa na matumaini ya kuwa nitapata Ajira. lakini mpaka sasa sina matumaini hayo tena.

Ni kweli ni wajibu wa serikali na sekta binafsi kutuajiri lakini kwa kasi ya ukuaji wa idadi ya watu inavoongezeka ni ngumu kufikiri ya kwamba serikali itatuajiri vijana wote tuliomaliza vyuo vikuu na vyuo vya kati. Pia ikumbukwe Matatizo yetu mengi kwenye jamii tunashindwa kuyatatua kwasababu ni serikali ndio ina wajibu na inapeleka njia ikizani kwamba hiyo ndio changamoto kuu ambayo wananchi wangependa kutatuliwa bila kuhusisha wananchi au vijana wenyewe. Matokeo yake jamii zetu zinaendelea kuwa na matatizo yaleyale kila siku bila suluuhisho la kudumu.

VIJANA AJIRA VILLAGE: Ni Mfumo rahisi kwa jamii na wahitimu kutengeneza Ajira pamoja kupitia changamoto za jamii husika. Kupitia mfumo huu, Jamii zenye changamoto zinajisajiri kupitia serikali za mitaa, changamoto hizo zinaweza kuwa ukosefu wa shule, maji, chakula, mbolea, nishati, afya, nk. Kupitia mfumo huu wahitimu watajisajiri kupitia vijiji, kata au wilaya zao. Wahitimu kutoka sehemu hizo na jirani watachagua Changamoto wanazohitaji kuzitatua kupitia kura ya jamii ambapo wananchi watapigia kura mipango bora na endelevu zaidi ambayo wananchi wangependa kuiona katika jamii zao kulingana na matatizo waliyonayo.

Wananchi watashiriki pamoja na vijana wao kuendeleza jamii zao. Kupitia mfumo huu wananchi watakuwa ndio wanaoamua ni matatizo gani ni ya kipaumbele kwao na yawe ya kwanza kutatuliwa, Matatizo ya jamii yataorodheshwa na kupigiwa kura katika mkutano wa kijiji au jamii. Matatizo machache yenye kipaumbele kila mwaka yatakuwa yanatangazwa kwa wahitimu na wanafunzi kushiriki kuzisaidia jamii zao. Kijiji au jamii husika itaandaa mkutano kati ya wahitimu/wanafunzi na wananchi ili kuwapa nafasi wahitimu kutoa mipango yao kwenye jamii zao.

Mipango bora itasajiliwa na jamii na mamlaka husika ili kujengewa uwezo wa kupata fedha kwaajili ya utekelezaji. Mradi utakuwa wazi kwa wananchi wote kwa ushiriki kikamilifu katika utekelezaji wake. Mfumo utawaiwezesha serikali kutambua matatizo gani yana umuhimu mkubwa kwa wananchi na hivyo kuisadia pia kujua ni miradi gani iwe ya kwanza kutokana na mahitaji ya wananchi husika. Serikali, Mashirika yanayotatua changamoto katika jamii kama ukosefu wa Ajira, elimu, Nishati, Afya, nk pamoja na Wadau mbalimbali wataweza kusupport vijana kwa vijana kupitia mfumo huu wa Ajira na hivyo kuweza kutatua changamoto kwa kugusa jamii iliyokusudiwa moja kwa moja.

KUANZA NI RAHISI
Sio lazima, kuanza kwa jamii zote nchini mara moja, njia nzuri ni kuanza na jamii chache zenye changamoto ambazo zinaweza kutatuliwa na wahitimu. Tunaweza kuanza na jamii/kijiji kimoja, viwili, vitatu au vitano nk. Kwamfano, Tunaweza kuamua kuanza na sekta ya elimu, kuna wahitimu wengi waliosoma Elimu ambao hawana Ajira na kuna baadhi ya maeneo bado hayana miundombinu bora ya elimu kama ukosefu wa shule, ukosefu wa walimu. Tunaweza tukaanzia huko. Tunaweza pia tukaanza na kilimo kwavile Taifa linaandaa dira na moja ya malengo ni Taifa la Tanzania Kulisha bara la Africa.

MFANO HAI:

Vijana Ajira Village.jpg

Picha
: Muitikio mkubwa wa wanachi katika kijiji cha Ugano, mkoani Ruvuma, Vijana wahitimu wa chuo wakiwasilisha mipango yao kwa jamii zao zilizowatuma chuoni na badae kupigiwa kula, vijana 3 walifanikisha kuanzisha shule, vijana 4 walifanikisha kuanzisha kiwanda kidogo cha kuchakata kahawa na wengine kuanzisha kiwanda cha uzalishaji mbolea malighafi kwaajili ya kusaidia wananchi kuboresha uzalishaji katika sekta kilimo.

FAIDA ZA MFUMO WA "VIJANA AJIRA VILLAGE"
-Mfumo unaweza kuunganishwa na teknolojia ya tovuti na simu kuwaunganisha wahitimu na jamii zao pamoja
-Msomi atasaidia jamii yake, atatatua changamoto ambazo hazijapatiwa ufumbuzi kwa muda mrefu
-Mfumo huu unaweza kutumiwa na serikali, mashirika na makampuni yanayotatua matatizo kwenye jamii zetu kuwagusa wananchi moja kwa moja.
-Vijana wengi waliohitimu watapata Ajira, kujiajiri na kuajiri wengine ikiwemo vijana ambo
hawakupata bahati ya kwenda vyuoni.
-Wanawake Kwenye Jamii husika nao watapata Ajira kupitia miradi inayoibuliwa na vijana moja
kwa moja kwenye maeneo yao.
-Serikali itapata msaada wa kupunguza gharama ya kuanzisha miradi inayogusa jamii
-baadhi ya miradi inaweza kuwa ya kiserikali na vijana kuunganishwa na ajira ya moja kwa moja ya
serikali kupitia Jamii zao.
-Miradi itayodhaminiwa na kusajiliwa,serikali itaweza kupata kodi na utaratibu wa kawaida wa urejeshaji deni la
mkopo utaendelea kupitia mishahara ya walioajiriwa kwenye miradi endelevu ya serikali.

MAOMBI KWA SERIKALI
Siku zote serikali yetu imekuwa ikitusisitiza vijana tujiajiri, lakini haijaandaa mfumo bora wa sisi kujiajiri.

-Serikali itambue mfumo huu kama njia mdadala ya vijana kujiajiri.
-Serikali za mitaa ziorodheshwe changamoto zake kuu zinazoguza watu ili wananchi wachague zipi wanahitaji zianze kutatuliwa na vijana wao.
-Serikali iwasajili vijnana wote wataohitaji kutatua changamoto kuu chache zilizoorozeshwa
-Wananchi kupitia serikali za mitaa, wajitokeze kusikiliza na kuchagua kwa Kura changamoto ya kuanza nayo na pia kuchagua mpango bora wa mhitimu kati ya walio
-Serikali iandae taratibu na pia itoe support kupitia fungu lake la 10% kwa vijana kupitia mfumo huu
-Tunafahamu serikali haiwezi kutuajiri watu wote lakini sasa basi serikali isiwe na ugumu kwa kuweka mazingira magumu na taratibu ngumu za vijana wasio na ajira kufanikisha malengo yao, kama kufungua biashara, taasisi, na miradi kama usajili.

Hatuwezi kusubiri serikali kutusaidia kutatua kila changamoto iliyopo mtaani wakati njia rahisi za kutatua changamoto za jamii (mamilioni ya changamoto) na changamoto za serikali yenyewe (yaani ukosefu wa ajira kwa vijana wake) zipo waziwazi. VIJANA AJIRA JAMII itaisaidia serikali kutatua changamoto nyingi kirahisi kwenye jamii na pia kuwasaidia vijana wengi kupata Ajira endelevu na kuondokana na dhana ya kuisubiria serikali iwapatie Ajira ambayo ni ngumu kwa kila mhitimu kuipata. Kwahiyo vijana wenzangu tujiongeze kutafuta fursa kwa kutatua changamoto kwenye jamii zetu. Tukumbuke Mitandao mikubwa, makampuni makubwa na taasisi kubwa duniani zinazoajiri watu wengi zaidi duniani leo hii zilianza na mtu mmoja ambaye aliona ni changamoto kwa jamii aliyoanza nayo. Serikali haiwezi kutuajiri sisi wote ni kama asilimia 5% ya wahitumu wote wanaweza kubahatika kupata ajira, wengi tutasubiri mpaka uzee na bado hatutapata Ajira. Vijana wenzangu Tuthubutu. Ajira zipo kwenye Jamii zetu.

AHSANTE
MHITIMU
 

Attachments

  • Vijana Ajira Village.jpg
    Vijana Ajira Village.jpg
    145 KB · Views: 12
Upvote 5
Mbaya zaidi na zaidi tunakufa na elimu zetu jamii ikiendelea kuishi na matatizo yaleyale kwa sababu ya kukosa mfumo bora na rahisi wa kutatua changamoto za jamii kupitia elimu iliyozalishwa na kupandikizwa kwa vijana wao waliowapeleka chuo
 
Wananchi watashiriki pamoja na vijana wao kuendeleza jamii zao. Kupitia mfumo huu wananchi watakuwa ndio wanaoamua ni matatizo gani ni ya kipaumbele kwao na yawe ya kwanza kutatuliwa, Matatizo ya jamii yataorodheshwa na kupigiwa kura katika mkutano wa kijiji au jamii
 
Wazo ni zuri na jema, lakini changamoto inakuja kwenye suala la support kutoka serikalini na suala la pesa mfano walimu hao wanalipwaje ili waweze kuendesha maisha yao?
 
Back
Top Bottom