Msweet
JF-Expert Member
- Mar 26, 2014
- 3,135
- 4,306
Maharusi wakiwa katika mavazi nadhifu ambayo huuzwa kwa gharama kubwa. Haya ni miongoni mwa mambo yanayoelezwa kuwa tishio kwa vijana wengine kuoa au kuolewa.Picha zote mtandao.
Vijana ambao ndiyo kundi kubwa wanakwepa kufunga ndoa kwa sababu mbalimbali Inaonyesha kuwa wanawake walioolewa au kuishi pamoja na wenzi wao walikuwa wengi zaidi na walikuwa ni asilimia 58, ikilinganishwa na wanaume waliooa au kuishi na wenzi wao ambao ni asilimia 57
Dar es Salaam. Ugumu wa maisha unaozikabili familia nyingi nchini unaelezwa kusababisha athari nyingi kwa maendeleo ya jamii.
Athari hizo zimegawanyika katika makundi mbalimbali yakitofautiana na mitazamo na hali ya maisha.
Hata hivyo baadhi ya athari hizo zinawakumba vijana ambao ndiyo kundi kubwa la Watanzania moja ikiwa kupata hofu ya kuamua kutekeleza au kuamua mambo mbalimbali ikiwamo kufunga ndoa.
Tatizo hilo ni ukweli unaowekwa hadharani na maelezo mbalimbali ikiwamo takwimu za kitaalamu za Sensa za Idadi ya Watu na Makazi iliyofanyika nchini mwaka 2012, iliyobainisha kuwa asilimia ya watu waliooa au kuolewa imepungua.
Taarifa za msingi za kidemografia, kijamii na kiuchumi ya matokeo muhimu yaliyojitokeza kwenye Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 zinaonyesha kwamba asilimia ya watu waliooa au kuolewa imepungua.
Takwimu za Sensa
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali (OCGS),Zanzibar hali hiyo inaweza kuwa imesababishwa na ugumu wa maisha na ugonjwa wa Ukimwi.
"Asilimia ya watu waliooa au kuolewa imepungua kutoka asilimia 54 mwaka 2002 hadi asilimia 51 mwaka 2012. Hii inaweza kuwa imesababishwa na ugumu wa maisha na athari za ugonjwa wa Ukimwi," imeeleza taarifa hiyo.
Inaeleza kuwa asilimia 58 ya watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi nchini wameoa au kuolewa au kuishi pamoja na wenzi wao.
Matokeo hayo muhimu yanabainisha kwamba idadi ya watu walioachana au kutengana imepungua kutoka asilimia tano mwaka 2002 mpaka asilimia nne mwaka 2012, hali ambayo ilielezwa kuwa ni ishara ya kudumu kwa ndoa kadiri miaka inavyoongezeka.
Ustawi wa Jamii
Kamishina wa Ustawi wa Jamii, Dunford Makala anakiri hali hiyo akieleza kwamba inasababishwa na mambo meng, ikiwamo ulimbukeni wa baadhi ya vijana kutaka mashindano ya sherehe za kifahari zisizo na tija tofauti na vipato au uwezo walio nao.
"Ni kweli inapozungumzwa ugumu wa maisha ni hali halisi, ambayo inawakumba vijana wengi lakini wengine wanashindwa kutimiza hatua hiyo kwa sababu ya kutaka kushindana waache historia ya sherehe zao za ndoa kwamba zilifana au walivaa mavazi ya kifahari," anasema Makala.
Anafafanua kwamba pia ni kweli ugonjwa wa Ukimwi nao umekuwa tishio kwani wengine kwa kuogopa kwenda kupima huamua kuwashawishi wasichana na kuwatia mimba ili waone matokeo yatakavyokuwa.
Makala anasema pia dini nazo zimekuwa ni kikwazo kwa vijana wengi kuungana rasmi, kwani wapo wengine ambao wamejikuta katika wakati mgumu walipokwenda kutambulisha wenzi wao watarajiwa na kujikuta wakikumbana na vitisho hasa za kutengwa na familia.
"Jingine ni kwamba vijana wengi wanaogopa majukumu hasa kulea, kwani wapo wengine ambao walichangiwa sherehe zao zikafana, lakini wamepata mtihani katika kuhudumia familia mara ndoa zinazojibu kwa watoto kuzaliwa, hao ndiyo wanakuwa mifano mibaya kwa wengine," anasema Makala.
Maneno ya viongozi wa dini
Imamu
Imamu wa Msikiti wa Mchangani Magomeni jijini Dar es Salaam, Sheikh Jaffari Fota anasema kuwa katika msikiti huo hali ni tofauti kwa sababu watu wanaojitokeza kufunga ndoa wamekuwa wengi.
Alifafanua kuwa mwaka 2012 walifungisha ndoa 120, kati ya hizo ndoa kumi zilivunjika na moja mume kufariki, mwaka 2013 walifungisha ndoa 130 ambapo kati ya hizo nane zilivunjika, ndoa mbili wanaume walikufa na ndoa moja mwanamke alikufa.
"Kwa mwaka 2014 kuanzia Januari hadi sasa tumefungisha ndoa 140, kati ya hizo ndoa kumi zina kesi, na tano wameshaachana, pia ndoa moja wote walifariki dunia."
Mchungaji
Mchungaji Eliona Kimaro wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kariakoo anasema kuwa kanisa hilo limekuwa likipokea waumini wengi kwa ajili ya kufunga ndoa.
"Hapa kwangu hali ni tofauti labda kwa sababu kanisa hili liko maeneo ya mjini, kwani nimekuwa nikipokea maombi mengi ya kufungisha ndoa hali ambayo inanilazimu nami kuwaomba wachungaji wenzangu kunisaidia," anasema Mchungaji Kimaro.
Anafafanua kuwa kusema baraka hiyo ya kufungisha ndoa kwa mwaka juzi zilifungwa 50 na kwa mwaka jana kuanzia Januari hadi Novemba wamefungisha ndoa 30 na wanatarajia idadi hiyo itaongozeka kwa sababu mwaka ulikuwa hujaisha.
Msaidizi wa Imamu Aboubakar Hussen wa Msikiti wa Manyema Kariakoo anataja idadi ya ndoa zilizofungwa mwaka juzi kuwa ni 34, kwa mwaka jana kuanzia Januari hadi Novemba wamefungisha ndoa 47.
Mwangalizi wa Kanisa la Kipentekoste, mchungaji William Mwanalanga anasema kumbukumbu alizonazo kwa ndoa zilizofungwa katika kanisa hilo kwa mikoa mitatu ambayo ni Mbeya, Dar es Salam na Iringa ni 18.
" Ni kweli kumekuwa na hofu kwa vijana ambayo inasababishwa na mambo mengi ikiwamo gharama kubwa za kufanikisha sherehe za ndoa, pia zilizotangulia nyingi zimejaa migogoro mingine ni mikubwa kiasi cha kuwa tishio kwa wengine," anasema Mchungaji Mwamalanga.
Anasisitiza kuwa uaminifu kwenye ndoa unazidi kutoweka hasa wanaume wengi hawataki kuambatana na wake zao, wengi wanarudi usiku wa manane nyumbani kwao wakitoka kwenye anasa hasa wakazi wa jiji la Dar es Salaam.
Makapera wanasemaje?
Mwenyekiti wa kikundi cha Makatambuga, eneo la Tabata Relini, Suke Suke anasema wanatamani kuwa na familia yaani kuwa na wenzi wao, lakini inawawia vingumu kwa kuwa hawana uhakika wa kipato. hivyo wametawaliwa na hofu ya kushindwa kuwatunza.
"Tumetawaliwa na hofu ya kushindwa kutunza wanawake. Binafsi niliwahi kutafuta msichana, nikaishi naye bila kufunga ndoa kwa miezi minne, baada ya hapo alinibadilikia akaanza kulalamika kwamba anahitaji nimwachie Sh10,000 badala ya Sh 5,000 kwa matumizi ya siku, eti kwa kuwa mke wa jirani yetu ndivyo anavyopewa. Nilichukia nikaona niachane naye," anasema.
Anabainisha kuwa hali hiyo ni changamoto kubwa na inayohatarisha maisha yao kwa namna nyingine, kwa kuwa baadhi yao hulazimika kwenda kusaka wanawake wanaojiuza katika maeneo mbalimbali, ili kujistarehesha hasa wanapopata fedha ambazo wao huona zinawatosha.
"Baadhi yetu tunakwenda kusaka makahaba huko Buguruni Kimboka, wakati mwingine Uwanja wa Fisi, Manzese. Maeneo hayo niliyokutajia wanawake tunaowapata wana ustaarabu kiasi, lakini kwenye madanguro ya Kinondoni ni vibaka," anasema.
Naomi Gabriel anasema hatamani kuolewa kwa sasa, ingawa anapenda kuitwa mama, akidai kuwa hali hiyo imemkuta baada ya kushuhudia wanaume wengi waliooa wasivyo waaminifu huku wakiishia kuwanung'unikia wake zao.
"Yaani wengi wamejaa tamaa ya ngono na ni wababe, mimi nimewashuhudia baadhi ya rafiki zangu wakiwa hawana amani na ndoa zao, nami kuna kijana ananipenda na anajaribu kunishawishi lakini nina hofu kama atabadilika baadaye na kuwa kama wenzake," anasema.
Kijana Brown Meshack (35), mkazi wa Sinza anasema kuna malengo aliyojiwekea ikiwamo kusoma kwa kuwa na kiwango cha shahada, na tayari amefanikiwa, lakini bado anataka kuhakikisha anajimudu vyema kimapato ndipo aoe.
"Pamoja na hayo kuna jambo linanichanganya bado sijui kama nitapata msichana mwaminifu, nitakubalika na familia yake kwani nina ushahidi kabisa baadhi ya ndoa hazipo kwa sababu ya ndugu, hasa wazazi kuingilia wakitaka kuwapangia mfumo wa maisha hasa ya kifahari," anasema.
Anasema kwamba kwa upande wake hapendi sherehe ya kifahari za kujionyesha kwa watu, bali anapenda kufunga ndoa na msichana watakayeelewana kwa kila hali, akiamini kwamba itawasaidia kuishi kwa amani na siyo mashindano.
Kwa upande wake Juma Hassan anasema amechelewa kuoa kwa sababu msichana aliyempenda alikuwa dini tofauti na yeye na hata walipojaribu kwenda kujitambulisha kwa wazazi walikutana na vikwazo pande zote, hivyo akaachana naye na tangu hapo hajajisikia kupenda mwingine.
"Nilimpenda kwa kweli yule msichana alikuwa ananielewa vyema yaani kwa kifupi yeye ndiye niliyempokea kwenye moyo wangu ili awe wa maisha yangu daima, nikiamini atanielewa na kunivumilia hata nikikosa cha kumpelekea," anasema Hassan.
Anasema kwamba wasichana wengi wa sasa hawana upendo wa dhati bali wanapenda vitu, wanatamani kuwa na mwanaume anayemiliki gari na nyumba siyo kwamba waanze wote maisha.
"Wengi wanatamani kufunga ndoa za kifahari tu, lakini siyo kuwa na mbinu za kuishi kwa mafanikio, wao wanapenda kuvaa mavazi ya gharama na kuwatishia wenzao, mwishowe wanakuwa siyo waaminifu," anasema.
Chanzo:Mwananchi