Kumekuwepo na kipande cha
video kilichochapishwa ukurasa wa Facebook wa Nalinga Media, kikiwa na nukuu kuwa mapigano makali yameripotiwa kuzuka kati ya vikosi vya Marekani na vikosi vya ardhini vya Iran (IRGC). Inadaiwa kuwa mapigano hayo yalitokea wakati wa operesheni ya kutua kwa njia ya anga iliyolenga kuwatafuta marubani waliopotea katika eneo husika.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, operesheni hiyo iligeuka kuwa mapambano ya moja kwa moja baada ya vikosi hivyo kukutana uso kwa uso, hali iliyodaiwa kuongeza mvutano wa kijeshi katika eneo hilo.
Video hiyo imeenea kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii, mara baada ya vyombo mbalimbali vya habari duniani kuripoti kuwa Iran imetangaza zawadi ya Tomans bilioni 10 kwa yeyote atakayefanikiwa kuwakamata marubani wa Marekani, wanaodaiwa kuwa bado wapo katika milima ya nchi hiyo baada ya helikopta ya kijeshi waliyokuwa wakitumia kudunguliwa.
Ni upi uhalisia wa video hiyo?
Ufuatiliaji wa kidijitali umebaini ripoti ya video hiyo inapotosha uhalisia wa kile ambacho kinaendelea. Video hiyo iliwaahi
kuchapishwa mtandaoni mwaka 2018, ikirejelea tukio la
shambulizi lililotokea katika gwaride la kijeshi mjini Ahvaz, kusini-magharibi mwa Iran, ambapo wanajeshi kadhaa wa kikosi cha mapinduzi waliuawa na wengine saba kujeruhiwa.
Mnamo tarehe 22 Septemba 2018, watu wenye silaha waliovalia sare za kijeshi walifyatua risasi katika gwaride la kijeshi lililokuwa linaadhimisha Vita vya Iran na Iraq.
Shambulio hilo lilisababisha
vifo vya watu 25, wakiwemo wanajeshi kutoka Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) pamoja na raia waliokuwa wakitazama.
Kundi la Islamic State (ISIS) pamoja na kundi la Arab Struggle Movement for the Liberation of Ahvaz yalidaiwa kuhusika na shambulio hilo.
Aidha, pamoja na mvutano unaoendelea Mashariki ya Kati, hadi sasa hakuna uthibitisho kuwa jeshi la Marekani limepeleka wanajeshi wake nchini Iran kuanzisha mapigano ya moja kwa moja. Ingawa kuna taarifa za kuwepo kwa wanajeshi wa Marekani katika kambi za kijeshi kwa ajili ya maandalizi, bado hakuna operesheni rasmi ya mapigano iliyoripotiwa kuanza.