Mphamvu
JF-Expert Member
- Jan 28, 2011
- 10,702
- 3,319
Makala hii ilichapishwa katika Mwananchi la 19 Mei 2014
Na Mphamvu Daniel
Katibu mkuu wa Fifa, bwana Jerome Valcke alifanya ziara hapa nchini wiki kadhaa zilizopita. Pamojana kufungua semina ya viongozi wa soka wa Ukanda huu (CECAFA), kulikuwa na masuala kuhusu marekebisho ya viwanja kadhaa hapa nchini ukiwemo uwanja wa Kaitaba mjini Kagera na Nyamagana jijini Mwanza. Marekebisho hayo ni pamoja na kuwekwa nyasi bandia katika eneo la kuchezea la viwanja husika.
Mradi wa FIFA wa Goal ndio unaoratibu na kufadhili mchakato wa uwekaji nyasi katika viwanja hivyo. Miradi mingine kama hiyo ilishafanyika hapa nchini katika viwanja vya Karume na Uhuru jijjini Dar na uwanja wa Gombani huko Pemba.
Siku chache baada ya ya ujio wa Valcke, mtaalamu wa nyasi kutoka FIFA akaja nchini na kufanya ziara ya ukaguzi katika viwanja hivyo viwili kujionea hali halisi, pengine na kufanya upembuzi wa kazi anayokuja kuifanya karibuni.
Bila shaka baada ya kuwekwa nyasi bandia, viwanja hivyo vitaachwa chini ya uangalizi wa TFF ambao ndio wasimamizi wakuu wa Soka hapa nchini.
Ubovu na uhaba wa viwanja bora vya kuchezea hapa nchini ni tatizo kubwa na la muda mrefu hapa na wadau wamekuwa wakipigia kelele. Wengi huelekeza lawama kwa TFF na wamiliki wa viwanja kwa kushindwa kujenga au kukarabati viwanja vilivyopo.
Wadau hawa wanasahau ukweli kuwa mhitaji mkubwa wa hivyo viwanja, na watakaofaidika navyo baada ya marekebisho ni vilabu vinavyoshiriki ligi mbalimbali nchini. Uwanja mkuu wa Taifa mathalani, haiingii akilini ya kuwa TFF imefaidika navyo kuliko vilabu vya Simba na Yanga ambavyo hutumia kama uwanja wao wa nyumbani.
Uwanja pekee ambao unaweza kusema kuwa TFF wanafaidika nao sana ni uwanja wa Karume, ambapo zaidi ya kufanyia hapo mashindano yake ya vijana lakini pia kituo cha Soka la watoto cha TFF hufanyia shughuli zake za kiufundi hapo.
Zaidi ya kufaidika kwa kuwa na uwanja wa nyumbani wa kuchezea mechi, timu hizi pia hupata mgao wa mapato ya mlangoni yanayotokana na mechi husika. Katika mapato haya TFF na Kamati ya Ligi huchukua kiasi kisichozidi asilimia tano lakini mgao mkubwa huenda kwa vilabu.
Hapa ndipo panapochekesha, kama mapato ni faida na ili upate faida unahitaji kuwekeza, kwanini wewe unayefaidika usifanye huo uwekezaji?
Kwa muda mrefu sasa vilabu vinavyomilikiwa na wanachama vimepuuza suala la uwanja, na hata vilabu vya zamani ambavyo vilimilikiwa na mashirika ya Umma navyo vilianguka katika mkumbo huu wa kupuuzia umiliki wa viwanja. Timu ya Ushirika ya Moshi ni kati ya timu chache za mashirika ambazo zilimiliki uwanja wake wa kuchezea.
Tukirejea katika timu za wananchi, sio simba, Yanga, Ashanti, Kariakoo, Coastal Union au yoyote nyingine ambayo imethubutu kuwa na uwanja, walau wa kuingiza washabiki 5000. Sarakasi za uwanja wa Bunju na Jangwani Stadium ambazo Simba na Yanga wamekuwa wakizipiga kwa miaka kadhaa sasa zimetuchosha.
Kuwa na uhakika wa mahali pa kuchezea au kufanyia mazoezi, wakati mwingine kunashawishi hata kuwa na timu za vijana, kwani wasiwasi wa sehemu ya kujifunzia haupo tena. Azam FC wameweza kufanya uwekezaji wa timu za watoto na vijana si tu kwa kuwa wana hosteli, lakini pia vipo viwanja vya kufanya mazoeza na kujifunza.
Vilevile uwanja ni kitega uchumi kwani huweza kukodishwa kwa wanachi na mashirika kwa ajili ya matamasha, mabonanza na shuguli nyingine mbalimbali.
Timu zetu za wananchi zimeendelea kuwa wategemezi wa viwanja vibovu vinavyomilikiwa aidha na manispaa, Serikali au Chama cha Mapinduzi huku malalmiko ya mashabiki wao yakiwa lukuki kuhusu ubovu wa viwanja husika.
Zipo timu kama Mtibwa na Azam ambazo zimethubutu kuwa na viwanja vyake vya mechi na mazoezi. Kitendo cha kuwa na timu ambazo zina viwanja hapa hapa ambako wengine wanalilia 'kubebwa' kutoka TFF kunaonesha kuwa inawezekana kwa timu kuwa na viwanja vyake. Katika kundi hili hatuwezi kuweka viwanja kama Mabatini wa JKT Ruvu Shooting kwa kuwa hizo timu zilikuta tayari uwanja upo, ambao hata hivyo ni mali ya Jeshi.
Klabu ya Mbeya City iliweza pia kwa kushirikiana na wamiliki wa Uwanja wa Sokoine, kufanya marekebisho makubwa katika eneo la kuchezea la Uwanja huo wakati wa mapumziko madogo ya Ligi na faida ya juhudi zao ni pamoja na mechi ya Timu ya Taifa kuchezwa hapo kwa mara ya kwanza katika historia.
Serikali yetu nayo kwa kushirikiana na Serikali ya Watu wa China wameweza kujenga Uwanja Mkuu wa Taifa, ambao ni moja kati ya viwanja vua kisasa barani Afrika, kwa hiyo sina shaka na Uwezo wa taasisi na watu wetu katika kujifanyia mabo yao wenyewe. Sasa kuna haja gani ya kuendelea kudeka na kujitia umasikini?
Uwanja ni jengo kama yalivyo majengo mengine na mchakato wa kuujenga ni mchakato wa kihandisi. Mashirika binafsi yamejenga majengo makubwa makubwa, vyama vya ushirika navyo viweza kujenga majengo makubwa, kwanini tushindwe viwanja?
Suala la mwisho ambalo linaniacha na taharuki ni usimamizi wa viwanja hivi vya msaada kutoka Fifa. TFF kwa sasa wanausimamia uwanja wao mmoja wa Karume, waliorekebishiwa miaka kadhaa nyuma na mradi huu wa Fifa ambao utafadhili uwekaji nyasi katika viwanja vya Kaitaba, Nyamagana na Gombani.
Usimamizi wa uwanja huu si wa kuridhisha, mwaka huu wakati wa mashindano ya Uhai, niliona kwa macho yangu nyavu za kwenye magoli ambazo zilikuwa zimenyofoka kwa chini zikiwa zimeshikiliwa na matofali.
Wakati wa mazoezi ya Timu ya Taifa mwezi jana, nilitembelea hapo uwanjani, nyazi hazikuwa katika muonekano mzuri na maji yalionekana kutuama uwanjani.
TFF wameshindwa kuusimamia ipasavyo uwanja huu wao ambao upo makao makuu yao, wataweza kweli kusimamia viwanja vilivyopo mamia ya kilomita kutoka walipo?
Ni wakati wa vilabu ambao ni wadau wakubwa wa viwanja kuchukua hatua zinazofaa ili kuhakiksha walau wanakuwa na kiwanja cha mechi kabla ya mambo mengine.
Simu :+255 713 049 852
Barua pepe: mphamvudaniel@gmail.com