SoC03 Viongozi wasiotimiza wajibu wawajibishwe ili kuwepo na utawala bora

SoC03 Viongozi wasiotimiza wajibu wawajibishwe ili kuwepo na utawala bora

Stories of Change - 2023 Competition

Chu joe

Member
Joined
Jul 15, 2021
Posts
7
Reaction score
3
Kiongozi ni mtu yeyote anayechaguliwa au kuteuliwa na mtu au watu kwaajili ya kuwaongoza wengine katika misingi ya utawala bora na kuwasimamia wengine katika njia sahihi yenye kuleta mabadiliko chanya na maendeleo kwa jamii husika.

Katika dunia yetu viongozi wapo wa aina tofauti, wapo wale wa kuchaguliwa, kuteuliwa, na wanaoingia madarakani kwa njia ya mapinduzi ya kijeshi, lakini pamoja na aina hizo dhima kuu ya uongozi huwa ni kuilinda, kuitetea na kuiletea maendeleo jamii anayoiongoza.

Leo kwenye makala hii nataka kuzungumzia kuhusu viongozi wanaoshindwa kutimiza wajibu na hawachukuliwi hatua za kisheria wakati ni wazi wameshindwa kufanya kile ambacho walikiahidi wanapoingia kwenye uongozi na jamii ilitegemea kukipata kutoka kwao.

Zipo sababu zinazochangia viongozi kutotimiza wajibu wao na kupelekea kuwepo kwa utawala usio bora, hivyo basi hapa nitaziweka Sababu hizo na kutoa maoni yangu ni kipi kifanyike ili kuondokana na viongozi wasiotii sheria za nchi wala maadili ya utawala bora.

Kutokuwa na elimu ya uongozi, nchini kwetu Tanzania hakuna somo rasmi linalofundishwa kuhusu uongozi katika shule za msingi na sekondari, na sheria inasema Ili mtu agombee ubunge anapaswa kujua kusoma na kuandika tu, ukichunguza kwa umakini utagundua sheria hii Ina mapungufu, kwahiyo ili kupata viongozi bora watakaozingatia utawala bora tunapaswa kuwa na somo rasmi katika shule zetu pia kubadili sheria hii inayompa mtu yeyote anayejua kusoma na kuandika uhuru wa kugombea.

Kutozingatia sheria za utawala bora, viongozi wengi wa Afrika mfano hapa kwetu Tanzania wanatawala bila kuzingatia kanuni za uongozi bora, hali inayopelekea kutotimiza wajibu wao kama viongozi na kushindwa kuwawakilisha vyema wananchi wao katika muhimili wa bunge, kwahiyo ili kuondokana na viongozi wa aina hiyo inapaswa itungwe sheria itayowabana wanaoshindwa kutimiza wajibu wao kutoendelea na uongozi na kukosa sifa ya kugombea tena.

Kuongoza kwa mazoea, baadhi ya viongozi wa serikali wamekuwa wakishindwa kutimiza wajibu wao kwasababu wanaongoza Kwa mazoea, na hiyo inatokana na viongozi hao kujua wazi katika maeneo waliyopo ni lazima chama wanachokisimamia kitashinda, mfano katika jimbo la Morogoro mjini chama cha mapinduzi kimekuwa kikiibuka na ushindi mara nyingi kwa miaka ya karibuni, hivyo ni rahisi kwa kiongozi kutoka jimbo hilo kuongoza kwa mazoea kwasababu hana hofu ya kupoteza wadhifa wake.

Viongozi kutowajibishwa wanapokutwa na kashfa za ubadhilifu wa mali za umma, katika nchi zilizoendelea mfano China kiongozi akibainika amefanya ufisadi basi ni lazima hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yake ikiwemo kufungwa ili kutimiza dhana ya utawala bora, lakini hapa nchini tumeshuhudia viongozi tofauti wakikiri hadharani kuhusika katika wizi wa mali za serikali mfano pesa za Escrow na wakaachwa huru bila kuenguliwa katika nafasi zao wala kushitakiwa mahakamani, kwahiyo ili kuwepo na utawala bora viongozi kama hao wanapaswa kuwajibishwa kisheria.

Kurithishana uongozi, Sababu nyingine inayochongia kutokuwepo na utawala bora ni tabia ya kurithishana uongozi, nchini Tanzania viongozi wamekuwa na tabia ya kuwarishisha uongozi watoto wao ili waendelee kuongoza katika maeneo yao, mfano Mzee Ally Hassan Mwinyi amemrithisha mtoto wake Hussein Ally Mwinyi uongozi japo sio moja kwa moja lakini inawezekana kwa kiasi kikubwa amemshawishi ili afuate nyayo zake kuwa mwanasiasa kwahiyo ili kupata viongozi bora watakaozingatia utawala bora hatupaswi kurithishana uongozi.

Kutokuwa na uchaguzi huru na wa haki, katika jamii yetu ya kitanzania tumekuwa tukishuhudia viongozi au wagombea wa vyama vya upinzani wakilalamika kuwa vipindi vyote uchaguzi huwa sio huru na wa haki, vile vile jumuiya za kimataifa zimekuwa zikizungumza kuhusu hilo mfano uchaguzi mkuu wa Zanzibar mwaka 2015 haukuwa huru na wa haki na hilo lilithibitika wazi baada ya mwenyekiti wa tume ya uchaguzi wa kipindi Hicho Jecha Salim Jecha, kufuta uchaguzi kwasababu kiongozi waliyemtaka hakuweza kuibuka mshindi, kwahiyo ili kupata viongozi bora watakaoleta maendeleo kwa jamii ni lazima kuwe na tume huru ya uchaguzi.

Yote kwa yote uongozi ni wito na ni mzigo mzito unaopaswa kubebwa na mtu mwenye maono na aliyetayari kuipeleka jamii yake katika nchi ya ahadi, kwahiyo viongozi wote wanapaswa kutii sheria za nchi na miongozo ya utawala bora Ili waweze kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
 
Upvote 0
Back
Top Bottom