MAKA Jr
JF-Expert Member
- Nov 17, 2016
- 267
- 209
UTANGULIZI
Watanzania tunasifika kwa upole na ukarimu. Hizi sifa na nyinginezo hazikuja bure. Waasisi wa Taifa hili walitumia mbinu nyingi kutujengea sifa hizi za kiungwana. Moja ya mbinu hizo ni kuhimiza matumizi ya lugha ya Kiswahili ambayo imetujengea utamaduni huo hadi leo.
Hata hivyo, pamoja na sifa hizi nzuri, utamaduni wetu umetujengea sifa nyingine. Sifa hiyo ni visingizio. Tabia hii ya kuwa watu wa visingizio imeota mizizi miongoni mwetu na inaleta athari katika maendeleo katika nyanja mbalimbali za maisha yetu.
Visingizio hivi sio vidogo. Kama hata kisingizio kimoja kinakuhusu, jiulize Watanzania 10, 20, 50, 100 au zaidi wakifanya kama wewe ni kwa kiasi gani tutakuwa tumerudi nyuma kimaendeleo.
Katika Sehemu hii ya Kwanza visingizio hivi vimepewa namba 1 hadi 10, lakini sio lazima usome kuanzia 1 hadi 10 kwa mtiririko. Unaweza kusoma kwa kuchanganya. Unaweza kuanzia katikati au hata mwisho kurudi nyuma.
Makala hii imetaja na kuelezea kwa kina kila kisingizio.
Vifuatavyo ni visingizio 20 vinavyorudisha nyuma maendeleo ya Watanzania - Sehemu ya Kwanza:
Kizingizio namba 01: Kiingereza kilikuja na ndege/meli.
Hiki ni kizingizio kwa mtu yeyote ambaye Kiingereza kimemshinda au hapendi kujifunza Kiingereza. Lugha ya Kiingereza ni 'Kiswahili' cha Dunia. Hata akikikwepa leo, atakutana nacho mahala pengine.
Kujifunza Kiingereza ni muhimu. Kama unaweza, jifunze Kiingereza au lugha nyingine zaidi ya lugha unazozijua. Hata mtalii kutoka Urusi akija Tanzania lazima ajue Kiingereza kwa sababu Tanzania hakuna lugha ya Kirusi, bali kuna Kiingereza.
Kizingizio namba 02. Kiswahili kinanitosha.
Ni kujidanganya kusema kuwa Kiswahili kinatosha. Unataka kusema kuwa Kinyamwezi kingekutosha hadi leo? Sio kweli. Ndio maana ulihitaji Kiswahili ili kujitosheleza zaidi.
Kama ambavyo ulikuwa na lugha yako ya Kinyamwezi na ukaamua kujifunza Kiswahili, vivyo hivyo ni uamuzi wa busara kujifunza lugha nyingine. Kujifunza lugha nyingine ni zaidi ya kujua maneno. Ni kujifunza utamaduni na ujuzi wa jamii husika.
Kisingizio namba 03. Kuongea Kiswahili nyumbani kwenu ni dharau.
Sio dharau kutumia Kiswahili nyumbani. Wakubwa na wasiojua Kiswahili ndio wanaona kutokujua kwao Kiswahili kunawaletea shida au wanaona wivu na ndiyo maana wakasema ni dharau. Hakuna dharau yoyote. Kwani unatukana?
Bado kila mtu ana muda wa kujifunza Kiswahili na yatupasa kuwaheshimu wanaojifunza kutumia Kiswahili kwa sababu ni faida kwao hata kwa wanaopinga pia.
Kisingizio namba 04. Kuongea Kiingereza ni kujidai.
Wengi wanaosema kuongea Kiingereza ni kujidai ni wale ambao hawajui Kiingereza na wanataka kujificha nyuma ya kimvuli cha kusema kuwa wanaoongea Kiingereza wanajidai. Kwa nini wanaoongea Kifaransa hatusemi wanajidai? Hiki ni kisingizio tu.
Ufumbuzi pekee ni kujifunza Kiingereza au lugha nyingine na kuwaheshimu wanaojifunza.
Kisingizio namba 05. Nisome vitabu ili nigundue nini?
Kwenye vitabu kuna ujuzi mwingi sana. Vitabu vimebeba kila aina ya ujuzi unaohitajika katika maisha yetu.
Kusoma vitabu ni moja kati ya njia muhimu za kupata ujuzi. Anayebeza usomaji wa vitabu ni sawa na anayemtukana mamba kabla hajavuka mto. Japo kutegemeana kupo, lakini ukweli ni kwamba asiyesoma anamtegemea sana aliyesoma. Kwa mfano usiposoma kitabu kuhusu ufugaji wa kuku, kuku wako wakipata shida, utamuuliza rafiki yako aliyesoma kitabu cha ufugaji wa kuku! Kwa hiyo, watu wasome, wasisingizie, na wawaheshimu wale wanaosoma.
Kisingizio namba 06. Unasoma sana. Umetumwa na Kijiji?
Kauli hii ni kisingizio kwa baadhi ya wanafunzi wa ngazi zote; shule ya Msingi hadi Vyuo Vikuu. Kauli hii ni kisingizio cha mvivu wa kusoma na anayemvunja moyo mwenzake anayesoma.
Ukikutana na kauli hii usikubali ikuvunje moyo. Endelea kusoma kwa mujibu wa ratiba yako. Watu wenye kauli hizi ndio ambao baadae hupata msaada kutoka kwa hawa hawa wanaowakejeli na kuwavunja moyo.
Kisingizio namba 07. Unanipa nisome kwani mimi mwanafunzi?
Uvivu wa kusoma na kuandika ni mkubwa kwa baadhi yetu kiasi kwamba ukimwambia mtu asome ni kama umeanzisha ugomvi wa ngumi. Kutokana na uvivu wetu wa kusoma, tumeamua kutoa visingizio kuwa wanaosoma ni wanafunzi tu au wale walioko shule. Huu sio ukweli.
Kusoma kuna faida nyingi. Unaposoma haupungukiwi chochote na badala yake unaongeza ujuzi kwa faida yako na Taifa kwa ujumla.
Kisingizio namba 08. Nitembee na kalamu kwani nimekuwa Mwalimu?
Kisingizio hiki kitakuponza mara utakapokutwa na jambo linalohitaji matumizi ya kalamu. Ukweli ni kwamba kalamu ni muhimu na hakuna ubaya wowote kutembea na kalamu. Watanzania tumeona ni kama kalamu anapaswa kutembea nayo Mwalimu tu. Lakini hawa hawa watu wenye kisingizio hiki ndio wanaongoza kuazima kalamu kutoka kwa wale wanaotembea nazo.
Japo inategemea na kazi unayofanya, lakini kutembea na kalamu ni jambo jema na lenye busara. Jambo unalofanya ni kwa manufaa yako na ya hao hao ambao wanebeza kutembea na kalamu.
Kisingizio namba 09. Nitembee na 'Notebook' kwani nimekuwa mwandishi wa Habari?
Shajara (notebook) ni kifaa muhimu sana. Unaweza kutumia Shajara kuweka taarifa zako binafsi, taarifa za ofisi, taarifa za mafunzo au semina, au dondoo za ujuzi fulani uliojifunza. Kisingizio hiki hakina uungwana na weledi katika Ulimwengu wa sasa. Wanaokataa kubeba na kutumia shajara kama kazi zao zinahitaji kuandika mara kadhaa wanakutana na mambo mengi yanayohitaji kuandikwa. Na kwa namna moja au nyingine, wanahangaika, na kusaidiwa na wale wenye shajara.
Kwa mfano, hata kondakta wa basi, anahitaji shajara kwa ajili ya kuweka taarifa mbalimbali za abiria wake.
Kisingizio namba 10. Niandike nywila (password) ya nini? Nitaiweka tu kichwani. Nitaikumbuka.
Ni rahisi kutengeneza 'nywila' (password), lakini ni vigumu kuitunza na kuikumbuka vizuri. Watu wengi tunapenda kusingizia kuwa tutakumbuka nywila zetu, lakini kila mara hatufanikiwi. Tumekuwa tukipata hasara na kupoteza vitu vingi sana kwa uzembe wa kupoteza au kutokumbuka nywila zetu kwenye vifaa mbalimbali tunavyotumia.
Tujenge desturi ya kutunza nywila kisasa. Njia pekee ya kutunza na kuikumbuka nywila ni kuiandika sehemu hasa kwenye shajara (notebook) au mahala pengine ambapo ni salama na rahisi kuzipata.
Tuache visingizio. Tutunge nywila madhubuti na tuzitunze mahala salama. Ulimwengu wa leo umetawaliwa na mambo haya. Tuyape umuhimu mkubwa.
HITIMISHO
Ili tujipatie maendeleo yetu binafsi na Taifa letu kwa ujumla yatupasa tuache visingizio hivi na tuchape kazi. Na kama kuna baadhi ya visingizio hapo juu vinakuhusu, fanya mabadiliko kimya kimya. Sio lazima uwatangazie watu. Watu wengi waliofanikiwa hawakuruhusu visingizio kama hivi kwenye maisha yao.
Upvote
1