SoC02 Visingizio 20 vinavyorudisha nyuma maendeleo ya Watanzania - Sehemu ya Pili

Stories of Change - 2022 Competition

MAKA Jr

JF-Expert Member
Joined
Nov 17, 2016
Posts
267
Reaction score
209

UTANGULIZI
Hali ya kuwa watu wa visingizio siyo ya kubeza. Ina athari na inarudisha maendeleo yetu nyuma. Visingizio hivi sio mtindo bora wa maisha. Ni mtindo wa kurudi nyuma.

Katika Sehemu hii ya Pili, visingizio hivi vimepewa namba 11 hadi 20, lakini sio lazima usome kuanzia 11 hadi 20 kwa mtiririko. Unaweza kusoma kwa kuchanganya. Unaweza kuanzia katikati au hata mwisho kurudi nyuma.

Vifuatavyo ni visingizio 20 vinavyorudisha nyuma maendeleo ya Watanzania - Sehemu ya Pili:

Kisingizio namba 11. 'Email' mimi sijui kuitumia. Nitumie barua kwenye 'WhatsApp.'


'Email' au barua pepe ndio kitovu cha mawasiliano mengi siku hizi. Mfano, huwezi kuwa na simu janja bila barua pepe. Wala huwezi kuomba ajira bila barua pepe. Watu wote wanaosingizia kuwa barua pepe sio muhimu, hupata tabu kila mara wanapotakiwa kuwa nazo.

Barua pepe ('Email') ni muhimu sana kwenye Ulimwengu wa sasa. Tengeneza barua pepe, itunze na ukumbuke 'password'. Epuka usumbufu na kuwa mtu wa kisasa kwa kuwa na barua pepe wakati wote katika maisha yako.

Kisingizio namba 12. Kila mara kutunza vitu kwenye 'Google Drive' naona ni kama usumbufu tu.

'Google Drive', 'MEGA', 'One Drive' na programu nyingine kama hizi ni muhimu sana katika kutunza taarifa binafsi na za kiofisi. Hizi programu ni za bure kabisa na hutumika kama 'stoo' ya kutunzia nyaraka. Sio usumbufu kutumia hizi programu. Ukiwa na shida, kwa mfano, ukipoteza vyeti, ndipo utakumbuka kuwa hizi programu ni muhimu.

Ni busara kuachana na visingizio kama hivi. Hizi programu zinasaidia sana hasa kutokana na kwamba kuna kupoteza vitu, kupata ajali ya moto au maji, na pia kuna kuibiwa.

Kisingizio namba 13. Wa kusoma utakuwa wewe?

Mtu anayesema haya anambeza mwenzake anayesoma au anatoa kisingizio baada ya kushindwa kusoma.

Anayesoma anatafuta ujuzi kwa faida yake na wengine. Jambo la msingi ni kumheshimu anayetenga muda wake wa kusoma.

Kisingizio namba 14. Unasoma 'dictionary'?

Tunapenda kumbeza mtu anayesoma 'dictionary' (kamusi). Hakuna ubaya wowote kusoma kamusi ya lugha yoyote ile iwe Kiswahili, Kiingereza au lugha nyingine.

Unaweza kusoma kamusi kuanzia neno la kwanza hadi la mwisho, na hakuna ubaya wowote. Malcom X, Mpigania Haki za Watu weusi nchini Marekani alikuwa ni mtu wa mtaani na alikuwa na Kiingereza kibovu sana. Alipogundua anahitaji kujua lugha ili aeleze vizuri mipango yake, alianza kusoma kamusi ya Kiingereza kuanzia neno la kwanza hadi la mwisho.

Kisingizio namba 15. 'Una-chat' na simu kila wakati?

Kisingizio hiki hutoka kwa mtu ambaye wala haoni simu ya mtumiaji kama inatumika kwa kazi gani. Huyu mtu anakuwa mbali, lakini bado anasema kitu asichokiona. Yeye anaamini kuwa kila aliyeshika simu 'ana-chat', akimaanisha kuwa anatumia simu kwa mambo yasiyo ya msingi.

Simu ina matumizi mengi zaidi ya 'ku-chat'. Kuna mtu anatumia simu kufanya biashara zake, kufanya mawasiliano, kuandika barua, kusoma, kujifunza, na kuandaa vitu mbalimbali.

Kisingizio namba 16. Huyu jamaa anashinda ndani kila wakati.

Hizi ni lawama kwa wasioelewa. Dunia imebadilika sana. Siku hizi kazi nyingine huwezi kuzifanya nje. Mtu anaweza kujifungia ndani ili afanye kazi au biashara kwa utulivu. Na wengine siku hizi wanasoma kozi mbalimbali mtandaoni. Kuna kozi nyingine inakuhitaji uisome kwa masaa sita mfululizo.

Wale wanaolaumiwa kuwa wanashinda ndani huku wanafanya kazi muhimu wanapaswa waendelee kufanya hivyo bila kuangalia kelele au visingizio kutoka kwa watu wasioelewa.

Kisingizio namba 17. Huyu huwa anashinda siku nzima anachezea kompyuta.

Ni nani aliyeturoga sisi Watanzania kuona kwamba kila anayetumia kompyuta na simu janja anacheza? Hiki nacho ni kisingizio kingine.

Japo sio kweli kwamba kila anayetumia kompyuta anaitumia kwa usahihi, lakini sio sahihi kubeza anachofanya mtu. Kompyuta ina kazi nyingi. Kompyuta ni daftari, ni ofisi, ni njia ya mawasiliano, na kadhalika. Kwa hiyo, sio sawa kuwa kila wakati mtu anachezea kompyuta.

Kama unafanya kazi yako muhimu iwe kwenye kompyuta au kwenye simu janja, endelea nayo na usithubutu kusikiliza visingizio vya watu wala kauli zao za kubeza au kuvunja moyo.

Kisingizio namba 18. Kila muda anavaa 'headphone'. Anasikiliza mziki tu. Ndio kazi yake.

Tufike mahala tuongeze uelewa wa vitu ili tupunguze visingizio na kauli zisizo na maana ili tupige hatua za maendeleo. Tuelewe kuwa anayevaa 'headphones' anafanya kati ya hivi vitu vifuatavyo, na sio kusikiliza mziki tu:
  • Kusikiliza mziki.
  • Kusikiliza taarifa ya habari au kipindi cha redio.
  • Kusikiliza hotuba.
  • Kusikiliza maelekezo.
  • Kusikiliza kitabu cha sauti.
  • Hasikilizi kitu. Amevaa ili kuepuka usumbufu kutoka kwa watu ili ajikite kwenye shughuli anazofanya.

Hakika, hata katika hili, endelea kufanya unachofanya ili uendelee kujiletea maendeleo na maendeleo ya Taifa kwa ujumla. Usiruhusu visingizio na kauli za kubeza zikurudishe nyuma.

Kisingizio namba 19. Wengi walianza, lakini walishindwa. Wewe utaweza?

Hiki ni kisingizio chenye lengo la kuacha kuendelea na kazi anayofanya mtu au kumvunja moyo mtu mwingine anayefanya kazi. Anayesema haya anatafuta uhalali au uthibitisho kuwa jambo fulani haliwezekani kwa sababu hata waliojaribu wameshindwa. Mtu huyu hataki watu wengine waendelee kujaribu.

Katika Dunia hii kila mtu ni wa kipekee na ana uwezo wa kipekee. Binadamu hatuna uwezo wa kufanana na pia hatuwezi kufanya kazi kwa kufanana au kwa viwango sawa. Unaweza kuishi Tanzania na ukafanya jambo ambalo hakuna aliyewahi kufanya duniani kote.

Kwa hiyo, kisingizio hiki ni batili kama vilivyo visingizio vingine.

Kisingizio hiki ni sawa na kisingizio kinachosema, "Acha wafanye hao hao."

Kisingizio namba 20: Unateseka


Baadhi ya watu wanapoona unafanya kazi fulani watasema unateseka. Hawakupongezi. Hawataki kukubali kuwa mtu lazima ateseke wakati wa kujenga msingi wa jambo analofanya au wakati wa kuwekeza.

Ukweli ni kwamba kufanya kazi sio kuteseka. Kufanya kazi sio kuteseka. Badala yake ni kuweka misingi imara. Pia kufanya kazi ni njia mojawapo ya kujifunza. Kadili unavyofanya kazi ndivyo unajifunza zaidi.

Kisingizio hiki kinafanana na kisingizio kingine kinachosema "Wanakutesa."

HITIMISHO
Hivi ni baadhi ya visingizio tu. Kama una visingizio ambavyo havijaorodheshwa hapa, viorodheshe, tujifunze pamoja. Kila mmoja akishiriki na kumshirikisha mwenzake, tunaweza kuleta fikra za mabadiliko katika jamii yetu.
Kama Watanzania tumeweza kuwa na upole na ukarimu hatuwezi pia kushindwa kuacha visingizio, na hatuwezi kubaki nyuma nyuma kama mikia.
Tuache visingizio. Wasio na visingizio hivi wanazidi kupiga hatua.
 
Upvote 4
Nimeishia no.12 na nimeielewa sana point yako kwa kuwa yame kwisha nipata matatizo kuhusu kuhifadhi nyalaka muhimu . Nitarudi baadae wacha nipige kazi kwanza.
 
Nimeishia no.12 na nimeielewa sana point yako kwa kuwa yame kwisha nipata matatizo kuhusu kuhifadhi nyalaka muhimu . Nitarudi baadae wacha nipige kazi kwanza.
Ndio. Hakika, Ulimwengu wa sasa unahitaji kuhifadhi nyaraka kidijitali maana kuna majanga ya moto, mafuriko n.k.

Karibu pia unipigie kura.
Pamoja sana πŸ™
 
Una vote yangu mkuu. Tupunguze lawama na visingizio Visio na tija
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…