Vita dhidi ya wauaji albino iwe endelevu

Vita dhidi ya wauaji albino iwe endelevu

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2009
Posts
42,872
Reaction score
34,363
Miongoni mwa taarifa zilizoripotiwa katika gazeti hili jana ni kuendelea kuwapo kwa mashambulizi ya kinyama dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).

Ilielezwa kuwa katika kipindi cha kuanzia 2006 hadi sasa, tayari kuna albino 74 wameuawa huku wengine 11 wakipata ulemavu wa viungo.

Ilielezwa kuwa wapo wengine 56 walionusurika kutoka mikononi mwa watu waliowavamia kwa nia ovu, hivyo kuwaacha baadhi yao wakiwa na athari kubwa za kisaikolojia kutokana na uwezekano wa kujirudia mara kwa mara kwa taswira ya majanga yaliyowakuta.

Uongozi wa Chama cha Albino Tanzania (TAS), ukishirikiana na Shirikisho la Vyama vya Walemavu Tanzania (Shivyawata), ulitoa tamko la kulaani vikali vitendo hivyo na kutaka jamii ichukue hatua zaidi za kuwalinda albino.

Ujumbe huo wa TAS uliotolewa juzi baada ya kufanyika kwa maandamano yaliyokuwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Amani Kimataifa ya Albino ulitaka pia kutolewe adhabu kali kwa watu wote wanaokutwa na hatia ya kuwashambulia albino.

Kwa mujibu wa uongozi wa TAS, ni kwamba licha ya jitihada za serikali za kuwa na vikosi maalum vya kudhibiti mauaji ya albino, bado vitendo hivyo vimekuwa vikiendelea kutokana na kile wanachoamini kuwa ni kuwapo kwa baadhi ya polisi wanaokwaza vita hiyo kwa kuwa vinara wa kupokea rushwa.

Na kwamba, kwa sababu hiyo, kati ya matukio zaidi ya 120 ya kesi za mauji ya albino, ni 11 ndizo zilizofikishwa mahakamani na kati ya hizo, ni chache tu ndizo zilizotolewa hukumu.

Kwa kurejea, taarifa rasmi za serikali zinasema kuwa hadi mwishoni mwa mwaka jana, watuhumiwa ambao tayari wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kutiwa hatiani kwa mauaji ya albino ni wanane.

Sisi tunaungana na walemavu wa ngozi kulaani vikali vitendo hivi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba wote walioshambuliwa na kuuawa au kujeruhiwa vibaya kiasi cha kuwa walemavu hawakuwa na kosa lolote.

Bali, ni matokeo ya kuwapo kwa vitendo vya ukatili dhidi ya Watanzania hawa wasio na hatia. Kama ambavyo tayari tumeshaandika mara nyingi, vitendo hivi vya kikatili dhidi ya albino havivumiliki kwa namna yoyote ile.

Jamii inapaswa kutambua kuwa albino wana haki ya msingi ya kuishi kama walivyo binadamu wengine. Muonekano wao wa ngozi ni matokeo ya sababu za Kibailojia na kamwe hakuna mmoja miongoni mwao aliyeomba kuwa hivyo.

Kadhalika, hatua za haraka zinapaswa pia kuchukuliwa kuhusiana na matukio ya mashambulizi dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi. Itakumbukwa kwamba tangu kuibuka kwa wimbi kubwa la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi ambayo yalitikisa nchi kati ya mwaka2007-2011, serikali ilichukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba kesi zote ambazo zilikuwa ngazi ya upelelezi zikifikishwa mahakamani, zikipangiwa majaji, zikisikilizwa kwa haraka na hukumu kutolewa.

Juhudi hizo hazikuishia hapo tu, serikali pia ilianzisha kampeni kubwa ambayo ilishirikisha viongozi wote wa serikali kuanzia ngazi ya mikoa, wilaya, kata hadi vijijini kuweka utaratibu wa kuwalinda watu wote wenye ulemavu wa ngozi.

Wakati kesi zikisikilizwa mashahidi mbalimbali walieleza jinsi wahusika wa unyama huu walivyokuwa wanaendesha ukatili huo, walishirikiana na nani na ni nini hasa yalikuwa matumizi ya viungo vya binadamu.

Baada ya kutulia kwa mauaji haya kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni, tulianza kujipa moyo kwamba jamii imebadilika na kutambua kwamba mauaji haya hayakuwa na kitu kingine chochote isipokuwa ni mwendelezo tu wa imani potofu za kishirikina; kwamba kuna utajiri unaweza kupatikana kwa kuua binadamu mwingine na kuuza viungo vyake vya mwili.

Tulijipa moyo kwamba jamii imeanza kutambua kuwa daima, hali bora kiuchumi huwa haiji kupitia nguvu za giza bali kujituma, ubunifu, kufanya kazi kwa malengo na pia kuwa na subira katika kila jambo.

Tuliamini kuwa jamii inajitambua kwamba kukumbatia vitendo hivyo hakika ni kujirejesha kwenye zama za mawe, zama za giza ambazo binadamu alikuwa amegubikwa na kuzidiwa nguvu na mazingira yake.

Kwa bahati mbaya, ndani ya jamii bado kuna watu wamekataa kuelimika. Wamegoma kutambua utajiri kamwe hauwezi kuletwa na kiungo cha albino, isipokuwa ni juhudi na maarifa.

Watu wa aina hii wanaifanya vita dhidi ya wauaji wa albino kuwa endelevu. Watu hawa wanapaswa kushughulikiwa mara moja na mkono mrefu wa dola.

CHANZO: NIPASHE
 
Chanzo kikubwa cha mauaji ya maalubino ni ushirikina unawahusisha watanzania wenye uchu wa madaraka katika siasa vyeo maofisini tamaa ya pesa au mali migodini na wavuvi suluhisho ni nchi kuwa na utashi wa kisiasa vigogo wengi nchi ni washiriki wa unyama huu ndo maana haliishi na kipindi hiki cha maandalizi ya uchaguzi mkuu.
 
Back
Top Bottom