SoC01 Vita ya pili ya Chimurega: Mapambano ya Afrika yanaendelea

SoC01 Vita ya pili ya Chimurega: Mapambano ya Afrika yanaendelea

Stories of Change - 2021 Competition
Joined
Jul 15, 2021
Posts
16
Reaction score
61
Ni mwaka mmoja sasa tangu Ndugu yetu Benjamin William Mkapa alivyotangulia mbele za haki tarehe 24 Mwezi wa Julai mwaka 2020. Nitumie fursa hii kushiriki nanyi kurejea hekima zake ili zituongoze kuleta maendeleo endelevu nchini kwetu.

Nianze kwa kukiri kuazima kichwa cha habari kutoka kwenye kitabu cha Rais mstaafu ndugu Benjamin William Mkapa kijulikanacho kama My Life, My Purpose (Kwa tafsiri yangu Maisha Yangu, Kusudi Langu). Katika kitabu hiki ndugu Mkapa ameeleza vyema historia yake, uzoefu wake kwenye siasa na uongozi na pia ametumia muda mwingi kuhoji mambo ya msingi huku akitukumbusha wajibu wetu kama taifa kwa ujumla.

Sura ya mwisho ya kitabu chake ndugu Mkapa yenye kichwa cha habari tajwa hapo juu imenisukuma kusisitiza mambo ya msingi ambayo ndugu Mkapa amehoji kwa uchungu mkubwa. Nikianza wa wasiofahamu vita ya kwanza ya Chimurenga (1896-97) ilikuwa na nia ya kupinga utawala wa kikoloni kupata uhuru kwenye jamii ya watu wa Zimbabwe kama moja wapo ya jitihada za kupinga ukandamizaji na uonevu.

Kwa msisitizo mkubwa Ndugu Mkapa anahoji maendeleo endelevu yatokanayo na ubadilishwaji wa viongozi barani Afrika. Ni ukweli kuwa, kila kiongozi akichaguliwa anakuja na maono, mikakati na mipango yake huku akitupilia mbali kile alichokikuta kimefanywa na watangulizi wake. Hii kwa kiasi kikubwa kimekuwa changamoto kubwa barani Afrika ambapo tunaona kwenye nchi nyingi mabadiliko ya sera na mipango kila mara inayopolekea kutokuwa na muendelezo endelevu. Kutambua juhudi za viongozi watangulizi ni muhimu kwani kipindi chao madarakani hakikuwa cha bure, walifanya mazuri ambayo ni busara kuyaendeleza ili kuwe na msisitizo kama chombo kimoja.

Ni muhimu sasa serikali zetu zikaweka mifumo ya lazima ya kuhakikisha kunakuwa na muendelezo wa sera na mipango kutoka uongozi mmoja kwenda mwingine ili kuondoa mianya ya kila kiongozi kuja na mbinu zake huku tukipoteza muda pesa nyingi kutupilia jitihada zilizopita. Nisisitize ni muhimu kwa nchi za Afrika kuwa na mifumo imara itakayosimamiwa na viongozi bora na hapa ni muhimu nguvu kubwa iwekwe kwenye mfumo badala ya watu maana mfumo ukiwa dhaifu basi watu watauchezea na kukosa muendelezo.

Kwenye sura hii pia Ndugu Mkapa ameeleza wazi na nakubaliana nae fika ya kuwa, mapambano ya awali na wakolini ambapo vita ya kwanza ya Chimurenga ilitokea ilikuwa nikupambana na adui tuliyekuwa tunamuona na hatima ya vita ile ilikuwa uhuru. Vita hiyo imepiganwa na imefanikiwa, sasa vita ya pili ya Chimurenga ndo ngumu zaidi maana adui haonekani kirahisi, ana mbinu nyingi tena zenye kubadilika. Kwenye vita hii ni muhimu kuhakikisha ukombozi wa kiuchumi na kuwaondoa watu kwenye umaskini unakuwa wa dhati kabisa bila ya kuweka rehani urithi wetu wa Afrika, utamaduni wetu, utu wetu na uwezo wetu wa kufikiri kama waafrika.

Ukitizama miaka 57 tangu uhuru wa nchi nyingi za Afrika bado utegemezi kwa wadau au wahisani wa maendeleo ni mkubwa sana kuanzia Marekani, Ulaya na sasa China ambako bila kujali utu wetu, tamaduni zetu tuko radhi kuyasahau hayo yote kisa tunataka misaada ama misamaha ya mikopo. Tunasahau jukumu letu kama bara la Afrika kuwa na maendeleo ya kujitegemea ambayo yatakuwa na maslahi mapana kwa watu bila kuathiriwa na mtakwa ya wale wanaotoa masharti magumu ya misaada ya maendeleo. Hapa ndipo Ndugu Mkapa anaposikitishwa kuona miaka 50 baada ya uhuru nchini Tanzania bado hatuna vyoo vya kutosha kwenye shule zetu na cha kustaajabisha zaidi vyoo vya shule vinajengwa kwa msaada wa wafadhili na wahisani na tunaweka nembo kabisa tukifurahia msaada wa vyoo hivi.

Swali la Ndugu Mkapa: Maendeleo ya kujitegemea kama taifa yako wapi kama tunashindwa hata kujenga vyoo vya shule zetu? Hapa ndipo tunapoona umuhimu wa wanajamii kuchukua jukumu la kufanya mambo bila kuisubiri serikali kufanya kwa niaba yao kama tulivyosisitizwa kwenye Ujamaa na Kujitegema. Kwanini wananchi wa shule husika wasichange ama kujenga vyoo wenyewe ili Watoto wao waweze kupata sehemu salama ya kujisitiri badala ya kusubir msaada kutoka nje kuja kuenga vyoo kwa Watoto wetu.

Katika sura hii pia Ndugu Mkapa amesisitiza dhana nzima ya maendeleo na namna tunavyotafsiri maendeleo. Wengi wetu tunatafsiri maendeleo kama vitu pindi tunapona miundombinu imara, umeme, maji, majengo na mengine mengi tunasema tumeendelea. Swali la msingi, je, ikifika kipindi miundombinu hii imechakaa ama kuharibika tunaweza kuitengeneza wenyewe? Kama jibu tunaweza kuikarabati wenyewe na kufanya iwe endelevu basi hayo ni maendeleo ila kama jibu ni hatuwezi kuikarabati na kuiendeleza mpaka tupate msaada kutoka kwa wafadhili basi vitu vyote hivyo vinakosa uhalali wa maendeleo na hivyo sio maendeleo. Msisitizo wangu hapa ni kwamba, kufikia maendeleo endelevu kama waafrika cha msingi kabisa tuweke msisitizo kwenye ubora wa watu na shughuli za uzalishaji kama kilimo vinaweza kuzalisha faida ya kutosha kuweza kuendeleza miundombinu yote inayoanzishwa.

Maneno mengi aliyoyasema Ndugu Mkapa yana ukweli na kilichonivutia zaidi ni kwasababu amekuwa kiongozi wa nchi ameshiriki kufanya mambo mengi na baada ya kutoka kwenye uongozi ni Dhahiri anaona mapengo na kutumia fursa ya kuandika kama alivyofanya inatupa wajibu sisi kujifunza na pia kufanya mabadiliko. Ndugu Mkapa hajaandika kutoka kwenye nadharia kwani ananyoyasema ameyaishi na kuyajaribu, kuna alipokwama lakini alijiribu hivyo uzoefu wake huu ni muhimu kufahamu na kuchukua jukumu kama wananchi.

Kitu kikubwa ambacho naweza kusisitiza hapa, maendeleo ni kazi yetu sote wananchi na sio kazi ya serikali pekee, ni Dhahiri bila sisi wananchi hakuna serikali basi kwanini tuitegemee serikali kuleta maendeleo huku sisi tumejitenga? Ni muhimu kama wananchi kuhoji serikali, kufanya kazi kwa nafasi zetu na kwenye jamii zetu, kuchagua viongozi bora na kuionya serikali. Kwa kufanya hivyi ndipo tunaposema tunashiriki kwenye kuleta maendeleo ya kujitegemea lakini pindi tunapojitenga na kuitegemea serikali ifanye huku sisi tukilaumu na kuendelea kusubiri maendeleo kama mana jangwani.

Ni jukumu letu kama wananchi na waafrika kwa ujumla kuanzisha vita ya pili ya Chimurenga yenye nia ya kujikomboa sisi wenyewe kwenye nyakati hizi za vita ya kiuchumi, kitamaduni, unyonyaji, na ukoloni mambo leo. Hakuna wenye jukumu la kupigana vita imara kama wananchi wenyewe.
 
Upvote 27
Back
Top Bottom