Elias Msuya
Platinum Member
- Dec 23, 2011
- 267
- 1,014
Vital Kamerhe, rais wa zamani wa Bunge la Taifa la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), amekosoa hatua ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila, kuongoza kundi jipya la kisiasa na kijeshi linaloitwa Front pour la Refondation de la Nation (FRN), akisema hatua hiyo akisema hatua hiyo inakinzana na kauli zake za kutaka amani nchini humo.
Soma zaidi: Joseph Kabila atangazwa kuwa kiongozi wa kundi jipya la kijeshi na kisiasa DRC
Katika taarifa iliyotolewa Jumatano, Oktoba 14, 2026, Kamerhe amesema Kabila hawezi kuzungumzia amani huku akihusishwa na harakati za kutumia silaha.
“Mnatoa wito wa amani katika hotuba zenu, lakini kwa vitendo mnatoa wito wa uasi. Wananchi watawahukumu kwa matendo yenu,” amesema Kamerhe, akimlenga Kabila.
Kamerhe ambaye ni mbunge na kiongozi wa chama cha Union pour la Nation Congolaise (UNC), pia amesisitiza kuwa matatizo ya DRC hayawezi kutatuliwa kwa kuanzisha mapambano mapya ya kijeshi, akimtaka Kabila awajibike kwa sehemu yake katika historia ya kisiasa ya nchi hiyo badala ya kulaumu utawala wa sasa.
Aidha, alitoa wito kwa Wakongo kuweka kando tofauti zao za kisiasa na kuungana kwa njia za amani kulinda mamlaka ya taifa, uadilifu wa mipaka na utaratibu wa kikatiba.
Alipinga matumizi ya uasi kama njia ya kupata madaraka, akieleza kuwa mazungumzo ndiyo yanayopaswa kupewa kipaumbele badala ya mapigano yanayoweza kusababisha vifo na kuongeza machafuko.
Kauli hiyo imekuja siku mbili baada ya Kabila kutangaza kuanzishwa kwa FRN mjini Goma, mashariki mwa DRC, ikiwa ni muungano mpya wa kisiasa na kijeshi unaohusisha makundi ya waasi, yakiwemo M23 na Alliance Fleuve Congo (AFC), yanayopambana na Serikali ya Rais Félix Tshisekedi.
Kabila, ambaye aliiongoza DRC kuanzia mwaka 2001 hadi 2019, anakuwa kiongozi mkuu wa muungano huo ambao umetangaza dhamira ya kupinga utawala wa Tshisekedi, kwa kutumia njia mbalimbali, ikiwemo nguvu za kijeshi.