Wadau wote,
Ninafuraha kubwa kuwajulisha kuwa jana tumeandikisha mwanachama mpya wa SACCOS yetu mpya. Ingawa tumeshaandikisha wanachama wengi wapya kabla yake lakini huyu imebidi niiweke bayana furaha yangu kwa kujiunga kwake nasi.
Si mwingine bali ni Bi Thureya Mohamed Sheikh wa Vitendo, Misugusugu. Bi Thureya ni mwanamama mmoja shupavu sana, aliyejitolea maisha yake yote ya ujana kuwakomboa watoto na vijana wasio na bahati.
Hapa kwetu Misugusugu Bi Thureya ni maarufu sana kwa ujasiri wake, moja katika sifa zake ni anapokuta mtoto hana malezi mazuri basi hufanya kila jitihada kuwajua wazazi wake na kuanza kuwaelekeza kuwasomesha na ikishindakana wazazi kubadilika basi huwachukua hao watoto na kuwalea yeye kwenye kituo chake.
Mpaka sasa Bi Thureya ameweza kuwasomesha watoto wengi sana kwenye shule za malipo ambazo kwa wengine huwa ni ndoto tu, ameweza ku lob, kupigana na hatimae kupatiwa nafasi za masomo kwa watoto wasio na bahati.
Hivi karibuni ameweza kupigania mpaka ameweza kujengesha shule ya chekechea na msingi usoni mwa nyumba yake.
Kituo cha Bi Thureya ni tofauti na vituo vingine vyote nilivyowahi kuviona vya kulelea yatima na watoto wasio na bahati, ukifika kituo chake utakuta yeye mwenyewe anaishi nao hao watoto hapo hapo akihakikisha wanapata "close nurturing" kama wanawe mwenyewe ambao nao wanaishi wote hapo hapo. Shule wanazosoma wanawe ndizo shule hizo hizo wanaenda watoto na vijana anaowalea hapo.
Bi Thureya ni mchapa kazi, mwanaharakati na mama mwenye huruma kubwa na mwenye uchungu sana na maendeleo ya jamii.
Binafsi humuita Bi Thureya "commando" maana ayafanyayo ni ukomando kweli kweli na si rahisi kwa mtu asiye na moyo wa kikomando kama Bi Thureya.
Kuna mengi sana mema ya kuuelezea wasifu wa Bi Thureya lakini ipo siku tutaandika wasifu wake kwa kina, kwa leo niishie hapo kwa kuiweka furaha yangu bayana kwa uwepo wake kwenye sacos yetu mpya.
Hakika ni mwanamke shupavu.
Tuna furaha kubwa kuwa nae katika saccos yetu mpya, tuna mengi sana ya kufaidika nayo kutoka kwake.