SoC01 Vitendo vya ubakaji na ulawiti kwa watoto wadogo; Je, tunawajibika ipasavyo kupambana na vitendo hivi?

SoC01 Vitendo vya ubakaji na ulawiti kwa watoto wadogo; Je, tunawajibika ipasavyo kupambana na vitendo hivi?

Stories of Change - 2021 Competition
Joined
Jan 22, 2020
Posts
27
Reaction score
35
Kumekua na matukio mengi ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto wetu wa kike na wa kiume. Kwa ujumla yapo matukio mengi ya kikatili kwa watoto lakini katika makala hii nitazungumzia zaidi ubakaji na ulawiti kwa watoto wa kike na wa kiume. Katika hali ya kusikitisha sana matukio haya yamezidi kushamiri kila kukicha.

Kinachoshangaza na kuumiza zaidi, wakati mwingine watoto wamekua wanafanyiwa ukatili huu na watu ambao wameaminika na wazazi. Watu hao ni kama baba mzazi au wa kufikia, ndugu wa karibu, wasaidizi wa kazi za nyumbani, au walimu wa shuleni wanaposoma watoto. Licha ya kuwaachia wazazi maumivu makubwa na makali mno, matukio haya yamekua na madhara ya moja kwa moja kwa watoto waliofanyiwa vitendo hivi.

Madhara hayo ni kama kuathirika kisaikolojia kama kukosa kujiamini na kujithamini, hali ambayo inaathiri hatma na mustakabali wa maisha ya muathirika. Pia vitendo hivi vinaweza kumsababishia muathirika maambukizi ya magonjwa ya zinaa kama UKIMWI na mengineyo. Kabla ya kuendelea ningependa kuonyesha ripoti kadhaa zinazozungumzia kadhia hii. Kuna ripoti hii Tanzania: Ukatili dhidi ya watoto waongezeka, polisi | DW | 28.04.2021 kutoka tovuti ya www.dw.com. Pia kuna ripoti nyingine juu ya kadhia hii inayopatikana tovuti ya www.bbc.com kupitia hapa Kwanini matukio ya ubakaji na ulawiti yameshamiri visiwani Zanzibar? - BBC News Swahili. Pia kuna ripoti nyingine Kanda ya Ziwa yatajwa kuwa kinara wa matukio ya ukatili kwa watoto – Dar24 inayopatikana katika tovuti ya www.dar24.com.

Zipo sababu mbalimbali zinazopelekea kutokea kwa matukio haya. Sababu ya kwanza ni ongezeko la watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Watoto hawa kwa ujumla wanakosa mtu wa kuwalea na kuwaongoza hivyo kuwaingiza moja kwa moja katika mazingira magumu na hatarishi. Katika harakati za kujitafutia mahitaji muhimu kama chakula na mahitaji mengine, watoto hawa hukutana na watu ambao sio wema ambao hutumia shida za watoto hawa kama fursa ya kuwafanyia vitendo vya kikatili kama ulawiti na ubakaji.

Sababu nyingine ni kuongezeka kwa watoto wengi wanaolelewa na mzazi mmoja. Kuna tofauti kubwa kati ya mtoto anayelelewa na mzazi mmoja na mtoto anayelelewa na wazazi wote wawili. Mtoto anayelelewa na wazazi wote wawili ana uwezekano mkubwa wa kuwa katika hali ya usalama zaidi kwa sababu ni rahisi wazazi kugawana majukumu. Wakati mzazi mmoja akiwa katika mihangaiko ya kutafuta mkate wa kila siku, mzazi mwingine anaweza kuwa nyumbani kwa ajili ya kuangalia familia, hivyo watoto wakawa kwenye hali ya usalama.

Kwa upande wa mtoto anayelelewa na mzazi mmoja tu kwa asilimia kubwa anakua na changamoto ya usalama wake, hii ni kwa sababu mzazi anapokua katika mihangaiko ya kutafuta mkate wa kila siku analazimika kumuacha mtoto kwa msaidizi wa kazi nyumbani, kwa ndugu, kwa jirani au kumuacha peke yake, hali ambayo haikikishi usalama kwa mtoto kwa asilimia mia moja. Vilevile mtoto wa kike anayeishi na mzazi mmoja wa kiume anaweza pia kufanyiwa ukatili wa kijinsia na mzazi huyo. Sababu nyingine pia ni mabadiliko ya kimaadili ndani ya jamii. Tofauti na miaka ya nyuma kidogo, siku hizi tumekua na jamii iliyopotoka kimaadili na isiyo na hofu ya Mungu.

Jamii ambayo kipindi cha miaka ya nyuma kidogo ilikua sehemu ya ulinzi wa watoto, leo imegeuka na kuwa tishio kubwa kwa usalama wa watoto. Kwa starehe na tamaa ya muda mfupi tuko tayari kufanya ukatili kwa watoto wadogo ambao matokeo yake ni kuharibu kabisa mustakabali wa maisha ya watoto hawa. Tumekua wababa ambao tunawageuka watoto wetu wa kuwazaa wenyewe na kuwatendea vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Tumekua wazazi tunaozaa watoto na kuwapeleka vijijini ili wakalelewe na ndugu zetu ili pengine tubaki tukiwa huru mjini. Tumekua wababa ambao hatutaki kuwajibika kwa hali na mali kuwalea watoto tuliowazaa na kuacha mzigo wote kwa mama wa mtoto, hali ambayo kwa namna moja au nyingine inaathiri pia malezi ya mtoto na usalama wake kwa ujumla.

Nisingependa kusema nawalaumu wazazi moja kwa moja kwa kadhia hii, kwa sababu wakati mwingine changamoto mbalimbali za kimaisha ambazo hazikwepeki, ikiwemo hali ya uchumi inaweza kuwa sababu ya tatizo kwa namna moja au nyingine. Lakini niseme, wazazi kama mlinzi namba moja wa mtoto hatuwajibiki vizuri katika ulinzi wa watoto wetu. Au hata kama tunawajibika basi hatuwajibiki vya kutosha au inavyotakiwa.

Pamoja na changamoto ya kuwa na majukumu mengine ya kutafuta mkate wa kila siku, tusijisahau na kuwaachia wasaidizi wa kazi nyumbani au ndugu na kuwaamini kwa asilimia mia moja juu ya usalama wa watoto wetu. Tujenge utamaduni wa kuwafanyia watoto wetu uchunguzi wa mahojiano na miili yao, ikiwezekana kila siku.

Hii ni kwa sababu wazazi wengi wamekua wanagundua kuwa watoto wao wamefanyiwa ukatili wa ubakaji au ulawiti kipindi ambacho wameshachelewa. Laiti kama wazazi hawa wangekuwa wanawafanyia uchunguzi watoto wao, pengine wangeweza kugundua tatizo hili mapema, kabla madhara hayajawa makubwa zaidi. Ni kosa kubwa sana kusubiri mtoto mwenyewe aje akuambie kuwa anapitia ukatili wa kubakwa au kulawitiwa, kwa sababu watu wanaowafanyia vitendo hivyo huwarubuni kwa vitu wanavyopenda kama pipi na biskuti, na wengine huenda mbali zaidi kwa kuwatishia maisha endapo wataripoti ukatili huo kwa mtu yoyote.

Pia tuwafundishe watoto wetu kujilinda wenyewe tangu wakiwa wadogo kabisa , kwamba wasiruhusu mtu yoyote aguse sehemu zao za siri. Watoto ni viumbe waaminifu na wa kweli, wakifundishwa hivyo watatoa taarifa pindi tu wanapotendewa vitendo hivyo. Lakini pia wazazi tusiwaachie ndugu (bibi, mjomba, shangazi) jukumu la kulea watoto wetu, tulee watoto wetu wenyewe. Hii ni kwa sababu ndugu nao wamekua sehemu kubwa ya watu wanaowafanyia vitendo vya ukatili. Lakini pia kama ikibidi kuwaachia ndugu majukumu ya malezi, tufuatilie kwa ukaribu usalama wa watoto wetu.

Na sisi ndugu tunapoachiwa majukumu ya kulea watoto, tuwe walinzi namba moja kwa watoto hawa. Tusimame kwenye nafasi ya mzazi kama nilivyoeleza hapo juu. Lakini pia wazazi tusikae kimya pale mzazi mwenza (mfano baba mzazi au baba wa kufikia) anapofanya vitendo hivi vya ukatili kwa mtoto. Hii ni kwa sababu mara kwa mara kumekua na vitendo vya ukatili kutoka kwa baba dhidi ya mtoto wake mwenyewe au mtoto wa kufikia.

Matukio haya yamekua yanakaliwa kimya kwa mwanamke kuhofu kwamba akichukua hatua za kisheria dhidi ya baba anayefanya vitendo vya ukatili kwa watoto, maisha yanaweza kuwa magumu kwa sababu baba huyo ndiye anayemlea yeye na watoto wake. Lakini pia matukio haya yamekua yananyamaziwa ili kuficha aibu, na wakati mwingine ndugu wa karibu wa aliyetenda ukatili hujitokeza na kutaka mambo yamaliziwe nyumbani.

Fikra za namna hii zinashangaza sana kwa sababu kama mtu ameweza kumfanyia ukatili mtoto wake mwenyewe, ni kitu gani kingine unasubiri afanye ili uamini kuwa huyu mtu sio mwema? Kina mama tuvunje ukimya dhidi ya matendo haya, mtoto wako ana thamani kuliko mahitaji unayoyapata kutoka kwa mwanaume katili. Lakini pia ndugu tunaojitokeza kutetea mtu aliyetenda kitendo hiki tunafanya makosa makubwa sana, kwa sababu kama mtu ameweza kutenda ukatili kwa mtoto wake mwenyewe, kesho na kesho kutwa anaweza kufanya ukatili huohuo kwa mtoto wako wewe unayemtetea leo.

Pia niendelee kuihimiza jamii iendelee kutoa taarifa kwa vyombo vya sheria pale tu inapopata taarifa ya uwepo wa vitendo vya ukatili au viashiria vya vitendo hivyo. Hili ni jukumu la kila mmoja wetu kwa sababu leo unaweza kunyamazia vitendo hivi dhidi ya mtoto wa mwezio, lakini kesho au kesho kutwa mtoto wako akafanyiwa vitendo hivi.

Lakini pia niishauri serikali iendelee kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya watu wanaothibitika kufanya vitendo hivi kwa watoto. Pia niishauri serikali iangalie namna gani inaweza kumaliza tatizo la uwepo wa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Serikali inaweza kutoa ruzuku kwa vituo vinavyowasaidia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi ili kuviongezea vituo hivyo uwezo na hamasa zaidi ya kuwatunza watoto hawa. Lakini pia serikali inaweza kutumia nafasi na ushawishi wake kutafuta wafadhili ambao wanaweza kuiongezea serikali uwezo wa kutatua tatizo la watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi.

Kama serikali imeweza kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi mpaka sekondari, basi inaweza kumaliza tatizo la watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Watoto hawa ambao ndio taifa la kesho wanaweza kukuzwa na kuwa na mchango kwa taifa lao kama watoto wengine. Nihitimishe kwa kutoa rai yangu kwa wazazi kwamba kama kuna mtu mmoja tu ambaye unatakiwa kumuamini kuhusu suala la usalama wa mtoto wako, basi mtu huyo ni wewe mwenyewe.

Ifuatayo ni video fupi kutoka mtandao wa www.youtube.com inayoonyesha simulizi ya moja ya matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto​

 
Upvote 0
Back
Top Bottom