Vitisho havijawahi kuleta 'Upendo' na Umoja ndani ya Taifa

Vitisho havijawahi kuleta 'Upendo' na Umoja ndani ya Taifa

Robert Heriel Mtibeli

Platinum Member
Joined
Mar 24, 2018
Posts
40,153
Reaction score
93,069
VITISHO HAVIJAWAHI KULETA UPENDO NA UMOJA NDANI YA TAIFA.

Kwa Mkono wa, Robert Heriel

Nianze kwa Kumshukuru Mungu mwenye uweza, huyo aliyeumba mbingu na nchi. Sifa njema zimfikie yeye pekee wala hakuna mwingine zaidi yake.

Suala la vitisho ni suala la kawaida sana hasa katika jamii ya watu wajinga wasio na elimu, na jamii ya watu masikini.
Ndani ya familia kwenye majumba yetu ni kawaida kwa wazazi kuwatisha watoto, ni kawaida kwa Baba kumtisha Mama/mke wake. Zingatia kanuni ni ile ile, ili vitisho viwepo ni lazima ujinga na umasikini uwepo eneo husika. Baba akimuona Mama/mkewe ni mjinga yaani hana elimu na ni masikini ni kawaida sana kumtisha. Kumtisha kunaendana sambamba na kumfanyia ukatili kama kumpiga wengine kuua kabisa, kumnyanyasa na kumdhalilisha kwa maneno ya masimango na matusi.

Wababa wenye vitisho wengi hutumia udhaifu wa wake zao kuwatisha, mwanamke akishakuwa mjinga na masikini kwao kutishwa na mwanaume ni jambo la kawaida. Lakini Vitisho pia hutumiwa na watu wenye kutaka kuogopwa, kujifanya miungu watu. Ndani ya familia wababa wenye vitabia hivi vya kipuuzi ni kawaida yao kutoa vitisho vya kipumbavu kama hivi. Unakuta mwanaume kutwa kumtisha mkewe, ooh! nitakurudisha kwenu, mara makofi, mara viboko, mara unajua mimi ndiye nalisha familia. Wababa wa hivi wengi ni wa hovyo, yeye hakosei kwa sababu ni mungu mtu, yeye ruhusa kuchepuka na wanawake wengine lakini mkewe hataki hata asalimiwe na jirani, yeye ruhusa kuchelewa nyumbani lakini mkewe achelewe siku moja aone kichapo chake. Wababa wa hivi huwa nawaitaga ni vichaa, wasio na akili nzuri. Mtu yeyeto anayejifanya yuko above the law ni mwendawazimu, na kichaa asiye na akili sawa sawa. Ni mtu anayejifanya mungu mtu wakati hana lolote.

Kikawaida vitisho huzaa chuki, ukiwa na tabia ya kumtisha mkeo unatengeneza bomu la chuki ndani ya nyumba yako. Hakuna Baba aliyejifanya mtu wa vitisho akabaki salama ndani ya nyumba yake, lazima itamrudia yeye mwenyewe ile chuki aliyoijenga. Kikawaida mtu anayetoa vitisho huishi kwa wasiwasi, Baba anayetoa vitisho ndani ya nyumba huishia kuumwa magonjwa ya moyo ya wasiwasi, anaogopa na hamuamini mke wake. Huwezi mtisha mtu alafu ukajidanganya kuwa yameisha huo ndio ukweli. Hata hivyo, moja ya sababu kwa nini wanaume wanakufa mapema kuliko wanawake ni pamoja na kupenda Vitisho vya kipuuzi puuzi. Wanaume wanaopenda vitisho kwa wake zao pasipo sababu ya maana huishia kufa mapema na wengi hawatoboi miaka 70 wakijitahidi sana ni 50. Upendo ni kinyume na vitisho.

Narudia na kusisitiza, watu wanaopenda vitisho huishia kupata magonjwa ya wasiwasi yanayohusu afya ya ndani kabisa ya moyo na ubongo.

Wazazi wenye vitisho kwa watoto wao mara zote huwajengea chuki watoto wao. Watoto hutishwa kwa ukosefu wao wa kujua mambo mengi, pia watoto hutishwa kwa kuwa hawana kimbilio lingine zaidi ya palepale nyumbani. Kumtisha mtoto ni mafunzo yenye kuamsha ari ya chuki na ubinafsi.
Mzazi hutisha mtoto kwa kumwambia nitakulaani, sijui kama sijabeba mimba yako miezi tisa, mwingine husema, nitavua nguo, basi ilimradi kumjengea mtoto hofu, kumbuka mambo haya yapo kwenye jamii masikini hasa Barani Afrika. Mzazi kumrithisha mtoto elimu potofu kuwa "Mzazi hakosei" jambo ambalo ni uongo wa mchana. Lengo ni kutotaka kukosolewa na kuonywa na mtoto wake. Jamii zenye mila potofu huamini kuwa mzazi hawezi kumuomba msamaha mtoto wake wa kumzaa, bila shaka ni ile kanuni potofu niliyoitaja kuwa 'mzazi hakosei'

Mzazi hakosei kiaje? Yeye ni Mungu? Haya makosa wanayotenda kila siku tunayaona ni nini? wanatufanya hatuna macho? Hata hivyo mimi nami ni mzazi, mbona kila siku nakosea na naona kabisa nakosea, sasa hayo yakusema mzazi hakosea yametoka wapi, au ndio kujifanya mungu mtu. Nilishasema kabisa, wanangu wakiniona nakosea waniambie, wasiniletee unafiki watakaousikia nje huko kuwa ati mzazi sikosei. Watoto wametishwa kuwa wasiseme pale wakubwa wanapofanya makosa, hiyo ni mila potofu iliyopitwa na wakati, tena iliyokatika jamii isiyo na uelewa wa mambo.

Watoto waliozea kutishwa mara zote hawanaga upendo, wanaishi kinafiki na wanaunda jamii ya kinafiki, yaani wao kkila kitu unafiki tuu.

Vitisho huzaa unafiki ndani ya familia, jamii na taifa kwa ujumla.

Huko makanisani na misikitini vitisho navyo havikosekani, ninyi mnafundisha upendo alafu muda huo mtishia watu. Mungu ni upendo, upendo ni kinyume na vitisho. Unakuta baadhi ya wachungaji hutishia watu wanapowakosoa na kuwarekebisha, hutumia vifungu kwamba "usimnyooshee kidole mtumishi wa Mungu" sijui usimseme mpakwa mafuta wa Bwana, wewe kama umpakwa mafuta basi usikosee na usifanye makosa, lakini unafanya makosa tunakuona alafu unasema tusikukosoa hiyo sio kweli, tutakukosoa dunia ingalipo sisi tukiwepo. Acha kutisha watu. Wewe/Mimi sio lolote na unajijua hivyo.

Ngazi ya taifa, wapo viongozi ambao hujifanya wao ni miungu, wakisimama mbele ya majukwaa huongea kana kwamba hawana akili. Vitisho mwanzo mwisho, mbaya zaidi badala watishie waovu matokeo yake hutishia mpaka watetezi wa haki. Hiyo sio sawa.

Wewe mtu kukuambia ukweli ndio umtishe, kama hakuogopa kuongea ukweli atakuogopa wewe ambaye fika unajijua huna lolote zaidi ya kujidanganya na kuihadaa nafsi yako kuwa unaogopeka. Uogopeke kwa kipi hasa, elimu? au utajiri? au uzuri? au mamlaka? embu wewe jiulize mwenyewe uogopeke kwa kipi hasa. Kila siku nawaambia, ukitenda mema ndio utaogopeka kwa sababu Mungu anakaa ndani yako, na si zaidi ya hapo.

Kuliko utumie Vitisho ni bora muda huo uwape watu mafundisho ya upendo, watu wapendane, wape njia ya watu kupendana, wape elimuya utambuzi, wape elimu ya uzalishaji mali, wape elimu ya kulinda afya zao, wape elimu ya umuhimu wa kuijenga nchi yao kwa njia ya kulipa kodi, wape elimu, elimu, elimu, elimu.

Unakuta lichungaji badala litoe elimu ya umuhimu wa kumtolea Mungu sadaka, linatishia watu, sijui hutaenda mbinguni, sijui utachomwa, sijui moto wa jehanamu ni mkali yaani vitisho vitisho tuu. Alafu fuatilia dini zenye vitisho mara nyingi hazina upendo, watu hawatoi sadaka kwa sababu ya vitisho.

Wachungaji wanatishia watu mpaka watu wanamchukia Mungu wao. Unapotishia waumini wako jua unatengeneza chuki ndani ya waumini wako kwa Mungu.

Mchungaji mmoja wa dini fulani alinitishia; nikamjibu kuwa; kwani nikichomwa wewe inakuhusu nini? au huyo unayenitishia naye aliyemwambia aniumbe ni nani? Kama aliniumba kwa upendo basi nifundisheni kwa upendo, kama aliniumba kwa chuki basi endeleeni kunitishia. Wala sitafuata mnayoyasema maana najua hamkutuwa bali mlijituma wenyewe.

Fundisheni upendo, watu wapendane, wasiibiane, wasidhulumiane, wasinyimane haki, hivyo yaani.

Huwa nawaonea sana huruma Polisi, kazi yao ni ngumu sana, wao hufuata Oda tuu na hawaruhusiwi kupinga. Nafikiri ipo haja ya wananchi kuchagua viongozi waadilifu ili kuwapunguzia mzigo Polisi wetu, tunajua polisi ni moja ya ndugu zetu, ni watu kama sisi, wapo kaka zetu, wake, waume, na marafiki zetu. Inanisikitisha sana kuona wakitumika vibaya.

Vitisho havijawahi leta upendo na umoja, vitisho huleta Unafiki na chuki.

Ulikuwa nami mwana wa nyota ya Tibeli, nyota yenye mbawa mbili irukayo kutoka upande huu kwenda upande huu.

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300
Kwa sasa Dodoma.
 
Back
Top Bottom