Viungo wakabaji watano bora zaidi duniani

Viungo wakabaji watano bora zaidi duniani

Kwenye holding midfield kwangu Mimi nampa SCOTT PARKER kama mnamkumbuka huyu mzungu alikuwa noma saana kwenye dimba LA chini akiwa na spurs kama sijakosea.
 
Siku hizi nafasi hii imekuwa msaada mkubwa kwa walinzi na nafasi yao ni kucheza kwa kuwasaidia walinzi na pia wakiwa na nafasi ya kutengeneza mashambulizi.

Viungo kama Claude Makelele, Patrik Vieira, Frank Rijkaard na Roy Keane walishaonyesha kile walichokuwa nacho kwenye nafasi ya kiungo mkabaji wakati wao wa uchezaji na kuzisaidia timu zao kutwaa mataji mbalimbali.

Majina ya wachezaji hao ndio kwa kiasi kikubwa yameonyesha umuhimu wa kiungo mkabaji na mwenye uwezo wa kukaa na kugawa mipira sehemu mbalimbali na pia kuliwalisha washambuliaji wake.

Kwa wakati huu kuna wachezaji kadhaa wameonekana kuwa na mafanikio kwenye nafasi hiyo. Na mara nyingi wachezaji wa nafasi hii huonekana kuwa ndio viongozi wa timu.

Makala hii inawaangalia viungo wakabaji watano ambao ndio bora zaidi kwa soka la sasa duniani:

5. Rodri (Manchester City)

Huyu ni mchezaji mwenye umri wa miaka 23, raia wa Hispania na amekuwa nguzo muhimu kwa kikosi cha Manchester City kwenye safu ya kiungo mkabaji pale kati tangu alipotua hapo akitokea Atletico Madrid kipindi cha majira ya joto kilichopita.
Akitarajiwa kuwa ndiye mrithi wa muda mrefu wa Fernandinho, Rodri amekuwa na uwezo wa kukaba kukaa na mpira na kutengeneza pasi zenye macho, huku pia akiwa na uwezo wa kusukumiza mashambulizi mbele.
Akiwa amecheza mechi 16 kwa City, takwimu zake zinaonyesha kwamba ana wastani wa kukaba wa 2.5, huku akiwa na pasi zenye uhakika wa asilimia 93. Katika umri wake wa miaka 23, ameonyesha kwamba anaweza kuimarika zaidi na kuwa nguzo muhimu zaidi katika kikosi cha timu hiyo kwenye safu ya kiungo kwa siku zijazo.

4. Casemiro (Real Madrid)
Kiungo huyu wa kimataifa wa Brazil, Casemiro amekuwa nyuma ya mafanikio yote ya Real Madrid katika miaka ya hivi karibuni akijiimarisha yeye mwenyewe kuwa mmoja wa wachezaji bora zaidi wa safu ya kiungo mkabaji duniani kwa sasa.

Casemiro, ameshinda mataji manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Madrid, na amekuwa mmoja wa wachezaji wenye kipaji kisichochuja chenye mwendelezo chanya kwa kipindi cha misimu kadhaa sasa.
Katika umri wake wa miaka 27 amecheza kila mechi kwenye Ligi Kuu Hispania, La Liga, msimu huu na amekuwa na uwezo wa kukaba wa kiwango cha 3.7.

3. Sergio Busquets ( Barcelona)
Mmoja wa viungo wenye ‘udambwi udambwi’ mwingi zaidi wa wakati wote, Sergio Busquets ambaye historia itamkumbuka kwa miaka mingi kuwa ndiye mmoja wa viungo wakabaji bora zaidi kuwahi kutokea katika nafasi hiyo.
Mhitimu huyu wa chuo cha kulelea vipaji vya soka cha pale La Masia amekuwa kama nguzo muhimu wa Barcelona kwenye nafasi ya kiungo kwa miaka mingi. Amebarikiwa uwezo na kipaji cha aina yake na kutawanya mipira na kumiliki mpira akiwa eneo lake la kujidai.

Raia huyu wa Hispania mwenye umri wa miaka 31 amecheza mechi 16 kati ya 18 msimu huu na anahitaji kuendelea kuwa kwenye kiwango chake bora ili Blaugrana hao waweze kutetea taji lao msimu huu.

2. Fabinho (Liverpool)
Baada ya kuanza taratibu maisha ya soka pale kwenye dimba la Anfield, Fabinho sasa anaonekana kama ameonyesha ubora wake na mmoja wa wachezaji muhimu zaidi wa kikosi hicho kwenye safu ya kiungo.

Mchezaji huyu mwenye umri wa miaka 26 amekuwa na kiwango cha kuvutia zaidi kwa wekundu hao na uwezo wake sasa umemfanya kuanza katika mechi 11 chini ya kocha Jurgen Klopp msimu huu.

Alikuwa mmoja wa wachezaji muhimu wakati Liverpool ikitwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita na kiwango hicho ameendelea nacho msimu huu. Sio jambo la kushangaza haraka amekuwa mmoja wa wachezaji wanaovutiwa zaidi na mashabiki wa klabu hiyo.

1. N'golo Kante (Chelsea)
Anayependa kutabasamu wakati mwingi, N'Golo Kante anachukuliwa na wengi ndio kama kiungo mkabaji bora zaidi duniani kwa sasa.

Mfaransa huyu amekuwa kwenye kiwango kizuri katika ukabaji, kugawa pasi za uhakika, na kutengeneza mashambulizi mbele.

Alikuwa nguzo muhimu zaidi kwa Leicester City wakati wakitwaa taji la Ligi Kuu England msimu wa 2015-16 na akashinda tena mwaka uliofuata akiwa na Chelsea, na kumfanya kuwa mshindi mara mbili mfululizo wa taji hilo.

Katika umri wake wa miaka 28 amekuwa nguzo muhimu kwa Chelsea katika kuwasukumizia mbele mipira washambuliaji wake na pia kufunga mabao kwa jina lake.

Alikuwa nje ya dimba mwanzoni mwa msimu huu, lakini amerudi akiwa imara na ameonyesha kwa uhakika kabisa kile alichokuwa wanakimisi Blues hao.

Yapo maoni yako kuhusu orodha hii? yupi kiungo wako bora aliyekosekana katika orodha hii na wewe unaamini anastahili kuwapo?

Credit: Nipashe
Casemiro da Silva na fabinho hawa ni brazilian player wenye uwezo mkubwa wa kukaba,world cup ya safari hii kama wasipopata majeruhi huenda brazili ikapata mafanikio makubwa na kutwaa taji
 
Back
Top Bottom