Hakuna Watanzania waatakaoweza kufanya jambo la kipumbavu na la kipuuzi kama hilo kutokana na sababu kuu nne.
Moja ni hulka na haiba ya Watanzania ambapo kwa kiasi kikubwa sisi ni watu ambao hatupendi sana mikwaruzano na ni watu wapenda amani. Kabla ya uhuru na hata baada ya uhuru hatukuwa ni watu wagomvi, washari ama wapenda vita. Ustaarabu ulitufikia mapema sana.
Mbili ni maendeleo ya elimu na utamdawazi, ambapo kwa kiasi kikubwa kadri siku zinavyoenda ndivyo watu huzidi kupanuka maarifa. Watu wasomi hawapingi mambo kwa kuingia msituni na kufanya uasi bali hutumia njia rafiki katika kujenga hoja za kuipinga serikali, lakini pia kumbuka ya kwamba nchi yetu ina tengeneza mfumo wa watu kuwa wenye kujikomba na kuabudu mamlaka (Uchawa) ili kupata angalau teuzi kidogo maisha yawanyookee.
La Tatu ni uwepo wa intelijensia kali katika kudhibiti mchakato huo, kama taifa tumeshashuhudia chokochoko za majaribu ya mapinduzi mara nyingi ndani ya nchi yetu. Tuliweza vyema kupambana na kadhia hiyo na kuyazima mapinduzi hayo ambayo yalitaka kutokea. Pia kumbuka wale majambazi waliokiwa wakijificha mapangoni kule Amboni na kadhia ya ujambazi kule Kibiti. Matukio yote yanaonyesha uimara wetu katika kudili na aina mbalimbali za matukio.
La Mwisho na hili ndio la msingi, nchi yetu haiuzwi lakini tunafanya mageuzi makubwa baada ya kufeli awali.
Iko hivi, wakati wa awamu ya kwanza, umiliki wa nyanja kuu za uchumi ulidhibitiwa na serikali (sera ya ujamaa na kujitegemea). Katika wakati huu Serikali iliweza kufanya biashara na kuongoza nchi. Sote tunafahamu ni kwa namna gani sera zile zilivyotufukarisha na kukosa huduma za msingi. Waliofuatia walianza utaratibu maalum wa kuanza mchakato wa kubinafsisha nyanja kuu za kiuchumi na zile za msingi zikibaki kwa serikali kwani ilishathibitika ya kuwa mfumo wa kijamaa kamwe hauwezi kufanya kazi nchini na ulishafeli, ukweli ni kwamba kadri siku zilivyokuwa zinasogea basi ndivyo maisha taratibu yanazidi kuimarika kuliko ilivyokuwa awali. Dunia ya sasa ni uwekezaji na kama ni hivyo tunatakiwa tufahamu ni jinsi gani nchi nyingi duniani zilizofungua fursa za uwekezaji leo ni matajiri. Inawezekana kuna makosa kadhaa yapo lakini yanatakiwa yarekebishwe ili yalete tija kwa maslahi mapana ya taifa.
Nchi hii haiuzwi bali inafanyiwa uwekezaji.