Blasio Kachuchu
JF-Expert Member
- Sep 7, 2016
- 721
- 438
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM – Vodacom M-Pesa Tanzania imetangaza ushirikiano mpya na PayPal utakaowezesha wateja kufanya miamala kwa urahisi kati ya akaunti zao za PayPal na pochi za M-Pesa kupitia M-Pesa Super App, hatua inayolenga kupanua upatikanaji wa huduma za kifedha za kidijitali kimataifa.
Kupitia mfumo huo mpya, wateja wa M-Pesa watakaokidhi vigezo wataweza kuweka fedha moja kwa moja kwenye akaunti zao za PayPal pamoja na kutoa fedha kutoka PayPal kwenda M-Pesa kwa njia salama, rahisi na ya haraka zaidi.
Huduma hiyo inalenga kurahisisha miamala ya kimataifa kwa wafanyakazi wa kujitegemea (freelancers), watengeneza maudhui, wajasiriamali wanaofanya shughuli katika uchumi wa kazi za muda (gig economy), pamoja na Watanzania wengine wanaotumia huduma za kidijitali.
Ushirikiano huo unakuja wakati mahitaji ya huduma za malipo ya kuvuka mipaka yanaendelea kuongezeka miongoni mwa Watanzania wanaojihusisha na biashara za kimataifa, kazi za kujitegemea pamoja na huduma mbalimbali za kidijitali.
Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa M-Pesa, Tulisindo Mlupilo, alisema ushirikiano huo unaonesha dhamira ya M-Pesa ya kuendelea kuwaunganisha wateja na fursa mbalimbali kupitia ubunifu na huduma jumuishi za kifedha.
“Uunganisho wa kidijitali unaendelea kufungua fursa nyingi zaidi kwa Watanzania kushiriki katika uchumi wa kimataifa kupitia biashara za mtandaoni, kazi za kujitegemea, utengenezaji wa maudhui pamoja na biashara za kuvuka mipaka. Kupitia ushirikiano huu na PayPal tunawarahisishia zaidi wateja wetu kutuma, kupokea na kutoa fedha kati ya mifumo hii kwa urahisi na uhakika zaidi,” alisema Mlupilo.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais Mwandamizi, Mkuu wa Kanda na Meneja Mkuu wa Mashariki ya Kati na Afrika wa PayPal, Otto Williams, alisema ushirikiano huo utaongeza muingiliano wa mifumo ya malipo kwa watumiaji wa huduma za kidijitali duniani.
“Duniani kote tunaendelea kushuhudia ukuaji wa biashara za kidijitali pamoja na ongezeko la ushiriki wa watu katika kazi za mtandaoni. Kwa kuwezesha uhamishaji rahisi wa fedha kati ya PayPal na M-Pesa kupitia kuunganisha akaunti, ushirikiano huu utasaidia kutoa huduma za malipo ya kuvuka mipaka zilizo rahisi, salama na zenye ufanisi zaidi kwa wateja nchini Tanzania,” alisema Williams.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wateja wataweza kutumia huduma hiyo moja kwa moja kupitia M-Pesa Super App kwa kuunganisha akaunti zao za PayPal na akaunti za M-Pesa kupitia mfumo wa usajili na uthibitishaji wa taarifa unaolenga kuhakikisha usalama wa miamala.
Hatua hiyo inaendelea kuimarisha nafasi ya M-Pesa kama kinara wa huduma za kifedha za kidijitali na ubunifu nchini Tanzania huku ikiunga mkono juhudi za kuongeza ujumuishaji wa kifedha na ushiriki wa Watanzania katika uchumi wa kidijitali.
Maelezo zaidi kuhusu namna ya kujiunga na huduma hiyo, viwango vya miamala, muda wa kuanza kwa huduma pamoja na mwongozo wa matumizi yatapatikana kupitia tovuti rasmi ya Vodacom Tanzania na njia nyingine rasmi za mawasiliano za M-Pesa.

