GE2025 Vyombo vya Habari Tanzania kuipa kisogo 'speech ya Askofu Gwajima; Ni kwa maslahi ya nani?

GE2025 Vyombo vya Habari Tanzania kuipa kisogo 'speech ya Askofu Gwajima; Ni kwa maslahi ya nani?

Matukio, Taarifa, Habari na Mijadala ya Wananchi WAKATI wa Mchakato wa Uchaguzi Mkuu 2025

Mwanamwana

Platinum Member
Joined
Aug 1, 2011
Posts
9,604
Reaction score
22,722
gwajimaaa.png

Zikiwa zimebaki siku mbili kabla ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, ghafla anaibuka mwanasiasa ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima na kutoa msisitizo wa baadhi ya mambo yanayoendelea kuelekea uchaguzi mkuu.

Katika hotuba yake, Gwajima amesisitiza msimamo wake wa kupinga vitendo vya utekaji na uonevu ambavyo anadai vinaendelea kushamiri nchini Tanzania.

Askofu Gwajima ameonesha wasiwasi wake kuhusu uwajibikaji wa mamlaka katika kukomesha vitendo hivyo, akibainisha kuwa vinaibua chuki ndani ya jamii na kukiuka haki za binadamu pamoja na kuchochea wananchi kukosa imani na viongozi na baadhi ya Taasisi muhimu.

Kauli hiyo ameitoa wakati kukiwa na maswali kuhusu usalama wake, baada ya kukaa kimya kwa siku kadhaa kinyume na ilivyozoeleka. Ukimya huo uliibua mijadala mitandaoni, huku baadhi ya watu wakijiuliza hali yake na sababu za kutotoa matamko kama kawaida.

Huenda hali hiyo isishangaze, lakini maswali yameibuka kuhusu sababu za vyombo vya habari kutochapisha au kurusha maudhui ya hotuba yake. Hata baadhi ya vyombo vya habari vya mtandaoni ambavyo kwa kawaida hurusha vipande vya hotuba zake, safari hii vimebaki kimya jambo linaloacha maswali kuhusu nini kinaendelea nyuma ya pazia.

Najaribu kujiuliza “kwanini?”, swali jingine linaweza kuibuka: Je, kama Gwajima angezungumza tu kuhusu amani bila kugusia masuala nyeti kama utekaji, vyombo vya habari vingeripoti, au anayoyasema hayana ukweli? Hili ni jambo la kutafakari.

Aliyekuwa Balozi wa Tanzania, Nchini Cuba na Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi, humphrey Polepole katika hotuba zake, aliwahi kudokeza kuwa vyombo vya habari vikubwa nchini vimepewa vitisho na TCRA kutozungumzia mambo ya msingi hasa wakati wa uchaguzi, huenda ndio sababu ya kuzipa kisogo taarifa nyingi.

Zaidi soma GE2025 - Polepole: Vyombo vikubwa vya Habari vimepewa vitisho na TCRA

Miongoni mwa maelezo ambayo TCRA imekuwa ikitoa kwa vyombo vya habari vilivyokuwa vikijaribu kurusha sehemu za hotuba hiyo, ni kwamba maudhui hayo hukosa mizania, Hoja hii iliyosababisha baadhi ya vipande vya hotuba hizo kuondolewa hewani.

Soma GE2025 - TCRA: Vyombo vya Habari vizingatie Miongozo na Kanuni za Uandishi wa Habari kuelekea Uchaguzi Mkuu

Katika mazingira kama hayo, baadhi ya vyombo vya habari vinaonekana kuichukulia hotuba ya Gwajima kama “picha ya Kihindi”, yaani jambo lisilo na uzito au linaloweza kuleta tafsiri tata. Hata hivyo, vyombo hivyo hivyo vimekuwa vikichapisha taarifa zenye maoni binafsi bila kuzuiliwa au kuhojiwa kuhusu usawa wa taarifa hizo. Mfano ni “Azimio la Wamiliki wa Vyombo vya Habari na Wahariri Waandamizi” ambalo limepata nafasi kubwa katika karibu kila chombo kikuu cha habari nchini.

Wakati huo huo ambapo giza limetanda kwenye vyombo vya habari kurusha baadhi ya taarifa, mitandao ya kijamii imeendelea kuwa mbadala wa upashanaji habari, hasa kwa matukio ambayo hayapati nafasi katika vyombo vya habari vya kawaida. Tumeshuhudia watumiaji wa mitandao kama Facebook, Instagram, TikTok na X wakitumia majukwaa yao kusambaza taarifa hizo.

Hata hivyo, jamii ipo kwenye hatari ya kukosa taarifa muhimu, hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya mitandao imekuwa ikifungiwa au kudhibitiwa na mamlaka nchini Tanzania.
 
Ni kwamba unataka waandike ili wadaiwe hela walizohongwa na ccm, au? Kumbuka njaa haina baunsa.
 
Back
Top Bottom