elivina shambuni
JF-Expert Member
- May 31, 2018
- 461
- 295
ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Mbinga, John Ndimbo amewaonya wabadhirifu wa fedha za miradi ya umma, kuacha uovu huo, kwani unaliangamiza taifa na kuumiza wananchi wa maeneo zilikoelekezwa kutumika.
Aidha, amemtaka kila mwananchi kutenda haki kwa upendo katika eneo lake, iwe kazini au nyumbani ili kuchochea amani na utulivu alivyodai haviwezi kuletwa na Rais au maaskofu peke yao.
Amekemea viongozi wanaotumia nafasi zao na kujifanya kama sawa na Mungu, huku wakiwanyanyasa watu kwa kuwanyima haki za msingi na kuwataka kuelewa kuwa wanatenda chukizo kwa Mungu hivyo wabadilike na kutenda haki.
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga, aliyasema hayo jana katika mahubiri aliyoyatoa katika Misa Takatifu ya Krismasi, iliyofanyika kitaifa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Kiliani mjini Mbinga mkoani Ruvuma. “Wakristo tuwe mstari wa mbele kutetea haki za wengine.
Tunapotazama na kusikiliza vyombo vya habari, tukiangalia harakati za mawaziri wanapoenda kutembelea miradi mbalimbali, unasikia waziri analalamika watendaji kukosa kutunza fedha za miradi, wanafanya ubadhirifu wa fedha za miradi, tukifanya hivyo tunatengeneza shimo la matatizo makubwa kule zilikokusudiwa. “Fedha za serikali zinapaswa kutumika vizuri.
Hawa wanaokemewa kufanya ubadhirifu na ambao si waadilifu ndio tunasali nao pamoja, ndio maana nasema sisi tunapaswa kuwa mfano lakini baadhi yetu ndio hao tunaharibu miradi ya serikali. Hakuna imani itatetea ubadhirifu au kukosa uadilifu kwa mali za umma,” alisema Askofu Ndimbo.
Alisema viongozi wanapaswa kuishi kwa mfano wa maisha ya Yesu Kristo, yalioongozwa kutumikia zaidi ya kutumikiwa. Alisisitiza kuwa viongozi wa leo, wanapaswa kuishi hayo kwa utenzi usemao; “Kuongoza kwa kutumikia na kutumikia kwa kuongoza” ili kuwavuta wengine kwenye utulivu, imani, matumaini na usalama.
Alisema kazi ya kiongozi ni kuona mahitaji ya anaowaongoza na kwa fadhila ya ubatizo, Wakristo wote ni viongozi wanaopaswa kuona mahitaji ya wengine na kuyatafutia ufumbuzi.
Aliwataka Wakristo kuwa wakala wa haki iliyoota mizizi moyoni kwa kuheshimu amri ya mapendo ambayo ni msingi wa amani na haki. “Anayempenda jirani atatenda haki na si kinyume chake.
Ili tuwe wakala wa amani yatupasa kuziishi heri, pale ambapo mmoja anajitutumua tutumua na kujidai yeye ni karibu na Mungu, tunaleta matatizo, mmoja kama kiongozi hakubali kushuka, tunasababisha makuu. Yesu akiwa kiongozi mkuu, anataka tujifunze kwake upole na kushuka,” alisema Askofu Ndimbo.
Aliwataka Wakristo kufanya kila linalowezekana, kutenda haki na kutambua kuwa lolote lililo kinyume cha utu wa binadamu ni baya, ikiwamo utoaji mimba, kwani ni ukatili wa haki ya kuishi aliyonayo Mungu mwenyewe kwa mwanadamu.
Aliwakumbusha kuwatunza wahitaji wasio na chakula na mavazi na kila mwenye dhamana, kuhakikisha kunaendelea kuwa na uhuru wa kuabudu, wa kujipatia kipato, wa kuchagua na kuchaguliwa na kila mtu anapata haki stahiki ya afya na elimu, kwani ikifumbiwa macho inaleta matatizo kwa kuwa jamii isio na elimu na afya ni tatizo.
Kuhusu amani Akisisitiza kuhusu amani, Askofu Ndimbo alisema inajengwa, kwa kila mmoja anapotambua ana wajibu wa kuindeleza, na si wajibu wa Rais peke yake, maaskofu au viongozi katika ngazi fulani, bali wajibu wa kila mmoja kuendeleza amani pale anapofanyakazi na anapoishi. “Ili kuzuia migogoro lazima amani iote mizizi kwa kila mmoja wetu kutoka moyoni mwake.
Katika jumuia nzima ya kimataifa itawezekana amani kwa kuheshimu sheria na upatanifu ulioasisiwa na Mungu mwenyewe. Amani lazima ichochewe na watu katika harakati za kujiendeleza ili kusonga mbele katika juhudi hizi za maendeleo ya kijamii na kiroho,” alisisitiza.
Alisema zawadi pekee kwa Mfalme wa Amani, Yesu Kristo ni kuheshimu malengo mazuri ya viongozi walionayo kwa jamii, mke na mume kuheshimu utu wa mwenzake na kumsaidia kutimiza ndoto zake njema huku wazazi na walezi wakiwasaidia watoto kufikia ndoto na matarajio yao.
Aliwasihi Wakristo wasiishie kuimba Tanzania ni kisiwa cha amani, bali waishi kwa mfano mwema na waiombee nchi na viongozi wote wenye nia njema ya ustawi wa jamii, wasaidiwe kutekeleza mipango hiyo kwa faida ya wote na kuwa wakala wa amani na upatanisho.
Akizungumzia kuzaliwa kwa Yesu Kristo, Askofu Ndimbo alisema ni sababu ya amani, usalama na utulivu, kwani ni tendo la safari ya ukombozi uliopatikana msalabani na ambao daima unasisitiza upatanishi, kusameheana, kuvumiliana na kuchukuliana katika jamii.
“Sasa ingetupasa tujihoji upi wajibu wa msingi wa watu wenye mapenzi mema wafurahie katika Kristo. Ni wajibu au kazi ya kutenda haki na si kujitendea haki wenyewe binafsi,” alisema. Aliongeza kuwa wakati wote mwanadamu anapomshirikisha Mungu katika utendaji wake, anakuwa na utulivu, matumaini, usalama, mambo yalio matunda ya kutenda haki.
Kabla misa haijaisha, akitoa Neno la Krismasi, Askofu Ndimbo aliwataka waumini wasirudi nyuma kwenye uovu kama tabia za nguruwe, ambaye hata aoshwe namna gani anarudi matopeni, bali waishi kipindi cha kimasiha (ukombozi) na maisha ya uadilifu na kutakiana amani wao kwa wao.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Pascal Mwanache alivishukuru vyombo vya habari kwa namna vinavyotangaza habari njema na jitihada za maendeleo na ustawi wa watu kiroho na kimwili na kuendeleza weledi huo.
Mjini Dodoma, Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT), Dk Dickson Chilongani pamoja na mambo mengine, amekemea tabia za baadhi ya wanasiasa kutafuta nafasi zao kwa kupitia kwa waganga wa jadi, jambo alilosema halifai na haliwezi kuwasaidia Watanzania kwa kuwa linawafanya wapate viongozi wasiotokana na Mungu.
“Mwakani tunafanya Uchaguzi Mkuu, sasa tabia ya wanasiasa kukimbilia kwa waganga nyakati za uchaguzi haifai badala yake wanatakiwa kwenda nyumba za ibada ili waombewe kama wanahitaji madaraka. Kiongozi mzuri ni yule anayetokana na Mungu na siyo anayetokana na nguvu za giza,” alisema Dk Chilongani.