Dk. Mwakyembe awaumbua wabunge wenzake
• Adai baadhi hawajui Kiingereza
na Sauli Giliard
MBUNGE wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe (CCM), amesema baadhi ya wabunge hawaijui lugha ya Kiingereza, hivyo kuwa kikwazo kwao kutoa mawazo wakati wa mijadala ya miswaada mbalimbali bungeni inayoandaliwa kwa lugha hiyo.
Mwakyembe ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alitoa kauli hiyo jana katika semina iliyolenga kuwawezesha wabunge kuzifahamu na kuzingatia kanuni wakati wa kufanya marekebisho ya miswada mbalimbali bungeni.
Akichangia katika semina hiyo ya siku mbili, iliyoendeshwa na Naibu Spika wa Bunge, Anne Makinda, na kuwashirikisha wenyeviti na makatibu wa kamati mbalimbali za Bunge, Dk. Mwakyembe alisema matumizi ya Kiingereza, yanawanyima fursa baadhi ya wabunge kuchangia miswada bungeni kwa kuwa wengi hawaifahamu lugha hiyo, jambo linalosababisha kupitishwa miswada ambayo baadaye utekelezaji wake huwa mgumu.
Mbunge huyo machachari ndani ya CCM, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza kashfa ya zabuni ya uingizaji wa mitambo ya kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond, alishauri Kiswahili kiwe mbadala wa lugha ya Kiingereza katika uandaaji wa miswada bungeni ili kutoa fursa ya kujadiliwa kwa kina na wabunge wote.
Dk. Mwakyembe alishangazwa na utaratibu wa kutumia lugha ya Kiingereza na kuhoji sababu za kutotumia lugha ya Kiswahili wakati wa kujadili na kupitisha miswada mbalimbali ya sheria.
Alisema kwa sasa sifa anazotakiwa kuwa nazo mtu anayetaka ubunge ni mbili tu, ambazo ni kujua kusoma na kuandika.
Akielezea athari nyingine ya kutumia lugha ya Kiingereza, alisema ni wanahabari kuwachanganya zaidi wananchi, wanapowasilisha kilichomo katika miswada iliyoko katika lugha hiyo.
Akizungumzia suala hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), Philip Marmo ambaye alifungua semina hiyo, alisema kuendelea kutumika kwa lugha ya Kiingereza bungeni, kunatokana na kasumba iliyopo katika nchi za Jumuiya ya Madola ambapo Tanzania ni miongoni mwao.
"Kinachofanyika kwa sasa ni kuandaliwa kwa mswada ambao utanguliwa na muhtasari kwa lugha ya Kiswahili, hasa katika mambo muhimu ili wabunge waweze kujadili wakiwa na uwelewa wa kutosha," alisema Marmo.
Naye Mama Makinda, aliwataka wabunge wakati wa kujadili miswada kuondoa mabishano yasiyo ya lazima, ili kutoa fursa ya kujadili miswada mingine.
Alisema ili wabunge waweze kuchangia vema, wanatakiwa kutengeneza mtandao wao na kufanya ushawishi ili hoja zao zikubalike katika jamii na kuacha kuendeleza majadiliano nje ya Bunge.
Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Mkanyageni, Habibu Mnyaa (CUF), alisema suala la kufanya ushawishi kwa namna moja, linaweza kutawaliwa na rushwa kwa wabunge kutumiwa na watu wenye maslahi binafsi.
"Nikiwa na pesa ninaweza kuwachukua wabunge na kuwapeleka sehemu, na baadaye bungeni wakaenda kujadili jambo lisilokuwa na manufaa. Tuiangalie hii ‘lobbying' (ushawishi) ni kwa kiasi gani," alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje na Usalama, Wilson Masilingi, alisema kabla ya mswada kupelekwa bungeni, kuna umuhimu wa kujadiliwa na umma ili kutoa maoni kwa lengo la kuuboresha na kuliwezesha Bunge kuujadili kwa kina.
Kwa mujibu wa Masilingi, kinachokwamisha kwa sasa ni fedha, lakini Idara ya Mawasiliano ya Bunge inatakiwa kutoa matangazo kupitia vyombo vya habari na tovuti ya Bunge ili wananchi wajue kinachoendelea na kutoa michango yao.
Awali, akifungua semina hiyo, Waziri Marmo alisema kuna umuhimu wa wabunge wote kufanyiwa semina kama hiyo, ili waweze kushiriki katika mijadala kwa nidhamu, huku wakifuata kanuni za Bunge.