Mahakama ya Wilaya ya Arumeru imewaachia huru watetezi wa haki za binadamu Jackson Martine Kabalo na Joseph Chaviruka Mrindoko, maarufu kama “Wachokonozi”, baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuendelea na ushahidi katika Shauri la Jinai Na. 000017735/2025.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), shauri hilo lilikuwa limepangwa kusikilizwa Mei 26, 27 na 28 pamoja na Juni 4 na 5, 2026. Hata hivyo, upande wa Jamhuri uliwasilisha shahidi mmoja pekee Mei 26 ambaye alikuwa shahidi wa saba wa upande wa mashtaka.
THRDC imeeleza kuwa katika siku zilizofuata, upande wa mashtaka haukuwasilisha shahidi yeyote wala kutoa maelezo ya kuridhisha kuhusu kutokuwepo kwa mashahidi hao.
Mahakama ilibainisha kuwa tayari ilikuwa imetoa maelekezo kutokana na shauri hilo kuchukua muda mrefu, huku ikisisitiza umuhimu wa haki kutendeka kwa wakati bila ucheleweshaji usio wa lazima.
Kutokana na hali hiyo, Mahakama iliamuru washitakiwa hao waachiwe huru kwa mujibu wa Kifungu cha 242(5) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20, Marejeo ya Mwaka 2023.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa kesi hiyo ilianzia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kama Shauri la Jinai Na. 15727/2025, ambapo Julai 27, 2025 upande wa Jamhuri uliomba kuiondoa kwa madai ya kutokuwa tayari kuendelea nayo, hatua iliyosababisha mahakama kuwaachia huru washitakiwa hao.
Hata hivyo, siku hiyo hiyo walikamatwa tena na kufikishwa Mahakama ya Wilaya ya Arumeru wakikabiliwa na mashtaka yale yale bila kutolewa maelezo ya msingi kuhusu hatua hiyo.
Mashtaka yaliyokuwa yanawakabili yalihusisha kutoa taarifa za uongo mtandaoni pamoja na kufanya shughuli za utoaji wa maudhui mtandaoni bila kuwa na leseni.
Katika kipindi chote cha usikilizwaji wa shauri hilo, Kabalo na Mrindoko walitetewa na mawakili Simon Mbwambo na Ally Mhyellah kutoka THRDC
Pia soma: Wachokonozi waachiwa huru, wakamatwa tena na kushtakiwa upya