Mzee wa Code
Member
- Sep 23, 2024
- 82
- 227
Tangu kufunguliwa kwa dirisha la uchukuaji wa fomu za kuwania ubunge na udiwani, wagombea wengi wameonekana kuepuka kabisa kuzungumza na vyombo vya habari au hata kutoa hoja za msingi mbele ya wananchi, licha ya mchakato huo kuwa ndio mwanzo wa safari ya kuwashawishi wapiga kura. Hali hii imetokana na maelekezo rasmi kutoka kwa baadhi ya makatibu wa CCM ngazi ya wilaya na mikoa — ambao pia ni wasimamizi wa uchaguzi ndani ya chama — wakitaka wagombea "wasiseme chochote" hadi pale watakapopitishwa rasmi na chama.
“Kwa sasa tumeambiwa tusiseme chochote kuhusu wabunge waliomaliza muda wao. Hata kama una hoja za msingi au unataka kueleza sababu zako za kuomba ridhaa ya wananchi, umeambiwa ukimya,” alisema mmoja wa watia nia aliyeomba kutotajwa jina lake.
Kwa mujibu wa maelezo ya baadhi ya wagombea hao, utaratibu huu wa kuwafunga midomo unaondoa kabisa nafasi ya wagombea kuwa na mjadala wa wazi na wa kistaarabu kuhusu mustakabali wa maendeleo katika maeneo yao. Badala yake, mfumo huu unaonekana kuwalazimisha kuwa sehemu ya mtiririko wa utii usiohoji, hali ambayo wachambuzi wa siasa wanasema inalenga kuzalisha viongozi wasio wakosoaji wa serikali, bali "machawa wa mfumo."
“Hili ni tishio kwa demokrasia ndani ya chama. Kama hatuwezi hata kutoa hoja za msingi kwa hofu ya kutoswa mapema, hiyo maana yake ni kwamba CCM haitaki viongozi wakosoaji. Wanataka watu wa kusema ‘ndiyo mzee’ muda wote,” alisema mtia nia mwingine.
Wakati CCM ikijinasibu kuwa kinazingatia misingi ya haki na usawa katika uteuzi wa wagombea, hali halisi inaashiria tofauti kubwa. Kukataza wagombea kuhoji utendaji wa waliowatangulia ni kinyume na kanuni za uchaguzi huru na wa haki unaotakiwa kutengeneza fursa kwa wananchi kuchagua viongozi bora kupitia hoja na mjadala.
Huwezi kuwa na uchaguzi wa haki kama mtu anazuiwa kuzungumzia mapungufu ya waliopita. Hiyo sio siasa bali ni ukiritimba wa fikra
Kwa sasa, wagombea wengi wanaendelea kuchukua fomu kwa ukimya mkali, wakizuiwa kuwa na kundi la wafuasi wao lakini bila kutoa kauli yoyote kwa vyombo vya habari wala kwa wananchi. Swali linalobaki ni: ikiwa mwanzo wa safari ya uongozi unaanza kwa ukimya na woga, je, sauti ya wananchi itaweza kusikika kupitia kwao kesho?