Sasa tunaongea, hii imetulia. Kusema ukweli wagombea wengi wanaanza kuingia kwenye trap ya CCM. Simply CCM wanachofanya ni kusoma mipango mbalimbali ya serikali na kuahidi kuwa watafanya hiki na kile kutokana na yale yaliyopo kwenye mipango ya serikali pamoja na bajeti.
Kwa kiwango kikubwa hii inatokana na uelewa mdogo wa wananchi wanaoshindwa kuwauliza maswali magumu. Ofcourse sasa hivi vyombo vingi vya habari ni vuvuzelas za vyama vya siasa na hatuoni hasa sera na mwelekeo. Wanasiasa na wagombea wananadi zaidi ahadi na mipango ya serikali.
Tunachotaka kusikia wengine ni mbinu za kibunifu za kuiondoa nchi katika matatizo. Kwa mfano mtu anapozungumzia kupunguza ukubwa wa serikali na kupunguza matumizi makubwa ya kodi yanayoelekezwa kwenye uendeshaji wa serikali, hii ni mbinu ni mkakati. Labda tu aende zaidi kwa kutoa takwimu, serikali sasa hivi inatumia kiasi gani; ikija serikali ndogo ya ukubwa X itaokoa kiasi Y cha fedha. Fedha hii itaingizwa katika miradi ya maendeleo kama ukuzaji wa bandari ya Dar es Salaam n.k.
Vile vile tungependa tusikie takwimu halisi; Ni kiasi gani cha fedha leo hii kinatumia kulipa posho za vikao (sitting allowances), Posho za safari za viongozi ndani na nje ya nchi, tunapoteza kiasi gani kwa viongozi kutumia zaidi ya asilimia 50% ya muda wao wa kazi nje ya vituo vya kazi (wakibangaiza viposho), Tunapoteza kiasi gani cha fedha kwa biashara zinavyofanyika kiholela mitaani bila kufuata kanuni na sheria zilizopo. Je tukileta ufanisi kwenye maeneo hayo tunatarajia kuokoa kiasi gani, na tutazielekeza kwenye maeneo gani.
Uchumi wetu uko hoi bin taaban kwa sababu mbali mbali, ni zipi hizo? Wagombea waseme sababu hizo watapambana nazo kivipi. Kwa mfano, miundo mbinu chakavu kama reli, bandari, bara bara, usafiri wa anga nchi kavu na majini, upatikanaji wa umeme wa uhakika, maji, n.k. Mgombea makini inatakiwa aje na Takwimu; kwa mfano sasa hivi bandari zetu zote zinashughulikia shehena za mizigo kiasi gani? Kwa nini shehena inayopitia kwenye bandari zetu ni sehemu ndogo tu ya mizigo inayopitia bandari ya Mombasa. Kutakuwa na mbinu gani ya kuziongezea bandari zetu competitive advantage na kuzifanya zitumiwe zaidi na waagizaji wa mizigo kutoka nchi jirani na kuongeza mapato ya bandari zetu (kwa kiasi gani), n.k.
Ubunifu katika ukusanyaji wa kodi kwa kupanua wigo wa kodi; Maeneo ambayo leo hii hayaguswi na wigo wa kodi kama kodi za nyumba (na za kupangisha), kodi nyingi za biashara ambazo hazisimamiwi vizuri na kuboresha usimamizi wa ukusanyaji wa kodi. Mapato ya serikali yanatarajiwa kuongezeka kwa kiwango gani na yakishaongezeka yataelekezwa wapi?
Kwenye kilimo kwa mfano ni mbinu zipi zitatumika kuhakikisha uzalishaji unaongezeka kwa viwango vinavyopimika. Mfumo wa masoko ya mazao ya wakulima ndo eneo lenye matatizo makubwa. Ikiwa ruzuku kwa mfano zitatolewa kwenye mbolea, ni mbinu gani itatumika kuhakikisha wakulima wanapata bei zinazolingana na gharama wanazotumia kuzalisha. Kwa nini Wagombea wasizungumzie jinsi ya kuwaunganisha wakulima moja kwa moja na wanunuzi ili kitakachozalishwa kiwe kinauzwa kwa faida. Wagombea wawe wanaongea kwa kutumia takwimu badala ya kuongea kama kasuku; kusema kweli kauli zingine za kusema simply tutafanya hili na lile bila kueeleza kwa undani zaidi zinatia wasi wasi hasa kama wanaosema hivyo wanaelewa wanavyoahidi... ndo mambo ya kuahidi viwanja vya ndege maeneo ambayo wanaotumia usafiri wa ndege ni viongozi tu.
Kampeni zimezama kwenye mipango na mikakati ya muda mfupi ya serikali. Hatusikii viongozi wakitueleza mikakati hasa inayopimika ni jinsi gani wataielekeza nchi hii kwenye ubepari wenye sura ya kibinadamu. Jinsi watakavyohakikisha mfumo wa masoko unadhibitiwa kuwalinda walaji na wauzaji vile vile, n.k.
Labda wito huu wa Mzee Mtei utasaidia. Ahadi tu hazioneshi jinsi tulivyo makini. Mikakati iko mingi na kuna taasisi zinazoendesha nchi kama TRA, benki kuu, Mabenki ya biashara, Makampuni ya simu, n.k. Wagombea inatakiwa watuoneshe mbinu mbadala wa kurekebisha taasisi hizo na sekta mbali mbali zilizopo ili zendeshwe kwa ufanisi zaidi na kuchochea ukuaji wa uchumi na biashara.
Kwenye matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano kama chombo cha kutawala na kutoa huduma bora, kama chombo cha kuleta ufanisi ndani ya serikali, kama chombo cha kutoa ajira na kukuza biashara, n.k. Ni maeneo gani hasa ambayo wagombea wanadhani hatujafanya ya kutosha kuweza kuvuna nguvu iliyopo kwenye matumizi makubwa ya teknolojia ya habari na mawasiliano. Kwa mfano kwenye maeneo ya ukusanyaji wa kodi kwa mfano Dar es Salaam nzima ni ofisi moja tu inayotoa huduma za ukusanyaji wa kodi za leseni za magari, usajili na kadhalika. Je matumizi ya teknolojia ya habari hayawezi kutusaidia kutawanya huduma hii maeneo mengi na kwa gharama nafuu na kuongeza ufanisi na ukusanyaji wa kodi za magari? Ni watu wangapi wenye magari wanaolazimika kuwalipa vijana uchwara waliojazana pale samora ili kuwasaidia kutokana na misongamano ya walipa kodi ndani ya eneo moja! Ni walipa kodi wangapi wanaochelewa kulipa ushuru na tozo mbali mbali (au kutolipa kabisa) kutokana na mfumo huu mbovu usiotumia mbinu za kisasa zilizopo?
Wagombea wetu watuambie watatumia mbinu gani mbadala kuongeza ufanisi (kwa viwango vinavyopimika) wa makusanyo ya mapato ya serikali; je inatakiwa VAT ishuke au iongezeke. PAYE je? ....n.k....n.k.
Hizi kampeni za kusema nitaleta maji, nitaleta meli, nitaleta bajaj, n.k. naona kama zinaakisi upungufu mkubwa uliopo kwenye timu za kampeni. Inaonekana hakuna watalaamu, kumejaa wabangaizaji na waganga njaa tu. Bahati mbaya hao ndo watakaohamia serikalini vyama vyao vitakaposhinda.