Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Shamsi Vuai Nahodha amekana kubebwa katika nafasi ya uwaziri kiongozi kama ilivyodaiwa hivi karibuni na vyombo vya habari.
Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya baraza la wawakilishi Maisara Mjini Unguja kufuatia kauli zilizotolewa na Balozi wa Tanzania Nchini Italia, Ali Abeid Karume katika mahojiano maalaumu na gazeti mmoja linalochapishwa wiki mara moja nchini kuhusu nafasi ya urais wa zanzibar.
Juzi gazeti moja litolewalo kila wiki liliripoti kwamba Balozi wa Tanzania Nchini Italia Ali Abeid Karume alisema kwamba wadhifa wa aliopewa waziri kiongozi ni wa kubebwa tu.
Kama mtu anasema mimi nimeokotezwa na kubebwa sasa ajiulize yeye amefika hapo kwa uwezo wa nani
.hata yeye alibebwa na na kufanyiwa hivyo na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa ambaye alimchagua kuwa balozi katika kipindi cha miaka kumi ya urais wake na sasa ni Rais Jakaya Kikwete ambaye amemchaguwa kubwa balozi wa Tanzania nchini Italia au amesahau hilo alihoji Nahodha ambaye anaonesha hakufurahishwa na kauli ya Balozi Karume.
Waziri Kiongozi alisema hana sababu ya kujitangaza na kupita kila sehemu kwa sababu anafahamika na uwezo anao ambapo katika kipindi chote hicho amefanikiwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu ikiwemo kuitaangaza ilani ya chama cha mapinduzi.
Nahodha alisema ni kweli wapo baadhi ya watu wanaohitaji kujitangaza na kupita kila sehemu kwa ajili ya kuomba nafasi ya kuomba Rais wa Zanzibar kutokana na kutokuwa maarufu au hawafahamiki vyema kwa wananchi.
Alisema yeye binafasi hana sababu ya kufanya hivyo kwa kuwa tayari ni maarufu na ameshakuwa katika nafasi nyingi alizozikamata mbali ya kuwa waziri kiongozi kwa muda wa miaka tisa sasa.
Uwezo ninao
sina sababu ya kujitangaza katika kuwania nafasi hiyo ya urais wakati ukifika nitafanya hivyo kwa kufuata utaratibu unaokubalika katika chama chetu lakini hivyo ni nani asiyenijuwa mimi Micheweni kote Pemba pamoja na Unguja yake mbona najulikana sana alisema Nahodha na kuwashangaa wanaomsema.
Nahodha alisema kumekuwa na watu wengi ambao wanatajwa kutaka kuwania urais wa Zanzibar mwaka 2010 akiwemo yeye lakini amesema bado ni mapema kusema azma yake hiyo na wananchi kama kweli wana hamu ya kumsikia iwapo yeye anataka kuwania wadhifa huo basi wasiburi wakati ufike kwani hivi sasa wakati haujafika.
Hata hivyo Nahodha hakutaka kuwaeleza waandishi wa habari nia yake ya kutaka kugombea urais wa Zanzibar wakati ukiwadia lakini alitumia utaratibu wake wa kila siku wa kuuliza swali yule aliyemuuliza.
Kama wewe umeongoza nafasi ya waziri kiongozi kwa muda wa miaka tisa utafanyaje? katika uamuzi wako hebu nambieni hiloaliuliza waandishi wa habari swali hilo .
Waziri Kiongozi ni miongoni mwa watu wanaotajwa kutaka kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar 2010 ingawa mara nyingi anapoulizwa husema kwamba anapojitizama aktika kioo huwa anajiona ni mdogo na hapaswi kuwa kiongozi wa ngazi ya juu katika nchi kutokana na muono wake wanavyojiona mwenyewe.
Lakini kauli yake hiyo ambayo aliwahi kuitoa mara kadhaa kwa waandishi wa habari katika kipindi chake cha kwanza cha kuwa waziri kiongozi imeanza kubadilika kila siku zinavyokwenda na ambapo sasa huwa anazungumza lugha nyengine kabisa na hiyo.
Nahodha aliwahi kunukuliwa akisema iwapo watu watamuona anafaa basi sawa lakini yeye binafsi anajiona hana uwezo huo kwa kuwa kioo kinamwambia hivyo lakini sasa inaonekana dhahiri ana nia na dhamira ya kuwania nafasi hiyo ya uongozi katika kipindi kijacho ambacho Rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume anamaliza muda wake kwa mujibu wa katiba.
Watu wengine ambao huwa wanatajwa kuwania kinyanganyiro hicho na kupewa nafasi kubwa ya ushindi kwa kuwa ndio chaguo la wana CCM Zanzibar ni Waziri Kiongozi Mstaafu Dk. Mohamed Gharib Bilali ambaye katika uchaguzi uliopita alipata kura nyingi za wajumbe wa halmshauri kuu ya CCM Zanzibar lakini kwa mujibu wa utaratibu wa CCM alitakiwa kujitoa katika kinyanganyiro hicho kwa kuwa utaratibu ni kumuachia Rais aliyepo madarakani kumaliza ngwe yake ya mwisho ya uongozi.
Balozi Ali Karume anatajwa kuwepo katika orodha hiyo ambaye tayari ametangaza azma yake hiyo ya kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar kufuatilia kumalizika kwa kipindi cha miaka kumi kaka yake Rais Amani Abeid Karume ifikapo mwakani 2010 .
Balozi Karume ni miongoni mwa mabalozi ambao wanashikilia nafasi za ubalozi kwa muda mrefu sasa tangu kipindi cha Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi akiwa balozi nchini Ubelgiji ambapo yeye ndio kiongozi wa mabalozi wote nchini.
Orodha ya wanaotaka kuwania nafasi ya urais Zanzibar ni kubwa ambapo wapo baadhi ya mawaziri waandamizi wa serikali ya mapinduzi Zanzibar na ya jamhuri ya muungano wa Tanzania akiwemo Makamu wa Rais Dk. Ali mohammed Shein, Waziri wa Afrika Mashariki, Mohammed Aboud, Waziri wa Muungano Mohammed Seif Khatib, na Balozi Seif Idd na wengine wengi.
Wengine kwa upande wa Zanzibar ni Naibu Waziri Kiongozi Ali Juma Shamhuna, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Hamid Mahmoud, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Haroun Ali Suleiman
SOURCE: ZANZIBAR YETU BLOG.