SoC03 Wajibu wa kila mwenye kipato kulipa kodi

SoC03 Wajibu wa kila mwenye kipato kulipa kodi

Stories of Change - 2023 Competition

tpaul

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2008
Posts
24,225
Reaction score
22,632
Bunge limetunga sheria mbalimbali za kodi ili kwamba kila mtu mwenye kipato halali aweze kulipa kodi, hivyo kuchangia mapato ya serikali. Lakini jambo moja la kusikitisha sana ni kwamba wanasiasa, ambao ndio wanaotunga sheria hizi, wameamua kujisamehe kulipa kodi kwa manufaa ambayo wanayajua wenyewe. Hakuna mtanzania hata mmoja anayefahamu umuhimu au faida ya wanasiasa kutolipa kodi huku wakijilipa mishahara minono kuliko wataalamu wengi wenye manufaa endelevu kwa taifa.

Keki ya taifa huchangiwa zaidi na watu masikini lakini wanasiasa ndio hunufaika zaidi na keki hii. Zaidi ya 50% ya mapato ya serikali hutumika kulipa mishahara, posho, marupurupu na takrima kwa wanasiasa. Wanasiasa wanapaswa kuona aibu kwa kuifaidi zaidi keki ya taifa inayotokana na kodi za wananchi huku walalahoi wakifa kwa njaa na magonjwa yanayoweza kutibika kwa kukosa dawa.

Pia wanafunzi wa nchi hii wanakaa chini kwa kukosa madawati na kusomea chini ya miti ilhali fedha ambazo zingetumika kununua madawati na kujenga madarasa zinatumika kulipa mishahara na posho za wanasiasa wasiolipa kodi. Hii haikubaliki hata kidogo. Nao wana wajibu wa kulipa kodi kwa kuwa wanapata vipato halali kama watanzania wengine.


1685562918105.jpeg

Wanafunzi wakisomea chini ya mti (Chanzo: mtandao)

Sheria ya kodi inatamka wazi kwamba kila mtu mwenye kipato halali lazima alipe kodi. Sasa iweje wanasiasa wanaojilipa mamilioni ya fedha wao wajitoe kwenye ulipaji kodi? Watu hawa hujilipa mishahara mikubwa kupindukia lakini hawataki kulipa kodi eti kwa kuwa wao ndio wanaotunga sheria, hivyo wanaweza kujipendelea kadri watakavyo. Hili ni sula la kibaguzi na linakiuka na kuvunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 13 kifungu cha kwanza (1) kinachosema:

“Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.”

Sasa ikiwa watu wote ni sawa mbele ya sheria, iweje wanasiasa wajitungie sheria inayokandamiza hiyo haki? Au tuseme kwamba wao sio watu bali ni misukule? Lakini hata misukule nao si ni watu pia? Tatizo ni kwamba raia wa chi hii tumezidi upole na tunakubali kuburuzwa na wanasiasa hata katika mambo ambayo yako wazi. Ni kwanini tusiingie barabarani kulaani na kupinga hii sheria kandamizi? Nakumbuka Mh Pinda aliwahi kuvunja sheria kwa kuwaamuru polisi wapige watu tu kupitia kauli yake ya “wapigwe tu” aliyoitoa bungeni na mpaka sasa hajawahi kukanusha wala kujutia matamshi yake haya, licha ya kuwa ameishastaafu siasa. Naomba Rais Samia aamuru sheria zote zenye ubaguzi, ikiwemo hii ya kodi, zifutiliwe mbali ili wanasiasa nao watusaidie kubeba mzigo wa kodi.

Serikali iliamua kuvunja katiba kwa makusudi kwa lengo la kuwalinda wanasiasa walafi wasiotaka kuchangia hata senti moja katika pato la taifa. Hilii suala halikubaliki hata kidogo. Natoa wito kwa watetezi wa haki za binadamu kuingilia kati uonevu huu na ikibidi kuiburuza serikali mahakamani ili kutoa fundisho kwa wabunge wa JMT walioamua kuisigina katiba waliyoapa kuilinda na kuitetea. Ubaguzi wa namna yoyote ile haukubaliki.

Utunzi wa sheria inayobagua nani alipe kodi na nani asilipe ni sawa na kukwepa wajibu halali wa kulitumikia taifa lako kwa kulipa kodi. Ni zaidi ya uhujumu uchumi. Ipo haja ya kuangalia upya suala hili kwani linakinzana na misngi ya utawala bora na haki za binadamu.

Jambo lingine la kushangaza ni kwamba urali wa kodi miongoni mwa walipa kodi hauko sawa. Kwa mfano, wafanyakazi hulipishwa kodi kubwa zaidi kuliko mtu yeyote katika nchi hii huku wafanyabiashara na wawekezaji wakitozwa kodi kidogo sana ukilinganisha na kipato chao au wakati mwingine wakisamehewa kodi kabisa. Hakuna mfanyakazi yeyote katika nchi hii anayesamehewa kodi. Aidha sio rahisi kwa mfanyakazi kukwepa kodi kama ilivyo kwa wafanyabiashara na wawekezaji. Hali hii huwafanya wafanyakazi kuonekana kama kundi linalokandamizwa sana katika suala zima la ulipaji kodi. Kipindi fulani serikali ilipunguzia kodi ya PAYE kwa wafanyakazi lakini kwa mshangao mkubwa kodi ikapunguzwa kwa 1% tu licha ya ahahadi kwamba kodi ingelipunguzwa kwa kiwango cha kutosha ili kuwapunguzia ukali wa maisha wafanyakazi.

Ili kuleta usawa wa kimaisha katika nchi hii, kila mtu mwenye kipato halali lazima alipe kodi kulingana na kipato chake. Kitendo cha wanasiasa kuendelea kujitenga na suala la ulipaji kodi, hakikubaliki hata kidogo. Huu ni ukiukwaji mkubwa wa haki na usawa wa binadamu na ni usiginaji wa katiba usiovumilika. Katiba ya nchi inasisitiza sana kuhusu usawa wa binadamu katika mambo muhimu ya kitaifa kama haya. Mtu yeyote hawezi kujiona mjanja kwa kujitoa kwenye ulipaji kodi huku akiwaachia walalahoi peke yao ndio wahangaike kulipa kodi. Kufanya hivyo ni sawa na kukubali kuwa fisadi, mnyonyaji na mchumia tumbo.

Nawasilisha.
 

Attachments

  • 1685562853854.jpeg
    1685562853854.jpeg
    116.8 KB · Views: 3
Upvote 2
Back
Top Bottom