Wakatoliki na mafundisho: Simulizi mbalimbali za maisha ya watakatifu

Wakatoliki na mafundisho: Simulizi mbalimbali za maisha ya watakatifu

The Dictator

JF-Expert Member
Joined
Jul 20, 2018
Posts
4,475
Reaction score
12,281
Mtakatifu MARIA GORETTI
images (3).jpeg


Maria Goretti alizaliwa tarehe 16 Oktoba 1890 katika kijiji kidogo huko Corinaldo, Italia. Familia yake ilikuwa maskini sana, lakini ilijulikana kwa imani na mshikamano wa kifamilia. Maria alikuwa mtoto wa pili kati ya watoto sita.

Baba yake, Luigi, alifariki akiwa mdogo, na familia ikalazimika kuhamia mji mwingine kutafuta kazi. Walipanga katika nyumba ndogo ya kukodisha pamoja na familia nyingine; familia ya Serenelli.

Na hapa ndipo historia yake ilipoanza kubadilika.

"Marietta" alikuwa binti mwenye upendo, alikuwa msichana mpole, mnyenyekevu, na mcha Mungu. Ingawa hakufanikiwa kwenda shule kwa sababu ya kazi nyingi za nyumbani; alijua kusali, na kila siku alisali rozari.

Hakuwa na nguo nyingi wala viatu vizuri, lakini moyo wake ulikuwa na upendo na heshima kwa kila mtu. Wengi walimpenda kwa tabasamu lake na heshima yake.
Miongoni mwa familia ya Serenelli; kulikuwa na kijana aitwaye Alessandro Serenelli, mwenye umri wa miaka 20. Siku zilikwenda na kijana alianza kumtamani Maria, alimtamani kingono. Siku moja alimwendea, na mara kadhaa alimwendea tena na tena akijaribu kumbembeleza afanye naye zinaa, lakini Maria alikataa kila mara, akisema:
“Hapana, Alessandro! Hii ni dhambi, na Mungu hataki!”
Ingawa jambo hilo lilimkosesha raha Maria ila hakumwambia mtu, kwa kuwa alikuwa anaogopa kuleta ugomvi kati ya familia hizo mbili.

Tarehe 5 Julai 1902, mama yake Maria alikuwa shambani na watoto wengine, akimuacha Maria nyumbani akishona nguo. Alessandro aliona huo ni wakati mujarab hivyo alimfuata tena nyumbani na kumkuta peke yake. Alijaribu kumshika na kumvuta, akajaribu kumlazimisha kumfanyia kitendo. Maria alipiga kelele na kupinga kelele kwa nguvu.

Alipoona hatokubali, Alessandro alijawa na hasira alichukua kisu cha jikoni na kumchoma mara kadhaa (takriban mara 14). Maria alianguka chini, akilia kwa uchungu.

Alessandro, akiwa na hasira na aibu, alitoroka na kutokomea. Maria alipelekwa hospitali haraka.

Hospitalini, madaktari walijaribu kumwokoa, lakini majeraha yalikuwa mabaya sana. Wakati wa mateso yake, Maria alisema wazi kwa wazazi wake kwamba amemsamehe Alessandro.

Siku iliyofuata, 6 Julai 1902, Maria alifariki akiwa na umri wa miaka 11 tu.

Alessandro alikamatwa na kufungwa miaka 30. Mwanzo alikataa kujutia kosa lake, lakini miaka mingi baadaye, akiwa gerezani, alianza kuota ndoto ambapo Maria alimtokea akimletea maua meupe kama ishara ya usafi na msamaha. Ndipo moyo wake ulipobadilika.

Alipotoka gerezani, jambo la kwanza alilofanya ni kwenda kumwomba msamaha mama wa Maria, ambaye alimkumbatia na kusema; “Maria alikusamehe, na nami nakusamehe.”

Baadaye, Alessandro aliishi maisha ya imani na utulivu, alifanyia kazi bustani ya kanisa hadi kifo chake.

Mnamo mwaka 1950, Papa Pius XII alimtangaza Maria Goretti kuwa Mtakatifu mbele ya hadhira kubwa, ikiwemo mama yake mwenye umri wa miaka 82.
Maria alitangazwa kuwa mlezi wa vijana, wasichana, na usafi.
 
MTAKATIFU INYASI WA LOYOLA.
images (5).jpeg


Inyasi alizaliwa mwaka 1491 huko Loyola (Hispania ya Kaskazini). Wazazi wake walikuwa matajiri wakajaliwa kupata watoto kumi na mmoja, watatu wakiwa wa kike na wanane wa kiume, Inyasi ndiye aliyekuwa kitindamimba.

Katika ujana wake aliingia kazi ya uaskari akapigana kwa uhodari na maadui wa nchi yake.Walipokuwa karibu kuuteka mji wa Pampeluna alipigwa risasi mguuni. Akapaswa kulala kitandani kwa masiku ili mguu wake upate kupona. Aliudhika sana kwa maana hakukuwa na kitu chochote cha kufanya hapo kitandani kutwa kucha. Mwishowe aliomba kitabu cha kusoma akapewa vitabu vya Maisha ya Yesu na Maisha ya Watakatifu.

Baada ya muda alipata kutambua kwamba ujasiri wa kweli unapatikana katika kuufuata mfano wa Watakatifu kuliko katika ushujaa wa kijeshi. Nia ya Inyasi sasa ilikuwa kumtumikia Yesu Mfalme. Alianza kufikiri juu ya maisha yake ya kiroho. Mambo hayo yalichukua muda wala hayakuendelea bila matatizo.

Siku moja bikira Maria alimtokea na mara mashaka yake yalikwisha. Alijitolea mwili na roho kwa Yesu akiapa kumtumikia mpaka kufa kwake atakuwa askari wa Kristu, na kufuata matendo ya ujasiri wa Watakatifu.

Inyasi alipopona alienda katika Kanisa la Monte Serat akaungama dhambi ya kiaskari na zote alizotenda tangu kupata akili. Alivua mavazi akautundika upanga wake kwenye altare ya bikira Maria. Alijificha muda wa mwaka mzima pangoni mwa Manresa akisali na kufunga kutwa.

Hapo ndipo alipoandika kwa uongozi wa bikira Maria; kitabu kile bora kiitwacho 'Mazoezi ya Kiroho'.

Watu wengi wamepata kuongoka na kupata Utakatifu kwa kufuata mashauri yaliyoandikwa humo. Kisha kumaliza mafungo ya mwaka mzima huko Manresa, alienda kuhiji Yerusalemu.

Aliporudi alijifunza muda wa miaka sita akianza na sarufi ya kilatini kwenye shule ya wavulana katika Chuo kikuu cha Paris (Ufaransa). Baadaye alisoma teolojia na alipokuwa na umri wa miaka arobaini na saba, alipata upadre huko Roma (Italia), akamaliza mwaka mzima akijitayarisha kwa Misa yake kwanza.

Huko Paris alikutana na Mtakatifu Fransisko Ksaveri na vijana wengine. Akiwa na hao vijana Inyasi alianzisha shirika la Wajesuiti au "Chama cha Yesu" Wajesuiti hao waliweka nadhiri ya kwenda popote watakapotumwa na Baba Mtakatifu wa Roma.
Walifaa sana kwa kusitawisha dini Katoliki katika nchi zote. Hata siku hizi bado wanashindana na maadui wa Kanisa Katoliki kila mahali duniani. Ndiyo maana watu wabaya wanawachukia, hata pengine wanajaribu kuwafukuza.

Mtakatifu Inyasi na Mapadre wa shirika lake huzoea kusema; "Tutende vitu vyote ili Mungu apate kusifiwa zaidi na zaidi".

Inyasi wa Loyola alifia huko Roma mwaka 1556. Pamoja na Fransisko Ksaveri aliandikwa katika orodha ya Watakatifu mwaka 1622.
 
Mtakatifu PONTIAN (PAPA PONTIANUS)
images (6).jpeg


Pontian alizaliwa Roma, huenda mwishoni mwa karne ya 2 BK. Alikuwa mzima sana, mwenye elimu na imani thabiti, akihusiana na viongozi wakuu wa Kanisa la wakati huo.

Mnamo tarehe 21 Julai 230 BK, Pontian alichaguliwa kuwa Papa wa 18 wa Kanisa Katoliki. Kipindi hiki kilikuwa na utulivu kidogo kuliko awali, na Kanisa lilikuwa linapanuka kwa idadi ya waamini.

Pontian aliongoza kwa busara, akishirikiana na maaskofu na mapadri katika kuimarisha mafundisho ya imani. Alisaidia sana katika kupanga liturujia na kuendeleza desturi za ibada ya Kanisa.

Hata ndani ya Kanisa, kulikuwa na migawanyiko ya kifalsafa na kiteolojia. Papa Pontian alijikuta akikabiliana na mgawanyiko na upinzani kati yake na kundi lililoongozwa na Hippolytus, padri na mwandishi mashuhuri, ambaye hakuafikiana na baadhi ya maamuzi ya mapapa waliomtangulia na Pontian mwenyewe.

Mwaka 235 BK, Mfalme Maximinus Thrax alipanda madarakani na kuanzisha wimbi jipya la mateso dhidi ya Wakristo. Papa Pontian alikamatwa pamoja na viongozi wengine wa Kanisa, akiwemo Hippolytus (ambaye wakati huo alikuwa ametengwa na Kanisa).

Wote wawili walihukumiwa na kufukuzwa Sardinia, kisiwa kilichotumiwa kama eneo la mateso na kazi ngumu kwa wafungwa.
Kwenye mazingira ya kikatili ya Sardinia; wafungwa walilazimishwa kufanya kazi ngumu migodini. Chakula kilikuwa haba, na magonjwa yalienea haraka.

Katika mateso haya, Pontian na Hippolytus walipata nafasi ya kuzungumza na hatimaye kupatana. Pontian, aliona hatakuwa na uwezo wa kuendelea kuongoza Kanisa akiwa kifungoni, aliandika barua ya kujiuzulu mnamo Septemba 235 BK hii ikawa mara ya kwanza kabisa katika historia ya Kanisa Katoliki ambapo Papa alijiuzulu rasmi.

Baada ya muda mfupi, alikufa kutokana na mateso, njaa, na magonjwa, mwishoni mwa mwaka 235 au mapema 236 BK.

Mwili wake uliletwa Roma na kuzikwa kwenye Catacomb ya Callixtus, sehemu iliyokuwa ikihifadhi miili ya mapapa wengi wa mwanzo.
 
Back
Top Bottom