Masaa kadhaa yaliyopita baada ya Mdude kutoa taarifa za kufuatiliwa akiwa aa Wakili Mwabukusi Mkoani Arusha, kwa takribani lisaa sasa wote wawili hawapatikani kwenye simu zao na haijulikani walipo.
Tumefanya Mawasiliano na Watu waliokuwa nao Mahakamani kucheki kituo vya Polisi Arusha kama wapo.
- Tunachokijua
- Agosti 28, 2023, Mdude Nyagali (Mdude Chadema) kupitia mtandao wa X (zamani Twitter) alitoa taarifa inayodai kuwa yeye pamoja na wakili Mwabukusi walikuwa wanafuatiliwa na mtu wasiyemfahamu, na kwamba alikuwa anawasiliana na watu wengine kuwapa taarifa zinazomhusu Mdude na mwenzie Mwabukusi.
"Huyu mtu pichani anatufuatilia tangu tupo mahakamani Arusha. Ikafika mahali anatufuata mpaka chooni mimi na mwabukusi. Tukaweka tahadhali ya kumfuatilia bila yeye kujua. Tulipoondoka mahakamani akawa anaongea na simu kuwajulisha wenzake kuwa tumeondoka akataja namba za gari yetu."
Kwa mujibu wake, alifika Jijini Arusha Agosti 27, 2023 ili kumjulia hali Wakili Madeleka anayeshikiliwa kwenye gereza la Kisongo, na kwamba angehudhuria mahakamani kusikiliza kesi inayomhusu wakili huyo Agosti 28, 2023.
Baadae, saa 7:53 mchana, Mdude alichapisha ujumbe mwingine unaodai kuwa walipata taarifa kuwa mtu anayewafuatilia ni mtumishi wa idara ya usalama wa Taifa. Mdude alisema;
"Taarifa za awali tumejulishwa kuwa mtu huyu ni mtumishi idara ya usalama wa taifa TISS, yuko under supervision ya RSO Manyara, na anaripoti kwa RSO wa Manyara. Jina lake anaitwa Matiko Kimenya. Tunaendelea kufuatilia na kuchukua tahadhali."
Madai ya kupotea kwa Mdude na Wakili Mwabukusi
Madai ya kupotea kwa Mdude akiwa na Wakili Mwabukusi yalianza kusambaa kwa kasi jioni ya Agosti 28, 2023 kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.
Miongoni mwa watu waliotoa taarifa za kupotea kwa wawili hawa ni Mtumiaji wa Mtandao wa X anayefahamika kwa jina la Baba Mwita.
Alidai uwepo wa taarifa kuwa Wakili Mwabukusi na Mdude wamepotea, hawajulikani walipo kwa zaidi ya masaa matatu sasa. Pia, aliomba mtu yeyote Mwenye taarifa kuhusu suala hili ampatie.
Mtumiaji mwingine wa mtandao wa X anayetumia jina la Ole Mtetezi aliandika;
“Baada ya Mdude kutoa taarifa za kufuatiliwa akiwa na wakili Mwabukusi mkoani arusha kwa takribani lisaa sasa wote wawili hawapatikani kwenye simu zao na haijulikani walipo
Tumefanya mawasiliano na watu waliokuwa nao mahakamani kucheki vituo vya polisi Arusha kama wapo.”
Ukweli wa Madai haya
Siku hiyo hiyo, saa 4:32 usiku kupitia Mtandao wa X, Mdude alitoa taarifa kuwa yupo salama, na kwamba anaendelea kuchukua tahadhari zote za kujilinda.
"Tuko salama mpaka muda huu. Tunaendelea kuchukua tahadhali. Mpaka saa 12 jioni hao vibaka walikuwa wanatumia land cruiser Prado STL wakitufuata kila eneo. Ila hawa vibaka tutamalizana nao wakiisogelea gari yetu tu tunaenda nao peponi. Safari hii tutaumia wote"
Pia, asubuhi ya Agosti 29, 2023, JamiiForums ilizungumza na Mdude na kupata uhakika wa taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu usalama wake.
Mdude aliiambia JF kuwa hakuwa amekamatwa kama watu wanavyosema na hakuna tishio lolote la kukamatwa.
Baada ya kupata ushahidi wa maelezo ya Mdude, JamiiForums imebaini kuwa maelezo yaliyokuwa yanasambazwa kwenye mitandao ya kijamii yakimhusu hayakuwa ya kweli.