Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 5,352
- 15,876
Olengurumwa ameeleza kuwa kama Urais una ukomo wa vipindi viwili pekee basi hata ubunge inawezekana kuwekewa ukomo wa vipindi vitatu pekee.
============================
Mratibu kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) wakili Onesmo Olengurumwa amesema unahitajika muafaka wa kitaifa wa maridhiano kuelekea Uchaguzi Mkuu, utakaokutanisha makundi mbalimbali ya kijamii hapa nchini ili kuwa na uchaguzi huru haki.
Hayo ameyasema leo Juni 18,2025 jijini Dar es salaam alipozungumza na wanahabari ofisini kwake.
Olengurumwa amesema kuwa kuna haja ya viongozi kufanyia kazi malalamiko yanayotolewa na wananchi kuelekea kwenye uchaguzi ili kujenga jamii yenye amani na utulivu, kwani bila kufanya hivyo madhara yake yanaweza kuonekana baada ya uchaguzi.
"Tunataka kuona viongozi wetu wanakuwa na utulivu, wanakuwa na amani wakati wa kuendesha nchi baada ya Uchaguzi, hakuna kitu kibaya kama kiongozi ukiwa kwenye taasisi fulani halafu manung'uniko yanakuwa ni mengi, kunakuwa na mivutano. Uongozi wako hautakuwa na utulivu, viongozi wetu wasiangalie tu kushinda uchaguzi, waangalie matokeo baada ya hayo ni yapi baada ya kushinda uchaguzi." Amesema Olengurumwa.
Olengurumwa amesema anaamini kuwa falsafa ya 4R iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaweza kuwa msaada mkubwa kwa Taifa kama itaendelea kuzingatiwa kwani inajenga hoja ya maridhiano.
Miezi michache iliyopita THRDC ilitoa mapendekezo kumi muhimu kuelekea uchaguzi Mkuu ili uchaguzi huo uwe wa amani bila kuwa na manung'uniko ya upande wowote ikiwemo marekebisho ya sheria na kanuni za uchaguzi, matumizi ya nguvu ya vyombo vya dola, uhuru wa wanahabari kuripoti mchakato wa uchaguzi na kutoenguliwa kwa wagombea wa upinzani bila sababu za msingi.