Magharibi mwa Kenya, mkulima wa mahindi Josephat Ouma alipitia kwenye safu za mabua ya kijani akiwa na simu yake janja mkononi. Alisita na kuinama kabla ya kupiga picha ya jani lililokuwa linaonekana kupatwa ugonjwa.
"Zamani nilikuwa nikisubiri mtu aje kusaidia. Tena baadhi ya wakati alikuwa haji kabisa. Lakini sasa, ninapiga picha tu, halafu APP inaniambia tatizo ni nini," aliiambia Xinhua katika mahojiano ya hivi karibuni.
Kama Ouma, maelfu ya wakulima wadogo nchini Kenya wanageukia teknolojia ili kudhibiti magonjwa ya mimea na kupambana na kupungua kwa mavuno.
Katika eneo ambalo huduma za ugani zimepungua kwa kuwa baadhi ya kaunti zina afisa mmoja tu kwa kila wakulima 1,500, zana za bei nafuu kama vile akili bandia (AI), app za simu na makundi ya WhatsApp vinaibuka kama njia muhimu za maisha.
Programu moja kama hiyo inaitwa PlantVillage Nuru, app ya bure iliyotengenezwa na watafiti wa Chuo Kikuu cha Penn State, ambayo hutumia AI kuchambua picha za mazao na kugundua magonjwa mara moja kama vile ugonjwa wa necrosis unaoua mahindi au ugonjwa wa mosaic unaoshambulia mihogo.
Inafanya kazi bila intaneti na kutumia lugha za wazawa, hivyo kuifanya kuwa muhimu sana katika maeneo ya vijijini. "App hii ni rahisi sana kutumia, hata kwa wakulima ambao hawajui kusoma na kuandika," alisema afisa wa ugani wa kilimo katika Kaunti ya Kakamega magharibi mwa Kenya, ambaye anafanya kazi kwa karibu na wakulima wadogo wanaotumia app hiyo.
Kote Kenya, makundi ya WhatsApp sasa yanafanya kazi kama mitandao midogo ya ugani.
Wakulima hupeana taarifa za wadudu, ushauri wa usimamizi wa mazao, na picha za mimea iliyoathirika, na kufanya watu wengine kutambua na kupata ufumbuzi kutokana na vyanzo vya watu. "Ni kama kliniki ya kila siku," alisema James Otieno, mkulima wa mahindi karibu na kaunti ya Kisumu, magharibi mwa Kenya. "Unaamka, unaingia kwenye kundi lako la WhatsApp kuangalia, na kuona kile ambacho wengine wanakabiliana nacho."
Katika Kaunti ya Bungoma, Catherine Wanjala alikuwa akipata hasara ya mara kwa mara kutokana na magugu yajulikanao kama striga au witchweed, mmea wa vimelea ambao hushambulia mizizi ya mahindi na mtama.
Mbinu za jadi, izikiwemo dawa za kuulia magugu na kubadilisha mazao, hazikufaulu. Kisha alifahamishwa dawa ya kuulia mimea kuvu ambayo iliongeza mavuno yake kwa kiasi kikubwa.
"Kabla ya kutumia dawa ya kuua mimea kuvu, mahindi yangu yalikuwa dhaifu na ya manjano. Hayakukua vizuri," Wanjala aliiambia Xinhua. "Baada ya matibabu, tofauti ilikuwa kubwa kama usiku na mchana."
Mashirika ya kilimo pia yanaongoza katika matumizi ya kidijitali.
Mpango wa Mfuko wa Ekari Moja wa Kenya wa Tupande umeunganisha mafunzo ya AI na mashine katika huduma zake ili kuboresha mapendekezo ya ngazi ya mashamba.
"Tunatumia mifumo ya hali ya juu kurekebisha ushauri kulingana na takwimu za ngazi ya mashamba kama vile unyevunyevu wa udongo na uzalishaji," alisema Makandi Laiboni, mkurugenzi wa mkakati wa kidijitali wa Tupande. "Hata mabadiliko madogo, kama kuongeza tarehe za kupanda, yanaweza kupunguza hasara kwa kiasi kikubwa na kuongeza mavuno."
App ya simu ya Tupande, ambayo ina watumiaji wapatao 150,000 hadi sasa, ni maarufu sana miongoni mwa vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 35.
"Kuwafikia wakulima vijana ni muhimu kwa mustakabali wa kilimo," aliongeza Karigu Ekumbo, Mtaalamu Mwandamizi wa Mawasiliano katika Mfuko wa Ekari Moja. "Wanakubali zaidi zana za kidijitali na kusaidia kuleta matokeo mazuri katika maeneo ya vijijini na mijini."
Kwa mujibu wa Ekumbo, vizuizi bado vipo. Wanawake, kwa mfano, wanaotumia App ya Tupande ni asilimia 30 pekee. "Ijapokuwa hiyo ni juu ya wastani wa kitaifa, tunalenga kuziba pengo la kijinsia katika teknolojia za kilimo kwa kuwapatia msaada wakulima wa kike," Ekumbo alisema.
Utafiti wa hivi karibuni wa Taasisi ya Kenya ya Utafiti na Uchambuzi wa Sera za Umma ulikadiria kuwa ni asilimia 20 hadi 30 pekee ya wakulima wa Kenya wanaotumia teknolojia ya kilimo ya kidijitali.
Utumiaji huu mdogo unabainisha wazi pengo kubwa katika kuongeza huduma hizi, ambazo zina uwezo mkubwa wa kuongeza uzalishaji, faida, na upatikanaji wa soko kwa wakulima wadogo.
"Tulizoea kusubiri na kuwa na matumaini. Lakini sasa tunajua na kuchukua hatua," Ouma alisema, akichunguza shamba lake lenye afya. "Sio uchawi. Ni taarifa nzuri tu tunazopata."