KUNA usemi kwamba ivumayo haidumu au haraka haraka haina baraka kutokana na tukio lililotokea juzi baada ya viongozi wakuu ambao ni waasisi wa Chama cha Jamii (CCJ) kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kutangaza kuwania ubunge kwa tiketi ya chama hicho na kumwacha kiongozi mmoja akifuatana na wanachama zaidi ya 9,000.
Viongozi hao waasisi, Mwenyekiti Richard Kiyabo alitangaza kugombea Bukene mkoani Tabora na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCJ Bara, Dickson Nghily, alitangaza kugombea jimbo la Temeke.
Licha ya viongozi hao waliojiunga na Chadema, Fred Mpendazoe, ambaye alikuwa Msemaji wa Chama hicho baada ya kutoka CCM mwaka huu, alitangaza kugombea ubunge jimbo jipya la Segerea, Dar es Salaam.
Chama hiki kilianza kwa kasi mwanzoni mwa mwaka huu na kupata umaarufu kwa kipindi kifupi na kutaka kuvifunika vyama vyote vya upinzani vilivyochukua miaka zaidi ya 10 kujitangaza na kujiimarisha.
Kama vile ni jambo rahisi, viongozi wake walijitapa kuingia Ikulu katika uchaguzi ujao wakati kilikuwa bado hata hakijapata usajili wa kudumu ambao ungekiwezesha kushiriki uchaguzi mkuu.
Nadhani kujulikana na umaarufu wa chama hicho, kulitokana na viongozi wake kuwa wanenaji wazuri katika vyombo vya habari na kufanya kionekane kama chama chenye watu wakali kisiasa.
Machi mwaka huu, chama hicho kilipata usajili wa muda na hivyo kuongeza ari kwa baadhi ya wafuasi wake na viongozi na kuendelea na ahadi kadhaa huku wakijitapa kushiriki uchaguzi mkuu bila kufahamu taratibu za kupata usajili wa kudumu lakini baadaye walianza kusaka usajili wa kudumu ili kujihakikishia wanashiriki uchaguzi ujao.
Licha ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, kuwashauri mara kwa mara wapate muda wa kutosha kuhakikisha wanajenga chama chao na kupata usajili wa kudumu, viongozi hao walikaidi na kujiona kuwa kwa muda uliopo wanaweza kukamilisha kila jambo.
Dosari zilianza katika kuhakiki wanachama mikoani kwa kuanzia na mikoa ya Pwani, Zanzibar na Dar es Salaam, Msajili John Tendwa alibaini chama hicho kutokuwa na wanachama wa kutosha na kuonesha wazi kuwa viongozi hawa walifanya mambo haraka haraka, hivyo kusababisha kushindikana kupata usajili wa kudumu.
Baada ya kuona wameshindwa na hawawezi kushiriki uchaguzi, sasa wameamua kukimbilia Chadema, jambo la kujiuliza kwa viongozi hao ni kwa nini wanakimbilia kushiriki uchaguzi wa mwaka huu, kwa nini hawakutaka kujipanga na kuimarisha chama kisha kushiriki uchaguzi wa 2015?
Pia viongozi hao wanatia shaka zaidi kwani kama wangekuwa wako kwa maslahi ya nchi, wangefuata utaratibu na kuhakikisha wanapata wanachama nchi nzima, lakini baada ya kuona jitihada zao za kupata usajili wa kudumu zimeshindikana wakakimbilia Chadema, je kulikuwa na ulazima wa kugombea uchaguzi wa mwaka huu?
Nina wasiwasi na viongozi hawa ambao walitafuta wanachama na kufikia zaidi ya 9,000 kisha kuwatelekeza bila kufanya mkutano wowote wa kuazimia kujiunga Chadema, inaonesha wazi kuwa kuna jambo la siri miongoni mwao na inabidi kuangaliwa kwa makini hasa kwa Chadema ambako wamejiunga.
Pengine wasiwasi alionao Katibu Mkuu wa CCJ, Renatus Muabhi, unaweza kuwa wa kweli, kwamba kuna dalili za kujengeka uchu na ulafi wa madaraka miongoni mwa wanasiasa hao, kwamba bila kuingia bungeni mwaka huu, basi malengo yao hayatatimia mwaka 2015.