Kuchujwa kwenye kugombea uongozi kwenye chama kimoja, ukakimbilia chama kingine, ni dalili fika ya uchu wa madaraka. Hivyo ndivyo alivyofanya Lowassa mwaka 2015. Watia nia wakiwa wengi na chama kikapendekeza mmoja wao, wale ambao hawakupendekezwa shurti wakubali uamuzi huo na kumuunga mkono aliyependekezwa. Hiyo ndiyo demokrasia. Kuthubutu kwako kujitokeza kuomba usimamishwe kugombea ni haki yako. Lakini kuchaguliwa mmoja kati ya waliojitokeza, ndiyo mwisho wa kutia nia kwako wewe uliyeachwa. Ulijiona unafaa. Chama kikakuona kweli unafaa lakini mwingine anafaa zaidi. Ndiyo kisa cha kumchagua huyo. Kama wote waliotia nia wakikomaa wasimamishwe wenyewe tu si itakuwa balaa?
Mfano mzuri ulionyeshwa na Rais Magufuli aliposhindwa mara tatu katika uchaguzi wa ubunge. Mara zote alikuwa akiyakubali matokeo kwamba "The people have spoken". Wapiga kura walikuwa hawajui ni nani wanayemkataa. Hata Biblia inasema jiwe alilolikataa fundi mwashi ndiyo limekuwa msingi wa nyumba. Sura nyingine ya Biblia inasema wasamehe kwa kuwa hawajui watendalo. Baada ya takriban miaka hii mitano ya urais wa Magufuli, bila shaka wapiga kura wa Biharamulo wametambua walikuwa hawajui nani waliyekuwa wakimkataa.
Wosia wangu kwa mpiga kura ni kwamba chagua mtu atakayekuletea maendeleo. Siyo kuchagua mtu mwenye uchu tu wa madaraka. Kipofu tu ndiye haoni uwezo wa Magufuli katika kuiendeleza Tanzania. Upinzani unachong'ang'ania ni kumuondoa tu Rais Magufuli madarakani, bila kusema ni kitu gani bora zaidi wao watakufanyia wewe mpiga kura. Ni uchu wa madaraka tu. Mpiga kura kumbuka msemo kwamba zimwi likujualo halikuli likakwisha. Lissu anatajwa sana na upinzani asimame kushindana na Magufuli ambaye tayari ameonyesha nini anaweza kuifanyia Tanzania. Mfano mmoja ni sheria ya madini ambayo Rais Magufuli amebadilisha kwa manufaa ya Tanzania, hata kama bado mpaka sasa hatujalipwa kiasi chote kilichokuwa kikiibiwa. Lissu alikuwa akikomaa Bungeni kwamba tukiwagusa hao mabeberu tutapelekwa mahakamani kwa kuwa tulitia sahihi mkataba. Lissu huyo huyo aling'ang'ana pia Bungeni kuwa kunana mkataba sijui wa lini ambao unasema ziwa Nyasa lote ni la Malawi. Vivyo hivyo alitaja mkataba uliosainiwa kati ya Uingereza na Misri ukitukataza Tanzania kuchukua maji kutoka Ziwa Victoria kupeleka Tabora na Dodoma. Wewe mpiga kura wa Tanzania jiulize mtu kama huyu akiwa Rais si atakuwa anapigania manufaa ya nchi nyingine tu?.