Waliozima hoja ya elimu bungeni uzalendo wao kwa taifa unatia shaka

Waliozima hoja ya elimu bungeni uzalendo wao kwa taifa unatia shaka

sulphadoxine

JF-Expert Member
Joined
Nov 1, 2010
Posts
2,257
Reaction score
649
KATIKA mkutano wa Bunge uliomalizika wiki iliyopita mjini Dodoma, Mbunge wa Kuteuliwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR- Mageuzi, Ndugu James Mbatia, aliwasilisha hoja yake akitaka Bunge liazimie kuitaka Serikali kufanya mabadiliko makubwa ya mfumo wa elimu nchini ambao kwa sasa unaonekana kupoteza mwelekeo. Kwa kutumia uwezo wake binafsi, Mbatia alijenga hoja yake kwa kuelezea udhaifu mkubwa uliopo kwenye sekta ya elimu na kulitaka Bunge la Jamhuri ya Muungano kama chombo chenye wajibu wa kuisimamia Serikali kuchukua hatua ya kuitaka Serikali kurekebisha hali hiyo.

Hata hivyo, Serikali ilijaribu kuizima hoja hiyo kwa kudai kuwa mambo yaliyosemwa na Mbatia yameingizwa kwenye mpango wa Serikali wa maboresho ya elimu na hivyo hakuna haja ya Bunge kuunda kamati ya kuchunguza suala hilo.
Licha ya hoja hiyo kuwa na umuhimu mkubwa kwa mustakabali wa maisha ya watanzania na taifa kwa ujumla, Mbatia alionekana kupingwa na idadi kubwa ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao walionesha ‘kuibeba' Serikali.

Kwa mtazamo wangu kupingwa kwa hoja ya Mbatia na idadi kubwa ya wabunge kunatokana tu na tofauti za itikadi za kisiasa na si kweli kwamba hoja hiyo haikuwa na uzito kama ambavyo imeshughulikiwa. Nasema hivyo kwa sababu wabunge walioonesha kumuunga mkono Mbatia walikuwa ni wale wa kambi ya upinzani ambao idadi yao ni ndogo bungeni, huku wabunge karibu wote wa CCM wakiegemea upande wa Serikali. Kwangu mimi, huu ni ushahidi tosha kwamba katika hoja hii ya elimu wabunge wetu waliweka kando uzalendo kwa taifa lao na kutanguliza maslahi ya vyama vyao. Nasema hivyo kwa sababu baada ya ‘kupuuzwa' kwa hoja ya Mbatia kuhusu elimu, nimejaribu kufuatilia japo kwa uchache hali ya elimu ilivyo nchini na kubaini kuwa uamuzi wa wabunge haukuzingatia kabisa hali halisi ya utoaji wa elimu nchini.

Kwa mfano wiki hii Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Dk. Michael Kadeghe, wakati akizungumza kwenye Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi ambayo hivi sasa imegawanywa na kuwa halmashauri mbili za Mbozi na Momba alisema kuwa ndani ya wilaya yake kuna zaidi ya wanafunzi 28,000 wa shule za msingi wanaosoma kati ya darasa la sita na darasa la saba ambao hawajui kusoma, kuandika wala kuhesabu. Dk. Kadeghe ambaye pia amewahi kuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mwandishi wa vitabu vya somo la Kingereza akawaeleza madiwani hao kuwa asilimia 70 ya wanafunzi waliochaguliwa mwaka huu kujiunga kidato cha kwanza wilayani humo hawana sifa za kuingia darasani kwa sababu walichukuliwa baada ya kukosekana wanafunzi wenye sifa. Akifafanua zaidi, Dk.


Kadeghe alisema kuwa kwa kawaida Serikali huchukua wanafunzi waliofaulu mtihani wa darasa la saba kwa kupata alama za daraja la A, B na C kuingia Sekondari.
Akasema kuwa kwa mwaka huu wanafunzi waliopata madaraja hayo walikuwa wachache mno kiasi cha kusababisha wachukuliwe hata wale waliopata daraja la D na F kujiunga na kidato cha kwanza. Nikirejea kwenye ulingo wa siasa, natambua kuwa mbunge wa jimbo hilo ni Godfrey Weston Zambi, ambaye licha ya kuwa hali ya elimu ndani ya jimbo lake ni tete, hakuthubutu kuiunga mkono hoja ya Mbatia.


Lakini nikifuatilia kwa karibu zaidi nabaini kuwa Zambi ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, asingeweza kuikubali kirahisi hoja ya Mbatia ambaye ni mbunge wa chama cha Upinzani hata kama hoja hiyo ilikuwa ni yenye manufaa kwa wapiga kura wake na wananchi wote wa Jimbo la Mbozi Mashariki kwa sababu tu za kutofautiana kwa itikadi za kisiasa na mtoa hoja. Hapo ndipo najenga hoja kwamba hoja ya Mbatia ilipingwa kwa nguvu zote na idadi kubwa ya wabunge kutoka Chama Cha Mapinduzi sio kwamba ni kwa sababu haikuwa na maslahi kwao, bali ni kutokana na tofauti za kisiasa.


Kwa mantiki hiyo nikaona ninayo kila sababu leo kuitumia makala hii kuwauliza wabunge wa CCM akiwemo Zambi kuwa kwa kupinga hoja ya Mbatia kuhusu uboreshwaji wa elimu nchini kweli walikuwa ni wazalendo kwa taifa au wazalendo wa chama chao cha CCM? Inawezekana wabunge wa CCM waliamua kumpinga Mbatia bungeni ili kuilinda Serikali iliyoundwa na chama chao, lakini kimsingi hiyo haikuwa njia sahihi ya wao kuwatetea wapigakura wao na watanzania kwa ujumla, isipokuwa walipaswa kuibana Serikali ili wajiwekee mazingira mazuri ya kuaminika, kupendwa na hata kuchaguliwa tena na wapigakura wao.


Nasema hivyo kwa sababu naamini kwa jinsi hali ya elimu ilivyo mbaya katika shule zetu hasa shule za Msingi na Shule za Sekondari za kata, inawezekana ikawatia chuki wapigakura na sitashangaa mwaka 2015 nitakapoona idadi kubwa ya wabunge wa CCM walipinga hoja ya elimu iliyotolewa na Mbatia wakiangukia pua na kushindwa kurejea bungeni. Lakini athari nyingine inayoweza kuwaathiri wabunge na Chama Cha Mapinduzi kwa ujumla ni vijana wanaohitimu katika shule hizo wakiwa ‘mbumbumbu' au na kiwango duni cha elimu kushawishiwa kirahisi na vyama vya upinzani hivyo kutumika kukiangusha Chama Cha Mapinduzi na Serikali yake katika siku zijazo. Nasema hivyo kwa sababu hata kama Serikali ya Chama Cha Mapinduzi itafanya mambo mazuri na makubwa kwa Watanzania, kama vijana hawana elimu ya kutosha kutambua mambo hayo mazuri, ni kazi bure kisiasa kwani vijana hao hawata kuwa na uwezo wa kuchanganua mambo na mwishowe kukubali kuwa mashabiki, wanachama na wapigakura wazuri wa vyama vya upinzani na hivyo kukiweka Chama Cha Mapinduzi na Serikali yake katika wakati mugumu.

Kwa mtazamo wangu wabunge wa CCM kama kweli wanakitakia mema chama chao katika siku za usoni, wanapaswa kuwa wakali katika masuala ya msingi kama vile elimu na kuilazimisha Serikali kutekeleza wajibu wake ili baadaye iwe na mtaji wa vijana wasomi, weledi na wenye mtazamo chanya wa kuendeleza chama hicho. Hilo lisipofanyika leo, naamini kuwa ni bomu linalosubiri kulipuka katika siku za usoni na litakapolipuka wasije wakamtafuta mchawi mingoni mwao juu ya tatizo litakalowapata. Lakini kubwa zaidi nililotaka kulisema katika makala hii ni shaka juu ya uwezo wa kufikiri wa wabunge wetu hasa wale wa CCM katika masuala ya msingi kama vile uboreshwaji wa elimu kwa Watanzania.

Najiuliza kama kweli ni agizo kutoka kwenye uongozi wa chama chao ndilo linalowasukuma kutokubaliana na hoja za wapinzani zenye maslahi kwa taifa au wao wenyewe wanajipendekeza kwa chama ili kujiwekea mazingira mazuri ya kuendelea kuteuliwa na chama chao kuwania nafasi walizonazo kwenye chaguzi zijazo.


Lakini kwa vyovyote inavyokuwa, hapa swali la msingi ni kwamba kwa namna wanavyo vyanya kweli wabunge hawa wanao uzalendo wa kweli kwenye taifa lao?
Mungu Ibariki Tanzania!
 
Back
Top Bottom