Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
''WAMATUMBI WANAVAA KANIKI TU''
Jana rafiki yangu Abdallah Said Hancha katika shughuli zake za utafiti kaniletea picha iliyokuwa na ''caption'' - ''Wakubwa wa Moshi'' iliyokuwa katika gazeti la Mamboleo la mwaka wa 1934.
Wakubwa hawa ni Mangi yaani machifu waliokuwa wakitawala Uchaggani.
Baadhi ya machifu hawa walikuwa wamevaa suti na kufunga tai.
Picha hii ikawa imenifurahisha sana kwa kuwa ndani yake kulikuwa na machifu ambao nilikutananao wakati natafiti kitabu cha Rajabu Ibrahim Kirama.
Nilisisimka kuwaona machifu hawa katika picha hii na hivyo kuziangalia haiba zao kama walivyokuwa zaidi ya miaka 86 iliyopita.
Nikaandika makala na kuiweka hapa barzani na nakala ya makala hii nikaiweka JF.
Msomaji mmoja akaiona kule JF na bahati mbaya kwake yote niliyoandika hakuyaona kama yana umuhimu wowote katika historia ya Uchaggani ila alichokiona yeye ni kuwa Wachagga walikuwa wameendelea sana kwa nyakati zile kwa kuvaa suti na tai wakati Wamatumbi huku pwani walikuwa wanavaa kaniki.
Maneno haya yalinisikitisha na kunidhihirishia kuwa bado watu wetu wako katika dimbwi kubwa la kiza katika uelewa wa mambo na kufahamu historia ya Tanganyika na watu wake.
Nikaamua kumjibu na kumpa darsa dogo kuhusu mavazi.
Nilichokifanya nilimfahamisha kuwa mavazi yanaendana na utamaduni wa jamii husika wala si kielelezo cha udhalili wa watu.
Sikuishia hapa.
Nilimwekea na picha ya mwaka wa 1933 ya babu zangu, Mashado Ramadhani Plantan, Mwalimu Mdachi Shariff, Kleist Sykes na wao pia wakiwa wamevaa suti na tai kama walivyovaa Mangi Abdiel Shangali, Petro Itosi Marealle na Ngilisho Sina.
Huyu ndugu yangu baada ya kusoma na kuona picha ile akanijibu kuwa ameelewa.
Naamini picha hii niliyomwekea imemuondolea ile fikra aliyokuwanayo ya kuwa kivazi cha kanzu, msuli, khanga na kaniki za Wamatumbi ni lebasi dhalili na suti za Wazungu walizokuwa wakivaa Wachagga ni bora.
Mvaaji wa nguo dhalili na yeye mwenyewe ni dhalili.
Nimeweka na picha yangu na ndugu yangu Kapufi Yunge tuliyopiga studio ya Victor au Gomez Acacia Avenue (sasa Samora Avenue) mwaka wa 1956, mimi ni huyo kushoto nikiwa na miaka 4.
Kabla ya kupelekwa studio tulipelekwa kwa kinyozi kukatwa nywele.
Siku zile kinyozi anakuwa chini ya mti na mbele kaweka kioo kikubwa kakiegemeza kwenye huo mkwaju au mkungu na anakata nywele kwa mkasi na wembe.
Kwa kuhitimisha naweka na picha ya waasisi wa TANU iliyopigwa mwaka wa 1954 atazame mavazi yao ili apate kujifunza zaidi.



