Spika wa Bunge Samuel Sitta amesema Rais Jakaya Kikwete hakukiuka sheria wala taratibu zo zote za fedha, kwa kuamuru baadhi ya fedha zilizokuwa katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) zitumike kwa ajili ya ruzuku ya mbolea na mikopo ya kilimo katika Benki ya TIB.
Kwa mujibu wa Spika, taarifa kuhusu kupatikana na kutumika kwa fedha hizo inaweza kuletwa bungeni. Ni utaratibu sahihi kabisa, alisema Spika Sitta. Alitoa ufafanuzi huo baada ya Suzan Lyimo (Viti Maalumu - Chadema) kutaka ufafanuzi huo kutoka kwa Spika kama ilikuwa sahihi kwa Rais kugawa fedha hizo.
Kauli kama hiyo pia iliwahi kutolewa katika vyombo vya habari na wabunge wengine wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa (Karatu) na Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini), ambao walijenga hoja kwamba Bunge ndilo lenye jukumu la kugawa fedha za matumizi kwa serikali.
Spika, ambaye alimwambia Lyimo kwamba amechomekea swali kwake, alisema kazi ya Bunge ni kuridhia na si kupanga matumizi ya serikali. Aliwataarifu wabunge kwamba mara kadhaa, mara baada ya kikao cha Bajeti, hupatikana fedha kutoka vyanzo mbalimbali, wakiwamo nchi wafadhili au watu binafsi kama bilionea Bill Gates wa Marekani. Zinaletwa wakati bajeti imepita na serikali haiwezi kuzikataa. Baadaye inaleta taarifa bungeni, alisema Spika.
Wakati akilihutubia Bunge wiki iliyopita, Rais Kikwete alitangaza kutwaa mabilioni hayo ya EPA, ambayo sehemu yake yalikuwa yamekwapuliwa, na kuyaelekeza katika mfuko wa ruzuku na Benki ya TIB. Ingawa hatua hiyo ilishangiliwa na wananchi, wabunge wa Chadema wanaendesha kampeni ya kueleza kuwa alikosea taratibu, kwani fedha hizo zilipaswa kufikishwa bungeni na lenyewe ndilo lingeweza kuamua zipelekwe wapi.
Source: HabariLeo