Wasalaam wanaJf. Naomba msaada juu ya Mwanzo 6:1-4. Ukisoma hii andiko unakutana na wanadamu, wana wa Mungu na Wanafili. Biblia inasema wana wa Mungu waliwaoa binti za binadamu na wakazaa nao. Muunganiko huu ulizaa majitu makubwa sana tena hodari walioitwa Wanefili.Suali langu ni kuwa hawa wana wa Mungu ni nani hasa, ni malaika au?
Mungu alichukizwa na matendo ya binadamu na akaamua kugharikisha watu wote isipokuwa familia moja watu wanane. Cha ajabu haya majitu makubwa wanaonekana kuwepo hata baada ya gharika. Ushahidi upo Hesabu 13:31-33. Hawa wana wa Anaki waliponaje kwenye gharika?
Swali la Kibiblia litajibiwa kwa sehemu kubwa Kibiblia. Nitajitahidi. Neno "wana wa Mungu" katika Biblia lina maana ya watoto wa Mungu. Hao ni wale wanaomcha Mungu miongoni mwa wanadamu (Yoh 1:11-12) hata na malaika (Ayubu 1:6, 2:1; 38:7) ukitofautisha na wale malaika walioasi ama wale wanadamu waliomwasi Mungu kabisa. Hao wote wanapoteza ile heshima ya kujumuishwa katika nyumba ya Baba Mungu (Ufu 12: 7-12).
Kabla ya gharika na baada ya anguko la Adamu kilitokea kizazi ambacho kiliamua "kuliitia tena Jina la Mungu," yaani kumgeukia Mungu na kumwabudu katika kweli (Mwa 4:36). Daima Mungu hutafuta kizazi cha aina hii kila mara; ama watu wa jinsi hii kila mara panapotokea shida ya uasi kuwaokoa wengine watakaopenda kurejea kwa Mungu(Yeremia 5:1).
Kibiblia wana wa Mungu basi ni wale miongoni mwa wanadamu wanaomcha Mungu. Hao hawakuruhusiwa kuoa nje ya wenzao walio "wana wa Mungu" yaani wachaji Mungu pia. Hili pia lilikuwa katazo kwa Israeli wasioe miongoni mwa wageni ama makabila yaliyopo Kanaani (Kumb 7:1-5). Hilo likifanyika linaleta hasira ya Mungu kama iliyotokea kwa Sulemani alipooa wanawake wa Kanaani (I Fal 11:1-13). Mungu alimwondosha katika Ufalme na akafutika kwa kiasi fulani.
Kwa maana hiyo inakuja laana, yaani kukosekana kwa Baraka ya Mungu. Basi chochote chaweza kutokea kama matokeo ya anguko hilo. Uzao unaweza kuharibika, vizazi vinavyokuja vikafikiwa na matokeo ya matendo maovu ya babu zao. Ndivyo ilivyokuwa katika Mwa 6. Wasomi wa Biblia wanasema hao wana wa Mungu ni ule uzao wa Sethi ulioamua kumgeukia Mungu. Waliendelea vizuri lakini wakaja kuharibika na kujitwalia wake miongoni mwa jamii isiyomcha Mungu (Mwa 6:1-4). Hao Wanefili (majitu) ni mbegu mbaya iliyotokana na mchanganyiko huo. Mungu aliumba mwanadamu kamili maana uumbaji wake wote ulikuwa mwema (Mwa 1:1-31). Hivyo wacha Mungu wakawaoa wasio wacha Mungu na kuzaa nao. Malaika hawezi kuoa na kuzaa Yesu anatuambia (Luka 20: 29-36)
\v 29 Basi, kulikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa mke, akafa hana mtoto; \v 30 na wa pili [akamtwaa yule mke, akafa hana mtoto;] \v 31 hata wa tatu akamwoa, na kadhalika wote saba, wakafa, wasiache watoto. \v 32 Mwisho akafa yule mke naye. \v 33 Basi, katika ufufuo atakuwa mke wa yupi? Maana aliolewa na wote saba. \v 34 Yesu akawaambia, Wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa; \v 35 lakini, wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi; \v 36 * wala hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo.
Malaika watakatifu ama wale waasi (mashetani) hawana miili kama ya kwetu. Wana miili ya roho naweza kusema – miili ya roho iliyotukuka (Malaika watakatifu) na miili ya roho iliyolaaniwa (mashetani). Paulo anafafanua sana juu ya tofauti ya hii miili. Anaita mwili wa asili na mwili wa roho (1 Kor 15: 35-49). Hivyo, ndoa ni ya hapa duniani. Wawili watakuwa mwili mmoja. Basi malaika haoi wala haolewi.
Kwa hiyo wanaohusika na Mwanzo 6 ni wanadamu tu – wachaji wa Mungu na wale wasiomcha Mungu kuoana na hatimaye mbegu tofauti kutokea.
Sasa kwa mtazamo wa kibiblia uharibifu ukiisha ingia ulimwenguni huendelea kuwepo mpaka mwisho wa mambo yote (2 Pet 1: 1-4). Kwa mfano mauti iliingia nayo bado ipo, ila kuna ahadi ya ufufuo wa baadaye (Yoh 6:39-40). Magonjwa bado yapo (ila uponyaji wa Mungu nao upo - Marko 16:15-20). Umaskini bado upo ila mtu akifanya kazi kwa bidii ataondokana nao (Mith 6: 6 -11). Ilibidi Israeli wakae Misri miaka mia nne mpaka pale uovu wa Waamori utakapotimia (Mwa 15:13 -16). Ndio maana hata Shetani yupo vile vile akiendeleza uovu wake mpaka wakati wake utimie. Wana theolojia na wanafalsafa wa dini wanajadiliana sana juu ya hili. Kwa nini Biblia inasema Shetani anao muda mchache (Ufu 12: 1 -9). Yesu naye alikuja pale utimilifu wa wakati uliomhusu ulipotimia (Gal 4:4). Tunajiuliza kwa nini Yesu alisema usiwatoe ulimwenguni bali uwalinde na yule mwovu (Yoh 17:15). Majitu hayo, na wote watendao mabaya, ma-Anti Kristo na wengineo wataendelea kuwepo hadi wakati husika ulioamriwa. Cha msingi hawana uwezo wa kuyadhuru maisha ya yule aaminiye ambaye daima hulindwa na nguvu za Mungu.
Mkumbuke Daudi alimuua Goliath. Hao wana wa Anaki, hawakuwazuia israeli kusafiri kuelekea Kanaani. Uharibifu huo ni pamoja na ule wa watu wafupi sana yaani mbilikimo. Hawa nao tusemeje. Namfahamu mhubiri ambaye ni mlemavu kabisa na anawaombea walemavu wapone yeye yupo hapo hapo. Paulo alikuwa na shida katika mwili wake ikimtatiza. Aliomba Mungu itoke, na Mungu akamwambia endelea na udhaifu huo maana hapo ndipo penye nguvu na uweza wangu (1 Kor 12:7 - 10)