Kumekuwepo na picha zinazosambaa mtandaoni zikionesha wanadiplomasia nchini Kenya wakiondoa kurejea makwao kwenye uwanja wa Jomo Kenyatta.
Inasemekana wamefanya hivyo baada ya kupewa notisi ya muda mfupi na Serikali ya nchi hiyo ikiwataka waondoke haraka.
Picha inayohusishwa na tukio la Wanadiplomasia kuondoka Kenya (Picha 1)
Inasemekana wamefanya hivyo baada ya kupewa notisi ya muda mfupi na Serikali ya nchi hiyo ikiwataka waondoke haraka.
Picha inayohusishwa na tukio la Wanadiplomasia kuondoka Kenya (Picha 1)
- Tunachokijua
- Julai 16, 2023, saa 11:27 jioni, Mtumiaji wa Mtandao wa Twitter anayefamika kwa jina la PhinelSenior aliweka ujumbe unaoelezea kuwa wanadiplomasia nchini Kenya walikuwa wameanza kuondoka nchini humo kufuatia amri ya Serikali ya nchi hiyo iliyowataka waondoke ndani ya muda mfupi.
Ujumbe huo nasema;
"Happening now at JKIA. Why are diplomats leaving Kenya in such a hurry and short notice? Is there something they know that we don't? Kuna kitu hatuambiwi hapa."
Hadi kufikia Julai 17, 2023, saa 3:15 asubuhi, ujumbe huu ulikuwa umesomwa zaidi ya mara 186,400, ulipendwa mara 2087 na watu 338 walishirikisha wengine.
Katika mjadala huo, baadhi ya wachangiaji walionesha kuafiki huku wengine wakipinga.
Pia, siku hiyo ya Julai 16, 2023, ukurasa mwingine wa Mtandao wa Twitter unaofahamika kwa jina la Movement for Defense of Democracy (MDD) iliweka ujumbe unaodokeza pia uwepo wa jambo hili.
Ujumbe huu ulio ambatana na picha ileile ya ndege ikiwa na nyongeza ya wasafiri wengine walio na mabegi ulisema;
"JKIA turns chaotic as amidst Diplomats rush out of the Country in a short notice. Flights to most African countries affected to allow planes enroute specific destinations. Sabina Murkomen Uhuru Thursday"
Hadi kufikia Julai 17, 2023, saa 3:15 asubuhi, ujumbe huu ulikuwa umesomwa zaidi ya mara 55,500, ulipendwa mara 507 na watu 98 walishirikisha wengine kwenye mtandao huo.
Ukweli wa Picha hizo
Picha nyingine inayohusishwa na tukio hilo (Picha 2)
Baada ya kusambaa kwa taarifa hizi, JamiiForums imechukua jitihada mbalimbali za kiuchunguzi kubaini ukweli wake.
JamiiForums imebaini kuwa tukio halisi linalohusiana na picha hili liliwekwa kwenye mtandao wa YouTube Novemba 9, 2019 na chaneli inayofahamika kwa jina la The Luxury Travel Expert. Ilikuwa inafafanua safari iliyoanzia uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Nairobi Jomo Kenyatta kuelekea Lusaka Zambia. Mhusika wa video hiyo alisafiri mwenyewe kwa lengo la mapumziko.
Aidha, Novemba 13, 2019, blog yenye uhusiano na chaneli hiyo ambayo pia inaitwa The Luxury Travel Expert iliweka chapisho linalofafanua kwa kina undani wa safari hiyo.
Chaneli ya YouTube na Blog hii zinamilikiwa na mtu mmoja. Hii inaweza kuthibitishwa kwa kutazama wasifu uliowekwa kwenye mtandao wa YouTube unaoziunganisha.
Pia, blog husika imewekewa kiunganishi kinachothibitisha uhusiano wake na chaneli ya YouTube iliyoweka maudhui hayo.
Taarifa za Ndege na Safari husika
Hizi ni taarifa zinazohusiana na safari husika pamoja na ndege iliyotumika;
- Safari: Nairobi (NBO) kwenda Lusaka (LUN)
- Kampuni ya Ndege: Kenya Airways
- Aina ya Ndege: Boeing 737NG
- Namba za usajili wa Ndege: 5Y-CYC (Imetengenezwa mwaka 2015)
- Namba ya ndege: KQ706
- Tarehe ya safari: Agosti 31, 2019
- Muda wa kuanza safari: Saa 1:15 asubuhi
- Muda wa kumaliza safari: Saa 2:45 asubuhi
Aidha, picha namba 2 inayoonesha wasafiri wakiwa uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta iliwekwa mtandaoni kwa mara ya kwanza Novemba 5, 2022 wakati wa mgomo wa marubani wa Shirika la Ndege la Kenya walipokuwa wanadai kuboreshewa maslahi yao.
Picha hii pia haina uhusiano na kile kinachotajwa kuwa ni safari ya wanadiplomasia kuondoka Kenya.
Uwepo wa notisi kwa wanadiplomasia nchini Kenya
Baada ya kubaini kuwa picha zinazosambaa mtandaoni hazina uhusiano wowote na tukio la kufukuzwa kwa wanadiplomasia nchini Kenya, ni muhimu sasa kufahamu kama kuna tukio lolote, au taarifa inayoonesha au kudokeza kuwa nchi ya Kenya imetoa notisi yoyote inayotaka wanadiplomasia waondoke nchini humo.
Kupitia vyanzo mbalimbali vya kuaminika, JamiiForums imebaini kuwa hakuna notisi yoyote iliyotolewa na Serikali ya Kenya inayotaka Wanadiplomasia wa nchi mbalimbali kuondoka nchini humo.
Hivyo, taarifa hii inayoambatana na picha kwa ujumla wake haina ukweli.