JK aja na ndoto mpya
na Asha Bani
RAIS Jakaya Kikwete, amesema kuwa serikali imekwishakamilisha mpango wake unaoitwa 'Tanzania Beyond Tomorrow' ambao utahakikisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano kila mwalimu atakuwa na ‘laptop' yake. Kikwete aliyasema hayo Ikulu juzi wakati alipokutana na baraza la watoto kutoka mikoa mbalimbali, ikiwa ni maadhimisho ya kilele cha mtoto wa Afrika ambapo watoto hao walipata nafasi ya kumuuliza rais maswali mbalimbali.
Kauli hiyo ya Rais Kikwete kwamba walimu watakuwa na laptop, ilitokana na swali aliloulizwa na mtoto Zurekha Kipupwe (14) kutoka Dar es Salaam, aliyehoji hatua ambazo serikali inazichukua kutokana na ukosefu wa walimu, nyumba, vitabu vya ziada na kiada, na maabara katika shule za kata.
Katika majibu yake, ndipo Rais Kikwete alipogusia kuhusu mpango huo Tanzania Beyond Tomorrow ambao alisema kuwa utahakikisha katika kipindi cha miaka mitano kila mwalimu anakuwa na laptop, yake na baada ya hapo kila mwanafunzi atakuwa na kompyuta yake.
Alisema, wao kama serikali watahakikisha mpango huo unafanikiwa na kwamba kwa kuanzia wataanza na mikoa sita kwa kuhakikisha kuwa walimu wote wa shule za msingi na sekondari wanakuwa na laptop na wanafunzi kompyuta.
Alisema tayari wamekwishafanya mazungumzo na wataalamu kutoka kwa wahisani kama vile Google na wengineo ili kuhakikisha mpango huo unafanikiwa.Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha kuwa walimu wanaacha kutumia chaki kama wenzetu Burundi ingawa sisi tumechelewa kuanza kutekeleza hilo. Awali akijibu swali na mtoto huyo, rais alikiri kuwa matarajio ya serikali ilikuwa ni kuhakikisha miaka mitano inatumika katika kujenga shule za kata lakini pia imeonekana wazazi walikuwa na shauku katika kujenga shule nyingi.
Pia alisema kuwa suala la upungufu wa walimu linashughulikiwa na kwamba serikali imeanzisha chuo cha Dodoma, Chang'ombe, Chuo Kikuu kishiriki cha Dar es Salaam, na chuo cha Mkwawa. "Hata hivyo kuhusiana na vitabu vya ziada na kiada serikali iko kwenye mkakati wa kuhakikisha kuwa kunapatikana vitabu kwa kuwa kwa sasa tunasubiri pesa tu kutoka kwa wahisani na kwa sasa tayari tumefikia katika hatua nzuri na wafadhili," alisema Rais Kikwete. Mbali na swali hilo, watoto hao walionekana kumuuliza rais maswali kadhaa mazito ikiwa ni pamoja na yale yanayohusiana na ufisadi.
Deogratius Michael (16), kutoka mkoa wa Mwanza alimuuliza Rais: "Kwa kuwa serikali imewashughulikia mafisadi kwa kuzikusanya fedha zilizochotwa na wengine kupelekwa mahakamani, je, kwa nini fedha hizo zisingepelekwa kwenye elimu?"
Akijibu hilo rais alikiri sekta ya elimu kuwa na matatizo mengi lakini akasisitiza kuwa kilimo ni muhimu katika kuhakikisha chakula cha kutosha kinaongezeka nchini. "Fedha hizo zilizokusanywa ni shilingi bilioni 40 na zimetumika katika kufungua dirisha la kilimo katika Benki ya TIB na fedha nyingine zimetumika katika kununulia pembejeo za kilimo ikiwa ni pamoja na mbolea na kutokana na hilo mavuno yameongezeka.
Maswali mengine aliyoulizwa ni pamoja na mpango wa serikali kuwarudisha mashuleni wanafunzi waliopata mimba na kisha kuendelea na masomo; rais alijibu kuwa suala hilo bado wanaendelea kufanya mazungumzo na wanaharakati. Wanaharakati wametofautiana: kuna kundi linadai warudishwe na sheria ipitishwe na wengine wanadai wasiruhusiwe. Akitolea majibu swali lingine aliloulizwa kwamba serikali inawasaidiaje wanafunzi walioshindwa kuendelea na masomo kwa kukosa ada Kikwete alisema kuwa serikali ina utaratibu wa wanafunzi wote waliokuwa na matatizo ya ada kujiandikisha halmashauri ambapo wanakuwa na mafungu yao kwa ajili ya kuwasomesha watoto.
Alieleza kuwa endapo halmashauri itazidiwa uwezo wa kuwasomesha watoto hao kama watakuwa wameomba wengi basi wanawasiliana na makao makuu na wanasaidiwa kwa hilo. Hata hivyo baada ya mahojiano hayo wanafunzi hao walimtaka Rais Jakaya Kikwete kuongeza muda wa miaka mitano na kupata ushindi wa kishindo tofauti na ule alioupata mwaka 2005..