Wanafunzi saba wanaosoma Shule ya Msingi Yombo Buza, jijini Dar es Salaam wamefukuzwa shule na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya kutajwa na wanafunzi wenzao kuwa ni vinara wa kuwalawiti wenzao.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Steven Kailembo, aliithibitishia NIPASHE Jumapili kuhusu kufukuzwa kwa wanafunzi hao kufuatia uchunguzi uliofanywa na gazeti hili baada ya kushamiri kwa vitendo hivyo katika shule za msingi.
Kailembo aliwataja wanafunzi hao (majina tunayo), baadhi yao wakiwa darasa la saba na wengine darasa la sita, wakati mmoja wao anaendelea kufanyiwa uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo.
Mwalimu Kailembo alisema Kamati ya shule imeridhia kufukuzwa kwa wanafunzi hao ili usalama uweze kuwepo kwa wanafunzi waliobaki. "Tumeona tuwafukuze kwani watu wachache hawawezi kutuharibia wanafunzi waliobaki," alisema Kailembo.
Alisema kabla ya kuwafukuza wanafunzi hao walibaini kuwa mwanafunzi wa darasa la nne ambaye ni mvulana alifanyiwa kitendo cha kulawitiwa na kuharibiwa ambapo mpaka sasa bado anaendelea kupatiwa matibabu baada ya kuharibiwa vibaya.
Kailembo alisema taarifa dhidi ya tukio hilo aliliwasilisha kwa Afisa Elimu wa Manispaa ya Temeke ambapo katika kipindi hicho waliagizwa maafisa elimu kulishughulikia suala hilo shuleni hapo. Alisema baada ya maafisa hao kufika shuleni hapo waliwafundisha wanafunzi kuhusu usalama wao kujitambua na kusema kitendo chochote kibaya wanachokiona au kufanyiwa.
Alisema baada ya hapo zoezi lililofuata kila mwanafunzi alitakiwa kuandika jina la mwanafunzi yeyote ambaye anajihusisha na vitendo vya kuwalawiti wenzake au kama alishawahi kufanyiwa vitendo hivyo aandike na kumtaja mtu aliyemfanyia.
Alisema zoezi hilo llilikwenda vizuri na lilianzia kwa darasa la kwanza hadi la darasa la saba.
Kailembo alisema wanafunzi 11 walitajwa katika shule nzima na kwamba walivyoendelea na uchunguzi wao dhidi ya majina ambayo yametajwa walibaini majina saba ya wanafunzi waliotajwa kuwa vinara wa kuwalawiti wenzao.
"Wanafunzi hao saba ambao wengi wao wapo darasa la saba walionekana ni vinara katika kura zilizopigwa na wanafunzi na maajabu mengine hata wanafunzi wa darasa la kwanza waliwataja katika kura walizopiga na kila darasa lilikuwa likiwataja wanafunzi hao," alisema.