Taasisi ya Mifupa-MOI
Senior Member
- Apr 15, 2025
- 118
- 214
Jumla ya wananchi 537 wamepatiwa huduma za kibingwa na kibobezi katika banda la Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Maadhimisho hayo yamehitimishwa leo, Juni 23, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe ambapo wananchi walipata fursa ya kuonana na Madaktari Bingwa na wataalamu kutoka MOI na kupatiwa ushauri, uchunguzi pamoja na matibabu ya awali ya magonjwa ya mifupa, ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu.
Akizungumza katika banda la MOI, Daktari Bingwa Bobezi wa Mifupa MOI Dkt. Godshal Mringo, amesema kuwa idadi kubwa ya wananchi waliowahudumia walikuwa na changamoto mbalimbali za mifupa, hususan maumivu ya magoti , nyonga na amumivu ya mgongo.
“Wananchi wengi tuliowapokea walikuwa na matatizo yanayohusiana na mifupa, hasa maumivu ya magoti , nyonga, maumivu ya mgongo na kichwa. Wengi wao tumewapatia ushauri wa kitaalamu pamoja na dawa za kutumia ili kupunguza au kuondoa changamoto hizo. Aidha, kwa wale waliobainika kuhitaji uchunguzi na matibabu ya kina zaidi, tumewapa rufaa ya kufika MOI kwa huduma zaidi,” amesema Dkt. Mringo.
Kwa upande wake, mmoja wa wananchi waliopata huduma katika banda hilo, Bi. Grace Kussaga, ameipongeza MOI kwa kuendelea kusogeza huduma za afya karibu na wananchi kupitia maonesho na matukio mbalimbali ya kitaifa.
“Tumepokelewa vizuri na wataalamu wa MOI na tumepata elimu pamoja na huduma za afya ambazo zimetusaidia kuelewa hali zetu za afya. Tunawashukuru kwa kuwaletea wananchi huduma hizi karibu zaidi,” amesema Bi. Kussaga.
MOI imekuwa miongoni mwa taasisi zilizoshiriki Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa kutoa elimu ya afya na huduma za uchunguzi wa awali, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha upatikanaji wa huduma za kibingwa na kibobezi karibu na wananchi.