Rais Xi Jinping wa China
Xi Jinping alipokuwa na umri wa miaka 59 aliteuliwa kuwa Katibu mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China kwenye Mkutano wa Kwanza wa Wajumbe Wote wa Kamati Kuu ya 18 ya Chama hicho, na ni kiongozi mkuu wa kwanza wa China aliyezaliwa baada ya kuanzishwa kwa China mpya. Baada ya Mao Zedong, Deng Xiaoping, Jiang Zemin na Hu Jintao, Chama cha Kikomunisti cha China kilikuwa na kiongozi mpya. Katika kipindi muhimu zaidi cha kujenga jamii yenye maisha bora kwa pande zote, Xi Jinping aliingia katikati ya jukwaa la kisiasa la China na kubeba majukumu ya kihistoria. Aidha, akiwa kiongozi wa nchi ambayo inashika nafasi ya pili kwa ukubwa wa uchumi duniani, pia yuko kwenye mstari wa mbele katika jukwaa la kimataifa.
Watu wote wa China na dunia nzima wanamwangalia Xi Jinping: Ataongoza vipi Chama kikubwa zaidi duniani ambacho kina wanachama zaidi ya milioni 82 kuutumikia umma vizuri zaidi? Atawaongoza vipi wachina bilioni 1.3 kufanya juhudi za kutimiza malengo mawili makuu ya “kukamilisha kazi ya kujenga jamii yenye maisha bora kwa pande zote ifikapo miaka 100 tangu Chama cha Kikomunisti cha China kianzishwe”, na “kukamilisha kazi ya kujenga nchi ya kisasa ya kijamaa yenye ustawi, demokrasia, ustaarabu na masikilizano ifikapo miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China”?
Ataiongoza vipi China ili kutoa mchango ipasavyo kwa ajili ya amani na maendeleo ya dunia?
Mchana wa tarehe 15, Novemba baada ya kufungwa kwa Mkutano wa Kwanza wa Wajumbe Wote wa Kamati Kuu ya 18 wa Chama, Xi Jinping alikutana na waandishi wa habari zaidi ya 500 wa China na wa nchi mbalimbali, akiwaelezea wazi kuwa anabeba wajibu mzito na alisema viongozi wa awamu mpya wanabeba wajibu wa aina tatu: wajibu kwa taifa, wajibu kwa wananchi na wajibu kwa Chama.
Ahadi hii aliyotoa kwa makini inaonesha kuwa, Xi Jinping atabeba wajibu wa kihistoria kwa Taifa la China na kuuchukulia kuwa ni nia yake na utafutaji wake wa kuendesha utawala wa nchi.
Novemba 29, 2012, Xi Jinping, Zhang Dejiang, Yu Zhengsheng, Liu Yunshan, Wang Qishan na Zhang Gaoli walitembelea maonesho ya “Njia ya ustawishaji”kwenye Jumba la makumbusho la taifa la China, na kutoa kwa mara ya kwanza wito wa Kutimiza Ndoto ya China ya ustawishaji mkubwa wa Taifa la China.
“Matarajio ya Wananchi juu ya Maisha bora, hilo ndio tunalopigania”, Bw. Xi Jinping aliwaambia waandishi wa habariakiongea mara ya kwanza baada ya kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China.
Muda mfupi baada ya kuingia madarakani, Bw. Xi na wajumbe wengine wa kudumu wa Kamati Kuu ya Chama walitembelea Maonyesho ya “Njia ya Kuelekea Ustawishaji”. Kwenye maonyesho hayo alisema: “Siku hizi, kila mtu anaongelea ndoto ya China, kwa maoni yangu, kutimiza ustawishaji mkubwa wa Taifa la China ni ndoto kubwa zaidi katika historia ya Taifa la China tokea Zama za Karibu”.
Xi Jinping anaendesha mkutano kuhusu maendeleo kwenye Ukumbi Mkuu wa Umma wa Beijing
Ili kutimiza lengo hili, Bw. Xi alieleza msimamo wake na kutoa mapendekezo yake kuhusu mambo mbalimbali ya maendeleo ya nchi. Kuhusu Maendeleo ya Uchumi, Bw. Xi anapinga kuangalia maendeleo ya uchumi peke yake, bali pia anahimiza msingi wa kujiendeleza kwa njia ya kisayansi, inaibidi China ijitahidi kujipatia maendeleo endelevu kwenye msingi wa kufanya usimamizi wa raslimali na mazingira ya asili.
Kuhusu Maendeleo ya Mambo ya Siasa, anasisitiza wazo la madaraka yote kuwa mikononi mwa umma na kuhimiza kwa hatua madhubuti mageuzi ya mfumo wa kisiasa huku njia ya Ujamaa wenye umaalum wa China ikiendelea kufuatwa. Pia alisisitiza kufuata kwa makini kanuni za Katiba ya Nchi, kuenzi misingi ya Katiba ya Nchi, kutekeleza majukumu yaliyowekwa kwenye Katiba ya Nchi, kufanya utawala wa nchi kwa mujibu wa sheria na kufanya mambo ya utawala kwa mujibu wa Katiba ya Nchi.
Kuhusu Maendeleo ya Mambo ya Utamaduni, anahimiza kuwaandaa watu wenye utaalamu, na kuhimiza kulea moyo wa kupenda Taifa la China, hasa kama ilivyoelezwa kwenye Wimbo wa Taifa: “Tutatumia miili na damu yetu kujenga ukuta wetu mkuu mpya”.
Kuhusu Maendeleo ya Jamii, amesisistiza kukumbuka kwa makini kuwa bado tuko katika hatua za mwanzo za Ujamaa. Tunatakiwa kuendelea na juhudi za kuhakikisha na kuboresha kiwango cha maisha ya watu kwenye msingi wa maendeleo ya uchumi, kuwa na mtazamo sahihi kuhusu heri na baraka, kuongeza mwamko wa kuchapa kazi zaidi kwa ajili ya kujenga maisha mazuri, na kufanya juhudi za pamoja kutoka kwa sekta zote ili kujenga jamii yenye masikilizano. Kuhusu Maendeleo ya Mazingira ya Asili, Bw. Xi anasisitiza umuhimu wa mkakati wa taifa wa kubana matumizi ya maliasili na kulinda mazingira ya asili, kufuata njia ya maendeleo endelevu na kutoa mchango kwa ajili ya maendeleo ya kudumu ya binadamu.
Aprili 9, 2013, Xi Jinping alipofanya ukaguzi huko Hainan, alivaa kofia iliyotengenezwa kwa mianzi aliyopewa na watu wa kabila la Wali kwenye Bustani ya shughuli za waridi ya Lande Ghuba ya Yalong
Kutoka Uwanda wa Juu wa kaskazini magharibi hadi Pwani ya kusini mashariki mwa China, kutoka kazi ya uongozi kwenye maeneo ya vijijini hadi kwenye uongozi wa taifa, Bw. Xi amefanya kazi zote za kisiasa na kupata uelewa wa kina wa hali ya nchi na watu wake. Bw. Xi amewahi kufanya kazi katika miji mbalimbali ikiwa ni pamoja na Shanghai na mikoa ya Shaanxi, Hebei, Fujian na Zhejiang akiwa ofisa wa Chama au wa serikali, ikiwa ni pamoja na kipindi alichofanya kazi jeshini, kabla ya kuja Beijing kuwa mwenyekiti wa kazi za kila siku za ofisi ya sekretarieti ya Kamati Kuu ya Chama. Alikuwa anajua vizuri kabisa umuhimu wa kuimarisha Chama na kusisitiza mara kwa mara kuwa Chama kinatakiwa kusimamia nidhamu yake kwa kufuata vigezo vikali. Chini ya uongozi wake, kanuni na taratibu mbalimbali za ndani ya Chama zilipitishwa.
Amekuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa Chama kinatakiwa kusimamia mwenendo wake na kujiendesha kwa nidhamu kali. Katika semina ya kwanza ya mafunzo ya Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya awamu mpya ya Chama, alisema “Kitu huoza kwanza halafu wadudu wanakua juu yake”1, “Mambo mengi halisi yameonyesha kuwa ufisadi sasa unakithiri; na kama hautazuiwa Chama chetu na nchi yetu vitakuwa hatarini. Tunatakiwa kuwa na macho sana!”
Bw. Xi anatetea sana “uchunguzi na utafiti kufanywa kwenye mchakato wote wa kutoa maamuzi”, pia anasisitiza kuwa maofisa wote wanatakiwa kwenda kwenye jamii za mashinani na kujua maoni ya watu na kujua wanayotaka ni nini, wanayofuatilia zaidi ni nini, wana wasiwasi zaidi juu ya nini na wanalalamika zaidi nini, ili kufanya uchunguzi na utafiti zaidi juu ya masuala husika na hatimaye kuyatatua.
Novemba 25, 2013, Xi Jinping akishikana mkono kwa upendo na mzee mwenye umri wa miaka 83 Wang Kechang kwenda kutembelea nyumbani kwake katika kijiji cha Zhu cha Wilaya ya Caozhuang ya eneo la Yimeng lililokuwa kituo cha zamani cha mapinduzi mkoani Shandong
Mwanzoni mwa mwaka 2008, Bw. Xi aliongoza kikundi kilichosimamia mafunzo ya nchi nzima na kutekeleza mtazamo wa kujiendeleza kwa njia ya kisayansi ndani ya Chama. Mpango huo wa miezi 18 ulisaidia kujenga maelewano kuhusu mtazamo wa kujiendeleza kwa njia ya kisayansi katika kuleta maendeleo kwa Chama na kwa taifa zima na kufanya wazo hilo kuwa nguvu kubwa ya kuhimiza maendeleo ya uchumi na jamii.
Bw. Xi pia ni kiongozi wa kikundi cha kuandaa rasimu ya ripoti ya Mkutano Mkuu wa 18 wa Chama na Kikundi cha marekebisho ya Katiba ya Chama, nyaraka mbili hizo zilipitishwa na Mkutano Mkuu wa 18 wa Chama na kuwa miongozo muhimu kwa maendeleo ya siku za baadaye ya China.