HEBU SOMA KITU HICHI ALICHOANDIKA MH MAHANGA
Ninavyojua mimi ni kwamba kama mtu hawezi kupeleka malalamiko yenye ushahidi fulani (hata kama si kamili) kwenye vyombo vya dola, ni vigumu sana vyombo hivyo kufanyia kazi tuhuma hizo. Kwa mtazamo wako unataka wananchi waachane na mkondo huu wa sheria na walalamike na kuwashitaki wanaodhani ni waovu kwa umma! Ili iweje? Wapigwe mawe? Wazomewe ili waache ufisadi? Kwa njia hii tuna hakika wataacha? Au nchi itakuwa salama? Mimi nadhani hii ni hatari.
Kwa mtazamo wako na hao wengine ni kwamba Tanzania kwa utawala bora ni sifuri kabisa na sasa wananchi wamekosa imani na serikali, na mahakama na vyombo vyote vya dola, na sasa wako tayari kuchukua mkondo wa mob justice. Je, mnataka wananchi waingie mitaani wawapige mawe wanaodhaniwa mafisadi au watawala wabovu, au wawatoe Ikulu kwa nguvu watawala waliopo sasa? Na hii eti ni kwa sababu wakifuata mkondo wa sheria kwa kutoa ushahidi polisi, takukuru na mahakamani ushahidi utaharibiwa na dola au hautafanyiwa kazi!
Huo mtazamo kwamba nchi hii haina utawala bora kiasi hicho mimi sikubaliani nao, na hata taasisi za kimataifa zinazopima utawala bora katika nchi mbalimbali hawakubaliani na mtazamo wako huo kwamba TZ ni ya mwisho mwisho katika utawala bora. Kwa kweli kinyume chake ndiyo kweli, kwamba TZ inasifiwa kwa jitihada zake za utawala bora kulinganisha na nchi nyingi za Afrika, hata zote zinazoendelea duniani. Ushahidi huu hata wewe unaujua.
Vile vile yaonekana wewe na wenzako mnadai kwamba serikali ya TZ haijali kabisa matatizo na kero na umasikini wa wananchi wake, bali matumbo ya watawala na washikaji wao. Hili nalo si kweli, ingawa suala la rushwa (kama ilivyo kwa nchi karibu zote duniani) bado ni tatizo hapa kwetu. Lazima tuendelee kukemea na kupiga vita rushwa kwa kufuata utawala wa sheria na haki za raia wote.
Lakini juhudi za serikali kuboresha huduma za jamii na kupambana na umasikini (kilimo, elimu, afya, maji, miundombinu na kupunguza umasikini nchini na kusaidia ajira hasa za kujiajiri, na hata kupambana na hiyo rushwa) ni kubwa sana na zinaonyesha jinsi serikali inavyojali wananchi wake. Angalia mgawanyo wa bajeti ya Taifa kwenye sekta hizo kila mwaka.
Wewe Ngurumo unajua pia kwamba nchi na taasisi wafadhili duniani hawapeleki misaada kwa nchi ambazo serikali yake haipangi bajeti yake kwa vipaumbele vya kulenga wananchi wake (pro-people budget) wala nchi ambapo utawala bora ni zero. Lakini angalia jinsi TZ inavyopata misaada mingi kuliko nchi nyingi kutokana na vigezo hivyo kuwaridhisha wafadhili. Hivi wao wameshindwa kuona hayo mnayoyaona nyie ya utawala mbovu na kutowajali wananchi? Hapana, sikubaliani na hilo.
Kuhusu ushahidi wa Dr. Slaa kukataliwa Bungeni, hili sina hakika nalo sana, lakini sijui kwanini hakupeleka ushahidi huo polisi au takukuru? Wangeziharibu? Huwezi kupeleka ushahidi kama huo ukaacha kubaki na nakala zako.
Kwamba tunapokuwa serikalini hatujui matatizo ya wananchi mpaka ati nije niache ubunge na uwaziri nirudi kuwa mwananchi wa kawaida ndipo nijue shida zao, si kweli. Tunazijua sana kero hizo (tunaishi nao) na zinatuumiza vichwa sana. Kiongozi mzuri ni yule anapotaka uongozi wa watu ajue anakwenda kushughulikia kero za hao wananchi, na si masilahi yake. Na mimi naamini asilimia kubwa sana ya viongozi wetu ni wa aina hiyo. Wanajali shida za wananchi.
Lakini hapa ninaloliona ni wananchi wengi kupiga siasa muda wote, badala ya kungojea msimu wa uchaguzi wafanye maamuzi ya kuchagua viongozi/chama kulingana na ahadi walizotoa, ili kabla ya hapo wajizatiti kufanya kazi kwa bidii kujiondolea umasikini. Tatizo ni CCM kuwakera watu wanaodhani ni muda muafaka kubadili chama tawala, lakini bila kungoja kutumia sanduku la kura. Tatizo ni kuwakosanisha wananchi na serikali/chama tawala kwa kushikilia mambo au jambo ambalo kwa ujumla wake halina tija kubwa sana kwa watanzania walio wengi bali lina mtazamo wa ubinafsi, chuki, wivu na uelekeo wa kisiasa.
Milton