The Sheriff
JF-Expert Member
- Oct 10, 2019
- 747
- 2,112
Picha: Mafuriko ni miongoni mwa athari nyingi zinazoletwa na Mabadiliko ya Tabianchi
Tafiti zinaonesha kuwa mabadiliko ya tabianchi bado hayajapewa kipaumbele kikubwa katika chaguzi nyingi za Afrika (Tanzania ikiwa miongoni mwazo), licha ya athari zake kubwa barani humo. Masuala yanayopewa uzito mkubwa wakati wa kampeni ni yaleyale ya siku zote kama vile ajira, elimu, huduma za afya, na huduma za nyingine za kijamii, huku mabadiliko ya tabianchi yakiachwa pembeni.
Kwa mfano, katika uchaguzi wa Nigeria wa mwaka 2023, licha ya mafuriko makubwa yaliyowafanya mamilioni ya watu kukosa makazi, wagombea urais walijikita zaidi kwenye masuala mengine, huku mada za tabianchi zikigusiwa kwa kiwango kidogo sana. Wanaharakati nchini humo walibainisha kuwa ukosefu wa uelewa wa kina miongoni mwa watunga sera kuhusu umuhimu wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni changamoto kubwa, na raia wengi waliona mada hizi zikitelekezwa au kuzungumzwa kijuujuu tu.
Mashirika kama Umoja wa Afrika (African Union) na Jukwaa la Uchumi (World Economic Forum) yanasukuma sera za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, yakitambua uhusiano mkubwa kati ya uharibifu wa mazingira na changamoto za kijamii na kiuchumi zinazoikumba Afrika.
Hata hivyo, si tu kuwa masuala hayo hayapewi kipaumbele katika majukwaa ya kisiasa, lakini pia uelewa wa mabadiliko ya tabianchi miongoni mwa wananchi katika bara la Afrika bado upo chini. Kwa mujibu wa utafiti wa Afrobarometer mwaka 2019, uelewa wa mabadiliko ya tabianchi unatofautiana sana baina ya nchi, huku maeneo ya mijini yakiwa na uelewa wa juu zaidi kutokana na upatikanaji bora wa taarifa. Jamii za vijijini mara nyingi hazina uelewa wa kutosha, ingawa zinakabiliwa moja kwa moja na athari za tabianchi kama ukame na mafuriko, hata kama hazihusishi hali hizo na mabadiliko ya tabianchi.
Utafiti huo pia unaonesha kuwa ni mmoja tu kati ya Waafrika wanne ambaye anafahamu kikamilifu; yaani ameisikia kuhusu mabadiliko ya tabianchi, anatambua kuwa yana madhara mabaya, na anakubali kwamba yanachochewa angalau kwa sehemu na shughuli za binadamu.
Hali Ipoje Tanzania?
Ripoti kuhusu mabadiliko ya tabianchi kama suala la msingi katika chaguzi nchini Tanzania zinaonesha kuwa mada hizi hazipati kipaumbele kikubwa katika kampeni za kisiasa. Waandishi wa habari wa mazingira na wataalamu wameonesha wasiwasi kwamba mijadala ya kisiasa nchini Tanzania mara nyingi inapuuza masuala ya mazingira, licha ya nchi kuwa na hatari kubwa ya maafa yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi kama vile ukame na mafuriko.
Hata hivyo, ingawa kuna sera na mipango ya kushughulikia mabadiliko ya tabianchi, utekelezaji wake umekuwa mdogo. Kwa mfano, utegemezi wa Tanzania kwa misaada ya kigeni kwa ajili ya miradi ya mazingira na ukosefu wa fedha maalum za kitaifa unaonesha pengo katika kipaumbele cha kisiasa.
Wanaharakati wa mazingira nchini Tanzania wanasisitiza kwamba masuala ya tabianchi bado hayaonekani kama masuala yanayoweza kushawishi kura, na kuna hitaji kubwa la kuongezeka kwa elimu ya umma kuhusu uhusiano kati ya mabadiliko ya tabianchi na maendeleo. Kutopewa umuhimu huko kunaonesha ukosefu wa kuingizwa kwa masuala ya mazingira katika ajenda za maendeleo ya kitaifa.
Tunachopaswa kufanya
Uhamasishaji mkubwa na kujitoa kwa viongozi wa kisiasa ni muhimu ili kufikia maendeleo makubwa, pamoja na kuelimisha umma kuhusu jinsi mabadiliko ya tabianchi yanavyoweza kuathiri maendeleo na maisha ya kila siku. Mijadala hii ni umuhimu zaidi wakati wa chaguzi, kwani sera za tabianchi zinaweza kushughulikia changamoto za mazingira na kijamii ambazo nchi inakutana nazo.
Ni muhimu mijadala ya mabadiliko ya tabianchi Iwe ya kina na ya dhati katika mikutano ya kisiasa. Wananchi wanapaswa kufahamishwa kuwa suala hili si la magharibi pekee, bali ni changamoto inayohusiana moja kwa moja na maisha yao ya kila siku katika mitaa na vijiji vyao. Hii inahitaji wanasiasa waeleze waziwazi changamoto zilizopo, hatua zinazochukuliwa, kama vile mipango ya kuhifadhi mazingira, kukabiliana na athari za tabianchi, na kuhakikisha kuna maendeleo endelevu.
Wanasiasa hawapaswi kujikita tu kwenye mazungumzo ya mazingira wakati kuna miradi inayowaletea ufadhili kutoka nje. Badala yake, wanapaswa kuweka ajenda hii kama kipaumbele cha sera zao, ikiwemo kuonesha mshikamano na wananchi katika kutafuta suluhu za mabadiliko ya tabianchi kupitia sera za kitaifa zinazotekelezeka.
Kuna haja ya kuhakikisha elimu ya mabadiliko ya tabianchi inawafikia watu wa kawaida kwa lugha rahisi na mifano halisi inayowaonesha athari zake na nafasi yao katika kuleta suluhu. Yote haya yakifanyika kwa usahihi, tutathibitisha kuwa hakuna ukweli kwamba sera za mazingira haziwezi kushawishi kura, kwani wananchi wanapofahamu athari na suluhu zinazowezekana, wanaweza kuunga mkono wanasiasa wanaoonesha dhamira ya dhati ya kushughulikia changamoto hii.
Jambo hili ni ajenda ya msingi inayogusa kila nyanja ya maisha na uchumi wa taifa. Kuipa uzito ajenda ya mabadiliko ya tabianchi si tu kwamba kutawapatia kura, bali pia kutawafanya wawe sehemu ya kizazi cha viongozi kinachochukua hatua kwa ajili ya mustakabali wa vizazi vijavyo.
Namalizia kwa kusema: Enyi wanasisa wa Tanzania, msipuuze Sera za Mazingira katika kampeni zenu za kisiasa majukwaani kwa kudhani hazishawishi kura. Mabadiliko ya Tabianchi ni kipaumbele kwa Wapiga Kura wote kwani yanamuathiri kila Mtanzania kwa nafasi yake. Watanzania wanahitaji kuelimishwa vizuri tu ili watambue walipo, wanapokwenda na namna bora ya kufika huko.