Parabolic
JF-Expert Member
- Dec 3, 2013
- 2,922
- 3,252
Wakati Serikali imezindua Mpango Mkakati wa Kisayansi wa Kukuza Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (2025/26–2030) kwa lengo la kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 watoto wote wa Tanzania wanamudu stadi za msingi, wadau wametakiwa kutekeleza mwongozo wa kitaifa wa utoaji wa chakula na lishe kwa wanafunzi.
Hayo yameelezwa leo Machi 2 na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir alipokuwa akizundua Kampeni ya Kikombe cha Ndoto jijini Dar es Salaam.
Kampeni hiyo inalenga kuunga mkono utekelezaji wa ajenda ya kitaifa ya Kusoma, Kuandika na Kuhesabu kwa kuwapatia chakula wanafunzi wawapo shuleni.
Kampeni hiyo inakwenda sambamba na Maadhimisho ya Siku ya Utoaji wa Lishe shuleni ya Afrika inayoadhimishwa kila ifikapo Machi 1.
“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuipa kipaumbele sekta ya elimu kupitia uwekezaji katika miundombinu, walimu na mazingira bora ya kujifunzia. Hata hivyo juhudi hizo haziwezi kufanikiwa ikiwa mwanafunzi anasoma akiwa na njaa.
“Hivyo utoaji wa chakula shuleni utaongeza uandikishaji, mahudhurio umakini darasani na ufaulu, huku ukipunguza utoro.
Kwa mantiki Serikali inaendelea kusisitiza utekelezaji wa mwongozo wa kitaifa wa utoaji wa chakula na lishe kwa wanafunzi, walimu wa elimu ya msingi sambamba na Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Sera ya Afya ya 2007 na Mpango wa Taifa wa Lishe wa sekta Jumuishi,” amesema Wanu.
Awali akizungumza, Mkurugenzi wa Mtendaji wa Shirika la Uwezo Tanzania lililoibua kampeni hiyo, Baraka Mgohamwende amesema lengo ni kuwajengea wanafunzi mazingira wezeshi a kujisomea.
“Mtoto anayepata kikombe cha uji asubuhi anaingia darasani akiwa na nguvu, ana uwezo wa kuzingatia masomo, na ana nafasi kubwa zaidi ya kumudu kusoma, kuandika na kuhesabu mapema. Hivyo, Kampeni ya Kikombe cha Ndoto si kampeni ya chakula tu; ni sehemu ya kuunga mkono utekelezaji wa ajenda ya kitaifa ya KKK.
“Kikombe cha Ndoto ni wazo lililozaliwa hapa hapa Tanzania. Ni mpango wa kizalendo, unaotokana na uhalisia wetu na unaojengwa juu ya mshikamano wa Watanzania. Tunaamini kuwa hatupaswi kusubiri kila suluhisho litoke nje ya nchi yetu,” amesema.